MKAZI wa Temeke Mikoroshini, Dar es Salaam, Mwanaidi Mruma amemwagiwa
maji yanayodaiwa kuwa tindikali na shemeji yake na kumsababishia uoni
hafifu.
Akizungumza na HabariLeo jana, Mwanaidi alidai kuwa tukio hilo
lilitokea Jumapili jioni nyumbani kwao akijiandaa kupika mlo wa usiku
kwa ajili ya familia yake.
Kwa sasa jicho lake la kushoto limevimba huku lingine likifunguka lakini yote yakitoa machozi muda wote.
Akisimulia, alidai kuwa kabla ya tukio alipita mdogo wake na kumwomba
amsindikize gengeni kununua bidhaa ambazo alitumwa na mama ambako ni
karibu na anakoishi Mwanaidi.
“Baada ya kufika nyumbani kwa wazazi wangu nilijadiliana nao masuala
kadhaa na kisha kuaga kurejea kwangu ambako nilifika na kumkuta shemeji
Shaban Ali akiwa nje amekalia dumu akionekana mwenye hasira na amelewa,”
alisema Mwanaidi na kuongeza kuwa hakumwuliza chochote akaingia ndani
na kuuliza wapangaji kilichotokea.
Alisema wapangaji wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu, walimwambia
waume zake walitaka kuuana na baada ya kusikia hivyo, Mwanaidi aliingia
ndani na kuendelea kuandaa chakula ndipo shemeji yake akiwa na dumu
alimmwagia kitu kama maji ambayo alidai yalimwasha na kushindwa kuona
vizuri.
Aliongeza kuwa kutokana na tukio hilo akiwa hajui alichomwagiwa ni
tindikali au maji ya betri, alichukua wanawe wawili na kupigia simu
wazazi wake waje kumsaidia, wakaja na kwenda kituo cha Polisi cha
Sandali kuripoti na kupewa fomu ya matibabu PF3 namba, Sand/RB/474/2013.
Aidha, alisema kituoni hapo alikutana na mumewe aitwaye Likwatu Ali
ambaye alikwenda kutoa taarifa za kushambuliwa na ndugu yake huyo,
Shaban, akidai alikuwa na hasira dhidi ya mmoja wa wapangaji ambaye
hakuwa amemalizia sehemu ya kodi ya pango.
Likwatu alidai ugomvi ulianza jioni baada ya kaka yake huyo kufika
amelewa ambapo alimwita na kumwuliza juu ya mpangaji aliyelipa kodi nusu
lakini yeye akamhakikishia kuwa asiwe na wasiwasi kwani fedha italipwa
tatizo ni hali ya uchumi kwa sasa kuwa mbaya.
Katika hatua nyingine, Mwanaidi aliongeza kuwa shemeji yake huyo
hajui ana visa gani naye, kwani mbali ya kuwa msaada mkubwa kwake
akimpikia chakula mtoto wake anayesoma darasa la saba, lakini pia
aliwahi kumtamkia kuwa ipo siku atamnyonga, na ugomvi huo kumalizwa na
baba mzazi wa mumewe.
Kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Englibert
Kiondo alisema taarifa hizo hazijafika ofisini kwake rasmi na kumtaka
Mwanaidi aende haraka ofisini kwake, ili kuwezesha kupatikana kwa
mtuhumiwa, kwani huenda akawa ni mmoja wa watuhumiwa wa tindikali
wanaotafutwa na Jeshi hilo.
No comments:
Post a Comment