Friday, September 13, 2013

OLOYA KUICHEZEA SIMBA AU YANGA BAADA YA KUKATAA KWENDA THAILAND

Oyola akiwa katika purukushani
Moses Oloya ameikataa ofa ya kwenda Thailand na kuzipambanisha kwa mara nyingine klabu za Tanzania; Simba na Yanga.
Oloya, ambaye alikuwa anaichezea Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, sasa yupo Uganda baada ya timu hiyo kushushwa daraja mpaka la tatu, ingawa mkataba wake unafika kikomo mwezi ujao.
Mmoja wa mawakala wa Oloya aliliambia Mwanaspoti jana Ijumaa kutoka Kampala kuwa mchezaji huyo amepata ofa ya kwenda Thailand, lakini ameikataa kwa sababu anadhani itakuwa ngumu kwake kupata timu ya Ulaya.
“Amesema kuwa anaangalia kati ya Simba na Yanga ni timu gani ambayo itampa masilahi mazuri, pia itakuwa tayari kumruhusu kwenda Ulaya akipata timu,” alisema wakala huyo ambaye hakutaka kutajwa kwa sasa.
Wakala huyo alisisitiza kuwa Oloya anafikiria kucheza Ulaya, lakini kwa sababu hana timu kwa sasa, yupo tayari kujiunga na Simba au Yanga, lakini atakuwa tayari kujiunga na timu ambayo itamruhusu kufanya majaribio Ulaya iwapo atapata timu. Hataki vikwazo.
“Hata akija Simba au Yanga itakuwa ni sehemu ya kupita tu na ndiyo maana anataka mkataba wake uwe wazi kwamba ataruhusiwa kwenda Ulaya iwapo atapata timu huko,” alisema wakala huyo.
Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hanspope amekuwa akisisitiza kuwa wamefanya mazungumzo ya kutosha na mchezaji huyo na kwamba atatua Msimbazi wakati wowote.
Hata hivyo, Yanga nao hawako kimya na ndio maana kuna wakati walimtumia tiketi ya ndege Vietnam, lakini alishindwa kuja Dar es Salaam baada ya viongozi wa klabu ya Saigon kumzuia.

No comments:

Zilizosomwa zaidi