OPERESHENI Kimbunga ambayo imeanza eneo la Magharibi ya nchi, sasa
imeingia Dar es Salaam ambako imepangwa kufanyika kwa siku tisa kukamata
wahamiaji haramu.
Kwa mujibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam,
hadi jana wahamiaji 465 kutoka mataifa 17 wakiwamo walimu wanaofundisha
shule za michepuo ya Kingereza wamekamatwa.
WakizungumzWa na waandishi wa habari jana, wajumbe wa Kamati hiyo
walisema operesheni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais
Jakaya Kikwete la kuhakikisha wahamiaji haramu wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kurudishwa kwao.
Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo alitaja
waliokamatwa kuwa ni Warundi 181, Wakongo 38, Wanyarwanda watano,
Waganda 16, Wakenya 38, Wapakistani sita, Wasomali 28, Wanigeria 12,
raia wanane wa Msumbiji, 114 wa Malawi, wawili wa Cameroon na 10 wa
India.
Aidha, walikamata raia watatu wa Uturuki, watatu wa Comoro, mmoja wa Afrika Kusini, mmoja wa China na mmoja wa Burkina Faso.
Alisema wahamiaji hao wengi wao ni vijana na wamekuwa wakijifanya
walimu wa shule za michepuo ya Kingereza, lakini hawana taaluma hiyo,
isipokuwa wanakijua tu Kingereza na wengine ni wauza kahawa, wafanyakazi
wa ndani, walinzi, watunza bustani, wauza matunda na maji.
Alisema baada ya agizo la Rais wengi walikimbia Kanda ya Ziwa na
kukimbilia Dar es Salaam wakijua hawatajulikana, lakini kutokana na
ushirikiano walionao Uhamiaji na Polisi wamekamata wahamiaji hao haramu
ambao wengine hujifanya Waha.
Alisema tayari 108 wamegharimiwa na Serikali kurudishwa katika nchi
zao na wengine kupewa siku saba warudi kwao, huku wakiendelea na
uchunguzi zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki alitaka wamiliki wa
shule hizo kufuata taratibu za kuajiri walimu kwa kuzingatia sheria na
taratibu zilizopo, ili kuepusha wimbi la wahamiaji haramu ambao wengi
wamegundulika kukosa vibali vya kuwa nchini.
Pia alionya wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya mikutano usiku na
wahamiaji hao haramu wakidai kuwa ni wapiga kura wao na kusema
maandamano ambayo wameandaa kwenda ofisini kwake, yawe ni ya raia ila
kama ni ya wahamiaji haramu watakamatwa hapo hapo na kuchukuliwa hatua.
Pia alitaka raia wa Malawi wanaolalamika, kwamba wameajiriwa na
Watanzania, kuhakikisha wanawalazimisha mabosi wao kufuata taratibu
zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuwa na vibali badala ya kuwaingiza kupitia
‘njia za panya’.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema Polisi inashikilia watuhumiwa wanane wanaojifanya
maofisa wa Idara ya Uhamiaji na kuingia katika nyumba za wakazi wa
Mwananyamala raia wa Malawi waishio nchini na kuwapora mali na
kuwajeruhi.
Alitaja waliokamatwa kuwa ni Amos Rabus (31) wa Mwananyamala, Jeremia
Thomas (21), wa Mbezi Kimara, Paulo Punjo (24) wa Kimara, Kamaraba
Innocent (35) wa Mwananyamala, Sotara Matiku (18) wa Mwananyamala Ujiji,
Innocent Pilih (20) na Athuman Rashid (19) wa Tandale.
No comments:
Post a Comment