Friday, September 13, 2013

MOTO WATEKETEZA NYUMBA MBWENI,WATOTO NA WAZAZI WANUSURIKA

Ni kuamkia leo asubuhi ya Tar.14/09/2013 huko mbweni pembezoni mwa jiji la Dsm,nyumba moja ya Ofisa mmoja wa UN Mtanzania huko SUDAN imeteketea kabisa kabisa kwa moto usiku wa Manane.Inasemekana moto umeanzia kwenye chumba cha watoto na haijafahamika kama ni hitirafu ya umeme au la?
Bahati mbaya sana hakuna kitu kilichookolewa hata kimoja,mali zote zimeteketea kwa moto na hakukuwepo na jitihada zozote za kuuzima kutokana na muda wa moto ulipoanza pia majirani hawakuwa na uwezo wa kudhibiti moto huo kwa sababu ulishika eneo kubwa la nyumba hiyo.

OLOYA KUICHEZEA SIMBA AU YANGA BAADA YA KUKATAA KWENDA THAILAND

Oyola akiwa katika purukushani
Moses Oloya ameikataa ofa ya kwenda Thailand na kuzipambanisha kwa mara nyingine klabu za Tanzania; Simba na Yanga.
Oloya, ambaye alikuwa anaichezea Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, sasa yupo Uganda baada ya timu hiyo kushushwa daraja mpaka la tatu, ingawa mkataba wake unafika kikomo mwezi ujao.
Mmoja wa mawakala wa Oloya aliliambia Mwanaspoti jana Ijumaa kutoka Kampala kuwa mchezaji huyo amepata ofa ya kwenda Thailand, lakini ameikataa kwa sababu anadhani itakuwa ngumu kwake kupata timu ya Ulaya.
“Amesema kuwa anaangalia kati ya Simba na Yanga ni timu gani ambayo itampa masilahi mazuri, pia itakuwa tayari kumruhusu kwenda Ulaya akipata timu,” alisema wakala huyo ambaye hakutaka kutajwa kwa sasa.
Wakala huyo alisisitiza kuwa Oloya anafikiria kucheza Ulaya, lakini kwa sababu hana timu kwa sasa, yupo tayari kujiunga na Simba au Yanga, lakini atakuwa tayari kujiunga na timu ambayo itamruhusu kufanya majaribio Ulaya iwapo atapata timu. Hataki vikwazo.
“Hata akija Simba au Yanga itakuwa ni sehemu ya kupita tu na ndiyo maana anataka mkataba wake uwe wazi kwamba ataruhusiwa kwenda Ulaya iwapo atapata timu huko,” alisema wakala huyo.
Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hanspope amekuwa akisisitiza kuwa wamefanya mazungumzo ya kutosha na mchezaji huyo na kwamba atatua Msimbazi wakati wowote.
Hata hivyo, Yanga nao hawako kimya na ndio maana kuna wakati walimtumia tiketi ya ndege Vietnam, lakini alishindwa kuja Dar es Salaam baada ya viongozi wa klabu ya Saigon kumzuia.

EMMANUEL OKWI AJIUNGA NA TIMU YA URA YA UGANDA


Emmanuel Okwi akiwatoka wachezaji wa timu pinzani 
Straia wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi amejiunga na URA ya Uganda ili kujiweka fiti akisubiri hatma yake kwenye klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Okwi amegoma kuichezea Etoile du Sahel mpaka itakapommalizia malipo yake ya kusaini mkataba pamoja na kumlipa malimbikizo ya mishahara ya miezi mitatu.
“Nimetulia kwanza nione suala langu linaendaje na suluhisho ni nini. Ninataka sana kurudi uwanjani kucheza soka la ushindani,” alisema Okwi.
“Ishu ni kwamba hawajanimalizia pesa ya kusaini mkataba pamoja na mishahara yangu ya miezi mitatu sasa,” alisema Okwi ambaye anaendelea kujinoa na URA ingawa haruhusiwi kucheza mechi ya mashindano kwa sababu ana mkataba wa miaka mitatu na Etoile du Sahel.
Wakala wa mchezaji huyo amesema kwamba wanaendelea na mazungumzo na Etoile ili kutatua suala la Okwi ingawa habari za ndani zinasema kwamba anafanya mpango wa kumpeleka kwa mkopo kwenye klabu moja ya Daraja la Kwanza Ulaya.
Okwi aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda na kucheza dhidi ya Senegal wiki iliyopita katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia na kushuhudia kikosi cha Kocha Sredojevic Milutin ‘Micho’ kikiambuliwa kipigo cha bao 1-0.
Wakati Okwi akiwa na malumbano hayo na klabu hiyo ya Tunisia, Simba ambayo ilimuuza nayo inasubiri malipo ya Sh480 milioni kutoka kwa Etoile du Sahel ambayo iliahidi kulipa fedha hizo kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetoa mpaka mwisho wa mwezi huu Simba iwe imelipwa.

GAZETI LAKO LA MTANZANIA LA LEO JUMAMOSI HILI HAPA

Banner 


HII NI RATIBA YA LIGI KUU UINGEREZA 'BARCLAYS PREMIER LEAGUE'

11:45Manchester UnitedvCrystal Palace
14:00Aston VillavNewcastle United
14:00FulhamvWest Bromwich Albion
14:00Hull CityvCardiff City
14:00Stoke CityvManchester City
14:00SunderlandvArsenal
14:00Tottenham HotspurvNorwich City
16:30EvertonvChelsea

PICHA MBALIMBALI ZA JANA KATIKA FIESTA PANDE ZA DODOMA


Haaaa haaaa...ukitaka kubana pua kabane nyumbani kwenu,hapa ni hip hop tuuu.....Msanii wa Bongofleva Ney wa Mitego wakioneshana umahiri umwamba wa jukwaani na msanii mwenzake  Dimond  kupitia wimbo wa Muziki Gani.
 Mmoja wa wasanii wanaokuja kwa kasi kwenye anga ya muziki wa Bongofleva a.k.a hip hop,Stamina akiwaimbisha wakazi wa Dodoma na vitongoji vyake waliojitokeza kwa wingi usiku huu ndani ya uwanja wa Jamuhuri,wakati tamasha la Serengeti Fiesta 2013 likiendelea.
 Msanii mahiri ambaye kwa sasa anasumbua vilivyo anga ya muziki wa Bongofleva,Diamond akiwaimbisha mashabiki wake usiku huu kwenye tamasha la serengeti fiesta 2013,linalofanyika usiku huu kwenye uwanja wa Jamuhuri.


 Sehemu ya mashabiki wakishangweka vilivyo usiku huu ndani ya tamasha la Serengeti Fiesta 2013.
Mmoja wa wakongwe wa muziki wa kizazi kipya kutoka kundi la Wateule Skwadi,atambulikae kwa jia la kisanii Mchizi Mox akiimba jukwaani usiku huu.  
Maelfu ya Watu wakiwa kwenye uwanja wa jamuhuri,usiku huu wakishangweka na tamasha la Serengeti Fiesta 2013.
Mkali mwingine wa Bongofleva,Dullysykes akiimba jukwaani usiku huu wakati tamasha la Serengeti fiesta likiendelea.
 Young Killer na Stamina  kama kawaida yao wakilishambulia jukwaa la fiesta usiku huu,huku maelfu ya watu wakiwa ndani ya uwanja wa Jamuhuri,mkoani 
 Ni burudani murua kabisa usiku huu ndani ya uwanja wa Jamuhuri,wakati tamasha la Serengeti Fiesta 2013 likiendelea
 Mwanadada ambaye wengi wanadai amerithi viuno na sauti kutoka mwanamuziki Ray C,anaitwa Rachael kutoka nyumba ya vipaji a.k.a THT akiimba jukwaani huku akionesha umahiri wake wa kukata mauno.
Mkongwe wa muziki wa kizaz kipya a.k.a Bongofleva Afande Sele a.k.a Baba Tunda a.k.a Simba Mzee akidhihirisha ukongwe juu ya steji ya tamasha la Serengeti linalofanyika usiku huu ndani ya uwanja wa Jamuhuri mkoani Dodoma,ambapo maelfu ya watu washabiki wamejitokeza kushuhudia tamasha hilo ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka.
 Makamuzi yakiendelea usiku huu 
 sehemu ya umati wa watu. 
 Dj Mully B akikamua mangoma
 wakishangweka.
Kutoka TMK Wanaume Halisi,alyewahi kuwa ndani ya kundi la mabaga flesh akishusha mistari yake mbele ya mashabiki wake usiku huu.

CHANJO INAYOANGAMIZA 'VVU' IMEPATIKANA

Wanasayansi nchini Marekani wamegundua chanjo ambayo wanaamini itaweza kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa binadamu.
Katika majaribio ya chanjo hiyo, wanasayansi hao wameelezea kuwa imeonyesha mafanikio kwa kuangamiza kabisa virusi wanaofanana na VVU kwa nyani.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limechapisha kwenye tovuti yake kuwa baada ya kubaini hilo sasa wamekusudia kufanya majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu.
Likinukuu taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la kisayansi linaloitwa; Nature, lilimnukuu Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Oregon, nchini Marekani akisema walijiridhisha kuwa chanjo hiyo iliangamiza virusi vyote kwenye mwili wa nyani.
Virusi hao jamii yake inafanana sana na VVU wanajulikana kama Simian Immunodeficiency Virus (SIV) ikiwa na maana ni virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga ya kujikinga na maradhi kwa nyani.
Taarifa za kisayansi zinaonyesha kwamba SIV ni virusi ambao wamekuwa wakienea kwa njia ya kujamiiana miongoni mwa vizazi vya nyani na vilibadilika baada ya kuambukizwa kwa binadamu vikawa vimezaa VVU.
Wanasayansi hao wanasema kati ya nyani 16 waliopewa chanjo hiyo, waliyoipa jina la Cytomegalovirus (CMV),tisa walipona kabisa maradhi ya SIV.
Mtaalamu wa Taasisi ya Chanjo na Jeni katika Chuo Kikuu cha Oregoni, ambaye alihusika kwenye utafiti huo, Profesa Louis Picker aliielezea chanjo hiyo kuwa ni ya kutia moyo ukilinganisha na nyingine ambazo zimewahi kufanyika.
“Katika chanjo nyingi ambazo ziliwahi kuonyesha mafanikio ya kuangamiza virusi ni kwamba kuna baadhi ya seli virusi walibakia,” alisema Profesa Picker, akifafanua:
“Lakini kwa chanjo hii tulichunguza sehemu nyingi nyeti katika mwili wa nyani tukagundua kwamba hakuna kirusi aliyebakia.”
Alisema chanjo yao wameiamini kutokana na uwezo wake wa kupenya maeneo mbalimbali ya mwili kiasi kwamba siyo rahisi kirusi kubakia.
Wanasayansi hao walisema kwa kawaida nyani ambaye ameambukizwa SIV hufa ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Mwananchi

HABARI YA PADRI KUMWAGIWA 'TINDIKALI' HUKO ZANZIBAR HII HAPA

Padri Anselmo Mwang'amba baada ya tukio la kumwagiwa tindikali.
Padri Anselmo Joseph Mwang'amba wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, mkoa wa mjini magharibi visiwani Zanzibar anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 50, amemwagiwa maji yanayodhaniwa kuwa ni tindikali alpoikuwa internet café majira ya saa tisa alasiri maeneno ya Mlandege.

Kwa mujibu wa kamanda wa Jeshi la Polisi mjini Magharibi, Mkaadanu Hassan Mkaadanu, Padri huyo alipigiwa simu, na alipokuwa akitoka nje ili kuisikiliza vema simu, hapo ndipo tukio likatokea, ambao haijajulikana kama ni mtu au kundi la watu lililofanya tukio hilo.

Taarifa za hivi sasa zinaeleza kuwa Padri Mwang'amba amelazwa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, wodi ya Mapinduzi mpya, ambayo ni wodi maalum kwa ajili ya viongozi.

Padri huyo amefanya kazi kwa muda wa zaidi ya miaka 35 huko Zanzibar, ambapo baada ya taarifa hizi kupatikana, askofu mkuu wa kanisa katoliki Zanzibar, Agustino Shao ameelezwa kujifungia kuanzia muda huo na kuendelea kuwepo hadi muda huu

Kwa hivi sasa taharuki ni kila mahali, hakuna kinachoeleweka, wakristo wakieleza kuwa hawana pa kukimbilia kwa kuwa ni zaidi ya miezi minne kupita tangu Padre Everist Mushi auawe na bado mwenendo wa kesi haueleweki, na kwamba sasa hawajui pa kwenda.

Kamanda Mkaadamu amekiri kuwa tindikali ni tatizo, na amesema kuwa wanaendelea kufanya jitihada ili kila kitu kiwe wazi.

UMOJA WA NCHI ZA AFRIKA 'AU' WATOA YAO KUHUSU ICC DHIDI YA KENYA

Muungano wa Afrika sasa unataka mahakama ya kimataifa ya ICC kusitisha kesi za Naibu rais wa Kenya William Ruto, Rais Uhuru Kenyatta na mwandishi Joshua Arap Sang katika mahakama hiyo hadi pale ombi lake kwa mahakama hiyo kutaka kesi hizo kurejeshwa nyumbani kuamuliwa.
AU pia inataka Bwana Ruto na Rais Kenyatta kuruhusiwa kuchagua vikao wanavyotaka kuhudhuria wakati wa kusikizwa kwa kesi zao kutokana na majukumu yao ya kikatiba.
Kwenye barua iliyoandikwa kwa ICC, AU inasema kuwa mahakama hiyo mwanzo ilipaswa kuamua ikiwa itaweza kuhamishia kesi hizo nchini Kenya kabla ya hata kuanza kuzisikiliza.
Katika barua yake kwa ICC, AU pia Imegusia swala la rufaa ambayo imewasilishwa katika mahakama hiyo na mwendesha mkuu wa mashtaka Fatou Bensouda dhidi ya kumruhusu bwana Ruto kuhudhuria tu baadhi ya vikao akisema kuwa majaji wangemlazimisha naibu rais Ruto kuhudhuria vikao vyote vya kesi yake kabla ya rufaa kuamuliwa.
Muungano huo umeelezea kuhusu mikutano mikuu miwili ya usalama inayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu ambayo Rais Kenyatta hataweza kuhudhuria kwa sababu kesi ya naibu rais William Ruto itakuwa inasikilizwa ICC.
AU imeongeza kuwa kesi hizo zitahujumu jukumu la Kenya katika ukumbi wa kimataifa ikisisitiza kuwa hazipaswi kuathiri majukumu ya viongozi hao wawili.
AU inasema kuwa licha ya kuwa Kenya imekuwa ikiheshimu mahakama hiyo, inapaswa kufanya hivyo kwa kuzingatia Katiba yake

BAADA YA KUBAKA NA KUSABABISHA KIFO, SASA ZAMU YAO KUNYONGWA

Mahakama nchini India imewahukumu wanaume wote wanne kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumuua mwanamke katika basi katika mji mkuu wa India Delhi mwezi Desemba mwaka jana.
Mmoja wao aliangua kilio na kuanguka baada ya kutangazwa kwa hukumu dhidi yao .
Msichana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 23 aliumizwa sana na baada ya wiki moja alifariki kutokana na majeraha .
Karibu miezi 9 baada ya ubakaji ulioitikisa India, jaji ametoa hukumu kwa wanaume wote wanne ambao tayari walikuwa wamepatikana na hatia ya uhalifu .
Wendesha mashtaka walikuwa wamewaombea hukumu ya kifo wakisema ingetoa ishara muhimu kwamba uhalifu wa aina hiyo hautakubalika kamwe .
Familia ya mwanamke huyo pia waliomba wanaume hao wanyongwe .
Lakini mawakili watetezi wa wanaume hao walipinga mapendekezo ya hukumu ya kifo , wakisema wateja wao hawakuwa na rekodi za uhalifu awali na kwamba wanastahili kusamehewa .
Kifo cha mwanafunzi huyo mwezi Disemba mwaka jana kilisababisha maandamano makubwa ya upinzani kote nchini India , yaliyoilazimisha serikali kubadili sheria zilizokuwepo za uhalifu wa ngono
BBC

AJIKOJOLEA NDANI YA CHUMBA CHA MAHAKAMA

Manfred Adam anayekabiliwa na kesi ya kutishia kuua katika hali isiyotarajiwa amelimwaga kojo katika Mahakama ya Mwanzo na kuleta vurugu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa meza ya Mahakama ya Mwanzo ya Mazimbu mkoani  Morogoro mwanzoni mwa wiki hii.
 
Katika vurugu hizo zilizolazimisha shughuli za mahakama kusimama kwa muda wa saa mbili, askari wawili waliokuwepo eneo la tukio walishindwa kumdhibiti Manfred, kitendo kilichofanya kuitwa kwa wengine zaidi ambao waliweza kumtuliza mtuhumiwa huyo.
Hakimu Alisile Mwankejela aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo namba 322 ya mwaka 2013 pamoja na makarani wa mahakama hiyo walitimua mbio kuhofia kudhurika, mara tu baada ya vioja hivyo kuanza kufuatia kuahirishwa kwa kesi ya mtuhumiwa huyo ambayo itasomwa tena Septemba 24,    mwaka huu.
“Ni kweli tukio hilo limetokea baada ya kuhairisha kesi, mshitakiwa huyo alikojoa mahakamani na kufanya vurugu kubwa,” alisema hakimu huyo alipokutwa ofisini kwake.
Karani wa makahama hiyo, Kidawa Minangu alisema

“Manfed asubuhi aliletwa hapa kwa ajili ya kesi yake, alipofika tuliita jina lake na aliingia mahakamani na kusomewa mashitaka yake, kesi ilipohairishwa cha ajabu alivua suruali na kukojoa hapa mahakamani, tuliwaita askari wawili wa hapa mahakamani walipomkamata alianza kupigana nao na kuvunja meza za mahakama ndipo tulipoamua kuomba msaada wa askari wengine ambao walifika na kumdhibiti.”

CCM YAPOTEZA NAFASI YA MEYA MJINI MUSOMA

Diwani wa kata ya mwisenge kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo mh. Bwire Nyamwero leo ametangazwa kuwa naibu meya wa halmashauri ya manispaa ya Musoma baada ya kumshinda diwani wa kata ya Nyasho kwa tiketi ya CCM Goldon Mumbala katika uchaguzi wa kumtafuta naibu meya wa manispaa ya Musoma. 

Mkurugenzi wa manispaa ya Musoma ahmed sawa ametangaza bwire kama mshindi na kwamba amemshinda mpinzani wake kwa kura 11 kwa 5.
Jumla ya madiwani 17 wameshiriki katika zoezi hilo ambapo kura moja imeharibika kati ya kura 16 zilizopigwa.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi mh. bwire amesema amefurahi kuchaguliwa tena katika nafasi hiyo na hivyo kuupongeza kamati ya uchaguzi huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa baraza la madiwani.
Amewaomba wananchi wamuunge mkono ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
naye diwani mumbala wa chama cha mapinduzi ameyakubali matokea hayo na kuahidi kushirikiana kwa moyo mmoja na naibu meya huyo ili kutekeleza shughuli mbalimbali za baraza hilo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na baraza ili kufanikisha ipasavyo maendeleo ya halmashauri.
Baada ya uchaguzi wa naibu meya baraza hilo la madiwani liliahirisha kikao hicho kwa muda ambapo baadae kiliikaa tena kwaajili ya kufanya uchaguzi wa kamati za kudumu ambapo Mh. Haile S. Sarai. alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya mipango miji maliasili na mazingira
Hata hivyo kamati ya elimu afya na huduma za jamii haikuweza kupata kiongozi wake kwa kuwa kamati hiyo haikufanya uchaguzi
kufuatia hali hiyo kamati ya elimu afya na huduma za jamii imepanga kufanya uchaguzi ndani ya siku 30 ili kumpata mwenyekiti wake

HIZI I FAIDA ZA KUTUMIA MBOGA YA MAJANI ''SPINACH''


SPINACH

1. Kinga dhidi ya matatizo ya moyo
 
2. Kinga dhidi ya matatizo ya mifupa
 
3. Kinga dhidi ya saratani (hasa saratani ya prostate)
 
4. Kinga dhidi ya matatizo ya tumbo…inapambana na seli ambazo zinaharibu utumbo


NICKI MINAJ ASHITAKIWA KWA KOSA LA 'KUCOPY NA KUPEST'

Rapa Nicki Minaj, ameshitakiwa kwa kosa la 'kucopy na kupest', kwa mujibu wa tuhuma hizo singo ya Nicki ya Starship iliyofanya vizuri mwaka 2012, alicopy kutoka kwenye kibao cha Neu Chicago kilichofanya na msanii chipukizi mmoja anayejulikana kwa jina la Clive Tanaka.

Kwa mujibu wa gazeti la Chicago Tribune, Clive amemshitaki msanii huyo kwa kuiba sehemu ya mistari yake iliyopo kwenye kibao cha Neu Chicago na kukitumia katika singo yake hiyo iliyotamba mwaka huo.

Kesi hiyo ilifunguliwa Jumanne septemba 10 mwaka huu, kwenye Mahakama ya wilaya Chicago pia imewataja Mtayarishaji RedOne, waandishi wa wimbo wa Starship kuwa nao pia walihusika katika kwenye kuiba wimbo wake

HIZI NI TIMU ZA TAIFA NA UBORA WAKE KIDUNIA ZAIDI..


bigpreview_Spain National Football Team, South Africa 2010
Shirikisho la kimataifa la soka FIFA limetoa viwango vya ubora wa timu za taifa vya kila mwezi huku vikiwa na mabadiliko kadhaa yanayoashiria kupanda na kushuka kwa viango kwa baadhi ya timu .
Viwango hivyo vinaonyesha kuwa timu ya taifa ya Hispania imeendelea kuongoza ikiwa kwenye nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Argentina ambao wamepanda kwa nafasi mbili toka nafasi ya nne kwa mwezi uliopita .
Hispania wameshikilia nafasi ya kwanza kwa karibu miaka mitatu wakiwa na rekodi ya matokeo mazuri kwenye asilimia kubwa ya michezo yake rasmi ya kiushindani na ile ya kirafiki.
Nafasi ya tatu na ya nne zimekwenda kwa Ujerumani na Italia huku Colombia ikikamilisha orodha timu tano bora duniani .
Timu ya taifa ya Ubelgiji ambayo imezidi kupanda kiwango ikiwa kwenye nafasi ya 6.
Timu ya taifa ya Ubelgiji ambayo imezidi kupanda kiwango ikiwa kwenye nafasi ya 6.
Ubelgiji ambao kwa sasa wanajivunia kuwa na kundi la wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu wanaounda timu yake ya taifa imepanda kwa nafasi nne toka nafasi ya kumi kwa mwezi uliopita wakiwa mbele ya Uruguay na Brazil zinazoshika nafasi za saba na nane .Brazil wamepanda toka nafasi ya tisa huku Uruguay wakiwa wamepanda kwa nafasi tano toka nafasi ya 11 .
Orodha ya timu kumi bora inakamilishwa na timu za Uholanzi na Croatia zinazoshika nafasi ya tisa na nafasi ya kumi . Uholanzi wameshuka kwa nafasi nne toka nafasi ya tano mwezi uliopita na Croatia wameshuka kwa nafasi mbili .
England wamezidi kushuka viwango kwa sasa wako kwenye nafasi ya 17.
England wamezidi kushuka viwango kwa sasa wako kwenye nafasi ya 17.
Timu ya taifa ya England imeendelea kushuka kadri siku zinavyozidi kuongezeka wakiwa kwenye nafasi ya 17 toka nafasi ya 13 . England waliwahi kufikia mpaka nafasi ya tatu mapema mwaka huu lakini kutokana na matokeo mabovu ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata imeendelea kushuka kwenye viwango vya ubora .
Tanzania iko kwenye nafasi ya 127 duniani sawa na nafasi ya 37 kwa bara la Afrika.
Tanzania iko kwenye nafasi ya 127 duniani sawa na nafasi ya 37 kwa bara la Afrika.
Kwa bara la Afrika viwango hivyo vinaonyesha kuwa timu ya taifa ya Ivory Coast inashika nafasi ya 19 ikiwa imeshuka toka nafasi ya kumi na nane ikifuatiwa na Ghana ambayo imeshika nafasi ya 24 kama ilivyokuwa mwezi uliopita .
Algeria , Nigeria na Mali zinakamilisha orodha ya tano bora huku Cape Verde wakizidi kupanda wakiwa kwenye nafasi ya sita . Misri , Burkina  Faso , Cameroon,Senegal  na Afrika kusini bzinamalizia top 10 ya bara la Afrika huku Tanzania ikiwa kwenye nafasi ya 37 kwa Afrika na 127 kwa Dunia ambapo imepanda kwa nafasi moja .

MFUNGWA ABAHATIKA KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA


Serikali imempa fursa ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu, mfungwa wa Gereza la Watoto lililopo jijini Dar es Salaam baada ya kumruhusu kufanya mitihani ya taifa ya darasa la saba kwenye Shule ya Msingi Ukonga.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Yusufu Kipengele, jana alisema kuwa amefanikiwa kuhitimu darasa la saba jana baada ya kuungana na wanafunzi wengine nchini kufanya mitihani hiyo akiwa chini ya ulinzi  wa askari magereza na wa polisi kuanzia juzi.
Alisema wakati anahukumiwa kwenda jela, alikuwa ni mwanafunzi wa shule moja ya msingi iliyopo wilayani Kibaha.
Alisema alisajiliwa kufanya mitihani yake katika shule hiyo na kwamba kutokana na umbali, aliombewa kuifanyika katika Shule ya Msingi Ukonga ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Alisema wakati akihukumiwa kwenda jela, namba yake ya kufanya mtihani ilipelekwa Mei mwaka huu kwenye shule aliyokuwa akisoma.
“Mwezi Mei huwezi kufanya mabadiliko ya vituo ila kutoa taarifa baraza la mitihani kama kuna tatizo kama hilo na kama kuna haja ya kulitatua kwa vyote inavyoona inafaa,” alisema.
Alisema baada ya baraza kupelekewa taarifa kuhusiana na mtahiniwa huyo liliagiza mkoa wa Pwani umtafutie shule iliyopo jirani na gereza hilo ili afanye mitihani hiyo.
Kipengele alisema kuwa baada ya kupata shule hiyo, mitihani yake ilifungwa kwenye bahasha ya peke yake na kupelekwa Kibaha kisha kupelekwa Shule ya Msingi Ukonga ambako aliruhusiwa kuifanya.
Alisema baada ya kufanya mitihani hiyo, ilipelekwa Kibaha kwenye shule alikokuwa akisoma na kuunganishwa na ya wenzake na kupelekwa kusahihishwa.
Alisema kwa siku mbili mfululizo mfungwa huyo alikuwa akitokea kwenye gereza hilo kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 12, mwaka huu na kupelekwa na askari hao kwenye kituo chake cha kufanyia mtihani na kurudishwa gerezani.
Alisema alihukumiwa kwenda jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wilayani Kibaha mapema mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu hatima yake ya kuendelea na masomo ya sekondari endapo atafaulu mitihani hiyo, alisema atalazimika kusubiri amalize kifungo.
Vilevile alisema kuwa wanafunzi 19 wenye ulemavu wa uoni hafifu nao ni miongoni mwa waliofanya  mitihani hiyo mkoani Pwani.
Kipengele alisema kuwa hakuna taarifa zozote za kuwapo kwa vitendo vya udanganyifu vilivyoripotiwa kutokea.

HII IMEANDIKWA NA GAZETI LA MWANANCHI ''ELIMU YA MSINGI IWE KIDATO CHA NNE''

Wanafunzi wa darasa la saba nchini kote jana walimaliza kufanya mtihani wa kuhitimu masomo ya elimu ya msingi. Tunafarijika kusikia kwamba mtihani huo ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu karibu nchi nzima, jambo ambalo pengine linadhihirisha kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imejifunza kutokana na makosa yaliyofanyika huko nyuma,  hivyo taratibu inaanza kutupeleka kule tunakotaka kwenda.
Kutokana na ukubwa wa nchi yetu, bado ni mapema mno kusema kwamba mambo yote yalikwenda kama ilivyopangwa, ingawa wahenga walisema siku njema huonekana asubuhi. Tulizoea kupata habari mbaya za mambo mengi kwenda mrama kila mtihani huo ulipokuwa ukifanyika, ikiwa ni pamoja na wizi wa mitihani, kucheleweshwa kwa vifaa, wasimamizi kutofika vituoni walikopangiwa na kadhalika.
Kwa siku mbili mfululizo, viongozi wa wizara hiyo katika ngazi zote nchini, wakiwamo Waziri, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo walikuwa wakizunguka katika shule mbalimbali kuhakikisha mtihani huo ulikuwa ukifanyika katika hali inayokubalika. Hii ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo viongozi wengi walikuwa wakikaa katika ofisi zenye viyoyozi wakisubiri kuletewa taarifa za mwenendo wa mitihani hiyo, pasipo kujua kwamba taarifa nyingi zilikuwa za kubuni na nyingine zilikuwa zimechakachuliwa.
Kinachotakiwa sasa ni Wizara kujielekeza zaidi katika kutatua matatizo yanayokwamisha elimu ya msingi, badala ya kuridhika tu na mipango, matamko na mikakati sio tu isiyoendana na vitendo, bali pia isiyotekelezeka hata kama inafanywa kwa nia njema. Kwa mfano, Wizara inaonekana kama imepagaa na ‘Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa’ ambao, pamoja na kufanikiwa katika nchi nyingine kama Malaysia, inabidi tafsiri na utekelezaji wake ufanywe kwa kutilia maanani mazingira tuliyomo.
Mpango huo lazima uwe na dira ili uweze kutekelezeka. Kwa mfano, wanafunzi zaidi ya 800,000 waliomaliza jana elimu ya msingi walitayarishwaje ili elimu hiyo iwawezeshe kumudu maisha yao? Je, elimu hiyo inatosha au taifa lijielekeze sasa katika kufanya elimu ya msingi kuwa kidato cha nne?  Mwaka jana wanafunzi asilimia 64 tu waliofanya mtihani huo ndio waliochaguliwa kwenda sekondari, huku asilimia 36 ikiachwa kutokomea mitaani kueneza ujinga na kugawana umaskini.
Bahati mbaya Waziri Kawambwa bado ni mateka wa takwimu zinazompa ndoto za kufaulisha wanafunzi 80 kati ya 100 ifikapo mwaka 2015 katika elimu ya msingi. Alikaririwa juzi akisema mwaka huu ufaulu utaongezeka kutoka asilimia 31 hadi asilimia 60 na kwamba ongezeko hilo litakwenda sambamba na ongezeko la madarasa. Tatizo ni kwamba anasahau kwamba suala la elimu ni mtambuka, kwa maana kwamba kuongezeka kwa ubora wa elimu kunategemea mambo mengine mengi kama vifaa vya kufundishia, vitabu, walimu bora, usafiri, mitalaa sahihi, miundombinu (mabweni, maabara, madarasa) na huduma za maji, afya, nishati, chakula na kadhalika.
Pamoja na kuwapo umuhimu wa kupanua elimu ya msingi kuwa kidato cha nne, tunadhani pia wakati umefika wa kubadilisha mitalaa ili ijikite katika kutoa elimu ya kujitegemea.
Mkazo uwekwe katika elimu ya ufundi, kwa maana ya kuhakikisha angalao kila wilaya inakuwa na chuo kimoja cha kutoa elimu stadi mfano wa VETA. Vinginevyo, majeshi tunayozalisha kila mwaka kutoka shule za msingi yatasababisha  maafa na tutabaki kulia na kusaga meno.

Zilizosomwa zaidi