Emmanuel Okwi akiwatoka wachezaji wa timu pinzani |
Okwi amegoma kuichezea Etoile du Sahel mpaka
itakapommalizia malipo yake ya kusaini mkataba pamoja na kumlipa
malimbikizo ya mishahara ya miezi mitatu.
“Nimetulia kwanza nione suala langu linaendaje na
suluhisho ni nini. Ninataka sana kurudi uwanjani kucheza soka la
ushindani,” alisema Okwi.
“Ishu ni kwamba hawajanimalizia pesa ya kusaini
mkataba pamoja na mishahara yangu ya miezi mitatu sasa,” alisema Okwi
ambaye anaendelea kujinoa na URA ingawa haruhusiwi kucheza mechi ya
mashindano kwa sababu ana mkataba wa miaka mitatu na Etoile du Sahel.
Wakala wa mchezaji huyo amesema kwamba wanaendelea
na mazungumzo na Etoile ili kutatua suala la Okwi ingawa habari za
ndani zinasema kwamba anafanya mpango wa kumpeleka kwa mkopo kwenye
klabu moja ya Daraja la Kwanza Ulaya.
Okwi aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya
Uganda na kucheza dhidi ya Senegal wiki iliyopita katika mchezo wa
kufuzu Kombe la Dunia na kushuhudia kikosi cha Kocha Sredojevic Milutin
‘Micho’ kikiambuliwa kipigo cha bao 1-0.
Wakati Okwi akiwa na malumbano hayo na klabu hiyo
ya Tunisia, Simba ambayo ilimuuza nayo inasubiri malipo ya Sh480 milioni
kutoka kwa Etoile du Sahel ambayo iliahidi kulipa fedha hizo kabla ya
mwisho wa mwezi huu.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetoa mpaka mwisho wa mwezi huu Simba iwe imelipwa.
No comments:
Post a Comment