Thursday, September 12, 2013

WAHAMIAJI HARAMU WAUZA KAHAWA JIJINI DAR

Wahamiaji haramu waliokuwa wakiishi Dar es Salaam, wameendelea kukamatwa na kurejeshwa kwao, ambapo pia imebainika wengi walikuwa wauza karanga na kahawa. Akizungumza na gazeti hili kuhusu msako huo jana, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sylvanus Mwakasekela, alisema waliwabaini wahamiaji hao kutokana na namna walivyokuwa wakiingia Dar es Salaam na makazi yao.
“Ni kweli miongoni mwa tuliowakamata, wapo wauza kahawa na karanga na ni wahamiaji haramu na wengi wao wamekuja nchini baada ya kuvunjwa kambi za wakimbizi ikiwamo ya Katavi,” alisema Mwakasekela.
Alisema ilikuwa rahisi kukamata vijana hao baada ya kubainika kuwa wamepanga chumba kimoja na kulala watu zaidi ya 10, na kila mmoja akilipa Sh 1,000 kwa siku katika nyumba zilizoko eneo la Jangwani.
“Tulikuwa tukienda hata usiku na kukuta wamerundikana kwenye chumba kimoja, wanaingia usiku na kutoka asubuhi. Tatizo kubwa hapa tulibaini ni wenye nyumba ambao wamekuwa wakihifadhi vijana hao kwa kuwatoza Sh 1,000 kwa siku,” alisema.
Wanavyoingia Dar Mwakasekela alisema Operesheni Kimbunga iliyoanzia mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita, imesababisha wahamiaji haramu wengi kukimbilia Dar es Salaam.
Wahamiaji hao kwa mujibu wa Mwakasekela, baada ya kukimbia mikoa ya mipakani, wamekuwa wakiingia Dar es Salaam kimkakati, tofauti na abiria wengine ambao si wahamiaji haramu.
“Wamekuwa wakiteremka kwenye mabasi Kibaha na Mlandizi na kupanda daladala ili wasishukiwe na vyombo vya usalama,” alisema.
Alisema bado Operesheni inaendelea na waliokamatwa na kukiri kuwa si raia, wamerejeshwa kwao na waliokana wanaendelea kuhojiwa.
“Tunawapa fomu ambazo kama si raia utashindwa tu kuzijaza, na tukiwabana baadaye wanakiri na kurudishwa kwao. Kwa wanaong’ang'ania kuwa ni raia, hatuwezi kulazimisha kuwapeleka kwa sababu italeta tatizo mpakani wakati wa kuwakabidhi kwa wenzetu,” alisema.
Gazeti hili lilishuhudia kundi la vijana wakijaza fomu maalumu kwa ajili ya kubaini uraia na ukazi. Fomu hizo mbali na kuuliza historia ya mjazaji, lakini kama mhusika si raia, hushindwa kujaza baadhi ya maswali. Operesheni Kimbunga Dar es Salaam imepangwa kufanyika kwa siku tisa na hadi juzi wahamiaji haramu 465 kutoka mataifa 17 walishakamatwa.
Mataifa hayo ni Burundi, DRC, Rwanda, Uganda, Kenya, Pakistani, Somalia, Nigeria, Msumbiji, Malawi, Cameroon, India, Uturuki, Comoro, Afrika Kusini, China na Burkina Faso.
Biashara yaadimika Kutokana na operesheni hiyo, biashara ya kahawa na kashata imeadimika Dar es Salaam kwa kuwa asilimia kubwa ya wahusika wameondolewa. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonesha tangu mwanzo mwa wiki hii wafanyabiashara wa kahawa wameadimika katika mitaa ya Dar es Salaam.
Gazeti hili lilipita baadhi ya maeneo ya Kariakoo, Mnazi Mmoja na katikati ya Jiji, eneo la Posta ambako biashara hiyo ilikuwa ikifanywa na vijana na sasa haipo tena. Mmoja wa wateja wa kahawa, ambaye alitaka atambuliwe kwa jina moja la Mzee Hamisi, alielezea kuadimika kwa biashara hiyo.
“Yaani nimekaa hapa nikiwa na imani muuza kahawa atatokea, haya mambo ya ujirani bwana,” alisema huku akifafanua kuwa baadhi walikuwa wakifahamika.
“Enzi za Nyerere (hayati Baba wa Taifa, Julius) jambo kama hili lilitokea Kenya, Wachaga walipata hasara ya kuacha ng’ombe na mali zingine baada ya kurejeshwa nchini,” alisema.
Chanzo: Habari leo

No comments: