Wanafunzi wa darasa la saba nchini kote jana walimaliza kufanya
mtihani wa kuhitimu masomo ya elimu ya msingi. Tunafarijika kusikia
kwamba mtihani huo ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu
karibu nchi nzima, jambo ambalo pengine linadhihirisha kwamba Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi imejifunza kutokana na makosa yaliyofanyika
huko nyuma, hivyo taratibu inaanza kutupeleka kule tunakotaka kwenda.
Kutokana na ukubwa wa nchi yetu, bado ni mapema
mno kusema kwamba mambo yote yalikwenda kama ilivyopangwa, ingawa
wahenga walisema siku njema huonekana asubuhi. Tulizoea kupata habari
mbaya za mambo mengi kwenda mrama kila mtihani huo ulipokuwa ukifanyika,
ikiwa ni pamoja na wizi wa mitihani, kucheleweshwa kwa vifaa,
wasimamizi kutofika vituoni walikopangiwa na kadhalika.
Kwa siku mbili mfululizo, viongozi wa wizara hiyo
katika ngazi zote nchini, wakiwamo Waziri, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu
wake, Philipo Mulugo walikuwa wakizunguka katika shule mbalimbali
kuhakikisha mtihani huo ulikuwa ukifanyika katika hali inayokubalika.
Hii ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo viongozi wengi walikuwa wakikaa
katika ofisi zenye viyoyozi wakisubiri kuletewa taarifa za mwenendo wa
mitihani hiyo, pasipo kujua kwamba taarifa nyingi zilikuwa za kubuni na
nyingine zilikuwa zimechakachuliwa.
Kinachotakiwa sasa ni Wizara kujielekeza zaidi
katika kutatua matatizo yanayokwamisha elimu ya msingi, badala ya
kuridhika tu na mipango, matamko na mikakati sio tu isiyoendana na
vitendo, bali pia isiyotekelezeka hata kama inafanywa kwa nia njema. Kwa
mfano, Wizara inaonekana kama imepagaa na ‘Mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa’ ambao, pamoja na kufanikiwa katika nchi nyingine kama Malaysia,
inabidi tafsiri na utekelezaji wake ufanywe kwa kutilia maanani
mazingira tuliyomo.
Mpango huo lazima uwe na dira ili uweze
kutekelezeka. Kwa mfano, wanafunzi zaidi ya 800,000 waliomaliza jana
elimu ya msingi walitayarishwaje ili elimu hiyo iwawezeshe kumudu maisha
yao? Je, elimu hiyo inatosha au taifa lijielekeze sasa katika kufanya
elimu ya msingi kuwa kidato cha nne? Mwaka jana wanafunzi asilimia 64
tu waliofanya mtihani huo ndio waliochaguliwa kwenda sekondari, huku
asilimia 36 ikiachwa kutokomea mitaani kueneza ujinga na kugawana
umaskini.
Bahati mbaya Waziri Kawambwa bado ni mateka wa
takwimu zinazompa ndoto za kufaulisha wanafunzi 80 kati ya 100 ifikapo
mwaka 2015 katika elimu ya msingi. Alikaririwa juzi akisema mwaka huu
ufaulu utaongezeka kutoka asilimia 31 hadi asilimia 60 na kwamba
ongezeko hilo litakwenda sambamba na ongezeko la madarasa. Tatizo ni
kwamba anasahau kwamba suala la elimu ni mtambuka, kwa maana kwamba
kuongezeka kwa ubora wa elimu kunategemea mambo mengine mengi kama vifaa
vya kufundishia, vitabu, walimu bora, usafiri, mitalaa sahihi,
miundombinu (mabweni, maabara, madarasa) na huduma za maji, afya,
nishati, chakula na kadhalika.
Pamoja na kuwapo umuhimu wa kupanua elimu ya
msingi kuwa kidato cha nne, tunadhani pia wakati umefika wa kubadilisha
mitalaa ili ijikite katika kutoa elimu ya kujitegemea.
Mkazo uwekwe katika elimu ya ufundi, kwa maana ya
kuhakikisha angalao kila wilaya inakuwa na chuo kimoja cha kutoa elimu
stadi mfano wa VETA. Vinginevyo, majeshi tunayozalisha kila mwaka kutoka
shule za msingi yatasababisha maafa na tutabaki kulia na kusaga meno.
No comments:
Post a Comment