Utangulizi
Ndugu wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa
kutujalia uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kuzungumza na
taifa juu ya masuala muhimu yanayohusu nchi yetu. Mwezi wa Saba
tunaoumaliza leo ulikuwa na matukio mengi baadhi yakiwa makubwa na
kushtusha na mengine yalikuwa matukio ya kawaida.
Mashambulio ya Mabomu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 3 Julai, 2014 na tarehe 07 Julai, 2014 kulitokea mashambulizi ya
mabomu nyumbani kwa Sheikh Sudi Ally Sudi na katika mgahawa wa Vama kwa
mfuatano huo. Kabla ya hapo, kulikuwa na matukio mengine matatu: Kanisa
la Olasiti tarehe 5 Mei, 2012, Mkutano wa Kampeni wa CHADEMA tarehe 15
Juni, 2013 na Baa ya Arusha Night Park tarehe 13 Aprili, 2014. Hali
kadhalika, tarehe 13 Juni, 2014 kulitokea shambulizi la mabomu katika
eneo la Darajani, Zanzibar.
Kila lilipotokea shambulizi uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa
kukamatwa. Lakini, watuhumiwa waliokamatwa safari hii wanaelekea kutoa
sura nzuri zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili
pale Arusha na kwingineko nchini. Watu 38 wameishafikishwa Mahakamani, wengine 8 watafikishwa Mahakamani kesho na uchunguzi na msako unaendelea kote nchini kuwapata watuhumiwa wengine.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri iliyotufikisha hapa tulipo
sasa. Tunawaomba waongeze bidii, maarifa na ushirikiano mpaka wote
waliohusika wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, natoa pongezi na shukrani maalum kwa wananchi wema waliotoa
taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa. Napenda kutumia nafasi
hii kuwasihi wananchi wenye taarifa kuhusu wanaotafutwa au ye yote
anayejihusisha na vitendo hivi viovu watoe taarifa kwenye vyombo vya
usalama ili hatua zipasazo zichukuliwe.
Kutupwa Viungo vya Binadamu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Julai, 2014, katika Bonde la Mto Mpiji lililopo eneo la Bunju
Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, viligunduliwa viungo vya binadamu na
baadhi ya vitendea kazi vya madaktari vikiwemo aprons na gloves. Viungo
hivyo vilivyokutwa vimekakamaa na kuhifadhiwa katika mifuko myeusi 85, vilikuwa
vimetupwa jana yake tarehe 21 Julai, 2014. Tukio hilo lilileta taharuki
na hofu kubwa katika Jiji la Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.
Uchunguzi uliofanywa uligundua kuwa viungo hivyo vilikuwa vinatumika
kufundishia wanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Tiba kilichoko
Mbezi Beach maarufu kwa jina la IMTU. Ni utaratibu wa kawaida kwa vyuo
vikuu vya udaktari nchini na kote duniani kutumia miili ya wanadamu
waliofariki kufundishia. Hata hivyo, pale viungo hivyo vinapokuwa
havihitajiki tena kwa shughuli hiyo, zipo taratibu zake za kuvisitiri
ambazo hazikufuatwa. Bahati nzuri mamlaka husika zimeona kasoro hiyo na
hatua zimeanza
kuchukulikuwa. Tuziachie mamlaka hizo kuchukua hatua zipasazo kwa mujibu
wa madaraka yao na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zinazotawala shughuli
za namna hiyo. Ni matumaini yangu kuwa yaliyofanywa na IMTU
hayatafanywa tena na Chuo hicho wala chuo kingine cho chote hapa
nchini.
Ziara Yangu Mikoani
Ndugu Wananchi;
Katika mwezi huu wa Julai, nimefanya ziara katika ya mikoa ya Tanga na
Ruvuma. Nimefurahishwa sana na hatua kubwa ya maendeleo waliyopiga
wananchi wa mikoa hiyo. Pamoja na mchango wa Serikali, ari na mwamko
mkubwa wa kujiletea maendeleo walionao viongozi na wananchi wa mikoa
hiyo vimechangia sana katika kuongeza kasi ya maendeleo na mafanikio
yanayoendelea kupatikana. Katika ziara hizo, nilizindua miradi
iliyokamilika na kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ile ya barabara, umeme,maji, afya, elimu, majengo ya
Serikali, nyumba na kadhalika.
Nimepata faraja kubwa kupata taarifa kuwa ahadi zangu nyingi na zile
zilizomo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zimekamilika na zingine
ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Ndoto ya miaka mingi, kabla
na baada ya Uhuru, ya wananchi wa Mikoa ya Kusini ya kutaka Mikoa yao
ifunguke na kuunganishwa na mikoa mingine kwa barabara za lami sasa kuna
uhakika wa kukamilika. Barabara ya kutoka Mbinga, Songea hadi Namtumbo
iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya Marekani imekamilika na
tuliizindua. Tuliweka mawe ya msingi ya kujenga barabara ya lami kutoka
Namtumbo, Tunduru, Mangaka hadi Mtambaswala kwenye Daraja la Umoja
linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika na Serikali ya Japan. Barabara ya kutoka Mangaka hadi Masasi
iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya Japan imekamilika na tuliizindua.
Katika barabara ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay kimebaki kipande cha kilometa 66 kutoka
Mbinga kwenda Mbamba Bay ambacho hakikuwa na mpango wo wote wa kuwekewa
lami kwa sasa. Bahati nzuri, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (ADB), Bibi Tonia Kandiero alitangaza pale Namtumbo kuwa Benki
yake itafadhili ujenzi wa barabara hiyo. Mambo sasa yamekamilika.
Kule Masasi mkoani Mtwara na Nachingwea mkoani Lindi tulizindua
kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Mbwinji unaomaliza tatizo kubwa
la maji kwa miji hiyo kwa miaka mingi ijayo.
Nyumba za Bei Nafuu
Ndugu Wananchi;
Nikiwa wilayani Mkinga na katika Manispaa ya Songea nilizindua nyumba za
gharama nafuu zilizojengwa na Shirila la Nyumba la Taifa (NHC). Nyumba
hizo za vyumba viwili na vitatu zinauzwa kwa bei ya shilingi milioni 31 hadi 42.
Wenzetu wa NHC walinieleza utayari wa kujenga nyumba zaidi endapo
watapatiwa maeneo na Halmashauri za Wilaya na Miji. Walinilalamikia kuwa
hawapati ushirikiano wa kutosha kutoka mamlaka husika. Nilipokuwa
Mkinga na Songea niliagiza Halmashauri hizo na nyinginezo nchini kutenga
maeneo kwa ajili ya NHC na Mifuko ya Hifadhi za Jamii yote ili waweze
kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wafanyakazi na wananchi kwa
ujumla.
Hii ni fursa ya aina yake kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati
kuweza kujipatia nyumba kwa urahisi. Halmashauri zisiwe kikwazo wakati
ardhi imejaa tele na kila wakati wanapima viwanja vipya. Jambo lingine
zuri waliloniambia viongozi wa NHC ni kwamba zipo Benki ambazo
wanashirikiana nazo kutoa mikopo kwa watu wanaonunua nyumba zao. Ni
matarajio yangu kwamba uongozi wa Halmashauri zote nchini utaitikia
maelekezo yangu na kwamba utatenga maeneo kwa ajili ya mashirika yetu
hayo.
Matibabu kwa Wazee
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa wilaya ya Kilindi nilifurahishwa sana na utaratibu wa
kuwapatia wazee huduma ya matibabu. Kama mjuavyo Sera ya Afya inataka
wazee na watoto wa chini ya miaka mitano watibiwe bure katika hospitali
za Serikali. Bahati mbaya vitambulisho wanavyopata wazee vimekuwa
havithaminiwi ya kutosha. Kwa sababu hiyo, nafuu wanayostahili kupata
imekuwa haipatikani kwa urahisi na wengine huikosa kabisa.
Katika Wilaya ya Kilindi, Halmashauri ya wilaya imeamua kuwakatia wazee
hao Bima ya Afya inayotolewa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na hivyo
kuondoa kabisa migogoro inayohusiana na vitambulisho vya wazee
vilivyokuwepo kabla. Kwa kuzingatia malalamiko ya mara kwa mara
ninayoyapata kutoka kwa wazee kuhusu matibabu, nashauri Halmashauri zote
nchini ziige mfano wa Wilaya ya Kilindi. Kama Kilindi wameweza kwa nini
wengine washindwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mikoa hii miwili nilipokea taarifa za kutia moyo kuhusu juhudi za
wananchi na Serikali katika kupanua fursa za elimu. Vijana wengi wenye
umri wa kujiunga na shule za msingi wanafanya hivyo na wale wote
wanaofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata fursa ya kwenda sekondari.
Hatuna tena tatizo la fursa. Pamoja na mafanikio hayo mazuri, taarifa
za wanafunzi wengi kushindwa kumaliza elimu ya msingi na sekondari,
zimenishtua na kunisikitisha sana.
Katika Mkoa wa Tanga kwa mfano, kati ya wanafunzi 50,921 walioanza darasa la kwanza mwaka 2007 , ni wanafunzi 41,017 tu ndiyo waliofanya mtihani mwaka 2013. Hivyo basi, wanafunzi 9,904 ambao ni sawa na asilimia 19.4 hawakumaliza elimu ya msingi. Kwa upande wa sekondari, katika mkoa wa Ruvuma, kwa mfano, kati ya wanafunzi 18,892 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2010 ni wanafunzi 9,968 sawa na asilimia 52.76 ndiyo waliofanya mtihani wa kidato cha nne. Hivyo basi, wanafunzi 8,924 sawa na asilimia 47.2 hawakumaliza
elimu ya sekondari. Taarifa za namna hii nilizipata pia katika ziara
zangu ya Mikoa ya Kagera, Geita na Simiyu. Nina kila sababu ya kuamini
kuwa hali ni hiyo hiyo kwa Mikoa mingine mingi nchini. Kwa kweli kiwango
hiki cha wanafunzi wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi na sekondari
ni kikubwa mno. Kinanisikitisha sana, hakikubaliki na hakiwezi kuachwa
kiendelee.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu wazazi, walimu na viongozi wanao wajibu maalumu wa
kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanahudhuria masomo shuleni tangu
wanapoanza mpaka wanapomaliza masomo yao. Huu ni wajibu wa lazima na
siyo hiari. Ni wajibu wa kisheria. Kwa hiyo, nimeagiza kwamba, wazazi,
walimu, Maafisa Elimu wa Wilaya wa Msingi na Sekondari na Kamati husika
katika Halmashauri zote nchini ziwajibike ipasavyo kuhakikisha kuwa
utoro mashuleni unakomeshwa. Ajenda ya mahudhurio shuleni iwe ni ya
kudumu katika vikao vyote vya Halmashauri.
Kuanzia sasa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ni lazima watoe taarifa za
mahudhurio ya wanafunzi kwa Maafisa Elimu wa Wilaya kila miezi mitatu.
Maafisa Elimu wa Wilaya nao watalazimika kutoa taarifa kwenye vikao vya
Halmashauri mwezi mmoja baada ya kupokea taarifa hizo. Halmashauri
hazina budi kuchukua hatua stahiki za kijamii na kisheria kuhakikisha
kuwa watoro wanarudi shuleni. Wazazi wa watoto hao au mtu ye yote
atakayebainika kuhusika na utoro huo abanwe ipasavyo.
Sheria ya Elimu ya 1978 ipo, itumieni kwa ukamilifu kulitatua tatizo
hili. Haipendezi kusubiri mpaka miaka saba kwa wanafunzi wa shule ya
msingi au miaka minne kwa wanafunzi wa sekondari ipite ndipo taarifa za
utoro kwa wanafunzi zitolewe au zijulikane. Lazima ufuatiliaji wa
mahudhurio uwe wa mara kwa mara ili hatua za kuzuia ziweze kuchukuliwa
mapema. Ninawataka viongozi wa TAMISEMI, Mikoa na Wilaya kuchukua hatua
stahiki kudhibiti tatizo hili la utoro na watoto wengi kutokumaliza
masomo. Litarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Umeme Vijijini
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa mkoani Ruvuma nimezindua ujenzi wa miradi mingi ya umeme vijijini. Kwa mujibu wa miradi hiyo vijiji 309 vitapatiwa umeme kati ya vijiji 509 vya
Mkoa huo vinavyohitaji umeme. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi
za dhati kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na
viongozi wenzake, viongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Umeme Vijijini
(REA) pamoja na TANESCO kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo ya kufikisha
umeme vijijini. Kwa kweli ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
suala la umeme vijijini kupewa msukumo mkubwa kiasi hiki, kwani
kinachofanyika Ruvuma kipo nchi nzima. Nawaomba wananchi wanaofikishiwa
umeme wautumie. Hata gharama za kuunganisha umeme zimepunguzwa makusudi,
ili watu wengi waweze kumudu kuingiza umeme majumbani na kwenye
shughuli za kichumi na huduma.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama tujuavyo, Bunge Maalum la Katiba lililoahirishwa tarehe 25 Aprili,
2014 kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la
Wawakilishi kushughulikia bajeti za Serikali husika, litakutana tena
tarehe 5 Agosti, 2014 kuendelea na kazi yake ya kutunga Katiba Mpya. Kwa
vile Bunge Maalumu la Katiba halikuweza kumaliza kazi yake ndani ya
siku 70 zilizotengwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
nimeliongezea Bunge hilo siku 60 kwa ajili ya kukamilisha kazi yake. Nimefanya hivyo kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Sheria hiyo hiyo.
Hatua Iliyofikiwa Kabla ya Kuahirishwa kwa Bunge
Ndugu Wananchi;
Itakumbukwa pia kuwa, tarehe 16 Aprili, 2014, baadhi ya Wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba hasa kutoka vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi
walisusia mjadala uliokuwa unaendelea Bungeni na kutoka nje. Wakati
wanatoka Bungeni, kazi kubwa ilikuwa imefanyika. Tayari Kamati zote 12
za Bunge hilo zilikuwa zimekamilisha kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita za
Rasimu ya Tume. Sura hizo zinazungumzia utambulisho wa nchi na muundo
wa muungano. Kamati zote zilipiga kura ya kupitisha uamuzi wao kuhusu
sura hizo mbili. Kamati kadhaa ziliweza kupata theluthi mbili ya kura kwa Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano, jambo lililoonyesha dalili njema kwamba Katiba mpya inaweza kupatikana.
Baada ya hapo, taarifa ya kila Kamati iliwasilishwa kwenye Bunge zima.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, maoni ya wachache nayo
yaliwasilishwa. Kazi iliyokuwa inafuatia, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge
ni kwa Kamati ya Uandishi kukamilisha taarifa yake na kuiwasilisha
kwenye Bunge zima kwa ajili ya kujadiliwa. Baada ya Wajumbe kujadili
taarifa hiyo itafuatia kupiga kura ili kuamua kuhusu Sura hizo mbili.
Kama yalivyo masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi
utafanywa kwa theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano wetu.
Sababu za Baadhi ya Wajumbe Kususia Bunge Maalumu la Katiba
Ndugu Wananchi;
Sote tumewasikia Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliosusia vikao vya
Bunge hilo wakielezea sababu zilizowafanya watoke Bungeni. Walitoa
matamko kwenye vyombo vya habari na pia katika mikutano ya hadhara
waliyoiitisha na kuhutubia sehemu mbalimbali nchini. Sababu walizotoa
zimekuwa zikiongezeka na kubadilika kadri siku zinavyosonga mbele na
upepo wa kisiasa unavyokwenda.
Hivi sasa wanazungumzia mambo mawili. Kwanza, kwamba Bunge Maalumu
halina mamlaka ya kuifanyia mabadiliko yo yote Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa maoni yao, kazi ya
Bunge Maalumu la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu ya Katiba ya
Tume na siyo kubadili cho chote. Pili, wametoa sharti la wao kurudi
Bungeni ni kuhakikishiwa kwamba, kitakachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya
Tume. Bila ya sharti hilo kukubaliwa, wamesisitiza kutorudi Bungeni.
Mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba
Ndugu Wananchi;
Mimi nimehusika katika kubuni wazo la kuwa na mchakato wa kuandika
Katiba Mpya, na katika maandalizi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ya
kuongoza na kuendesha mchakato huo. Kwa kweli sikumbuki wakati wo wote
katika vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba tulipozungumzia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kuwa haiwezi kufanyiwa marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.
Mimi siyo Mwanasheria na hivyo nakiri kwamba naweza kuwa na upungufu
katika kuelewa maana ya baadhi ya maneno ya kisheria. Hata hivyo,
sikumbuki kuwepo kwa kifungu cho chote katika Sheria kinachosema kuwa
Bunge Maalumu la Katiba halina mamlaka hayo. Tangu tulipoyasikia maneno
hayo yakisemwa nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa madai hayo bado
sijaambiwa vinginevyo. Kama ukweli huo upo naomba anisaidie. Badala yake
naambiwa kuwa maneno yaliyotumika katika Sheria haiakisi dhana
inayotolewa kuwa kazi ya Bunge Maalum la Katiba ni kubariki Rasimu na
siyo kufanya vinginevyo. Nimeambiwa kuwa sheria inasemaTume itaanda Rasimu ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba litatunga Katiba iliyopendekezwa.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Desemba, 2010, nilipozungumzia dhamira yangu ya kuanzisha
mchakato wa kuandika Katiba Mpya nilieleza wazi nia ya kuwepo kwa
uwakilishi mpana wa Watanzania katika mchakato huo. Ndiyo maana katika
Sheria tukaweka ngazi nnekatika mchakato wa kutunga Katiba. Ngazi
ya kwanza ikiwa ya wananchi kutoa maoni yao juu ya kila wanachotaka
kijumuishwe katika Katiba ya nchi yao. Ngazi ya pili, ni ya wananchi
kupitia wawakilishi wao katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na Mabaraza
ya Kitaasisi kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya kwanza ya Katiba
iliyotayarishwa na Tume.
Ngazi ya tatu inajumuisha wawakilishi wa wananchi waliopo kwenye
Mabaraza ya Kutunga Sheria ya Sehemu zetu mbili za Muungano, yaani Bunge
la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi, wakichanganyika na
Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii ya Watanzania kutoka pande
zote mbili za Muungano. Hawa ndio wanaounda Bunge Maalumu la Katiba,
lenye jukumu la kutunga Katiba inayopendekezwa.
Mamlaka ya kutunga Katiba kwa mila na desturi za Mabaraza ya Kutunga
Sheria ni uwezo wa kurekebisha, kubadili, kufuta na hata kuongeza
kilichopendekezwa. Ingekuwa kilichokusudiwa ni kubariki tu lisingetumiwa
neno la kutunga Katiba. Hali kadhalika, lisingewepo sharti la kupiga
kura na msisitizo wa kupata theluthi mbili kwa kila upande wa Muungano.
Aidha, kama ingekuwa jukumu la Bunge Maalumu ni kubariki tu Rasimu
lisingepewa siku 70 za kazi na Rais kupewa mamlaka ya kuongeza siku zaidi kadri aonavyo yeye inafaa.
Ngazi ya nne na ya mwisho, tuliweka kura ya maoni ya wananchi kukubali
au kukataa Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba. Kama
ingekuwa Rasimu ya Tume haiwezi kubadilishwa hata nukta kwa nini basi
tuweke kura ya maoni ya kuwahusisha wananchi wote?
Ndugu Wananchi;
Tulizibuni ngazi hizi nne kwa dhana kwamba kile ambacho
hakikuonekana au hakikuwekwa sawa katika ngazi moja kitaonekana na
kurekebishwa katika ngazi inayofuata katika ngazi zile tatu za mwanzo.
Na, iwapo Katiba iliyotungwa haitawaridhisha wananchi wanayo haki ya
kuikataa. Kwa kufanya hivyo, wananchi ndiyo waliopewa turufu ya mwisho.
Ndugu wananchi;
Kwa kweli, napata shida kuelewa mkanganyiko unatoka wapi na hasa wale
wanaoongoza kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu kuwa ni wale wale waliotunga
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tena hatua kwa hatua. Nashangazwa zaidi
ninapoona wale wale waliotunga Kanuni za Bunge Maalumu ndiyo wanaoongoza
kuhoji uhalali wa kile walichokitunga.
Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, Ibara ya 33 (8) inasema: Nanukuu: “Wakati
wa mjadala, Mjumbe yoyote anaweza kutoa mapendekezo ya marekebisho,
maboresho au mabadiliko yaliyomo katika Sura za Rasimu ya Katiba
zinazojadiliwa kwa utaratibu ufuatao: (a) Ikiwa ni marekebisho,
maboresho au mabadiliko yanayobadilisha jambo la msingi, au
yanayobadilisha maudhui ya Ibara, mapendekezo ya marekebisho yatapelekwa
kwa maandishi kwa Katibu siku moja kabla ya mjadala wa Ibara husika.
(b) Ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo hayabadili msingi au maana,
mapendekezo ya marekebisho yatawasilishwa na mjumbe wakati wa mjadala
baada ya kupata ruhusa ya Mwenyekiti”. Mwisho wa kunukuu.
Kanuni hii ilipotungwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalumu pamoja na wale
ambao baadae walisusia vikao vya Bunge walikuwepo Bungeni na walishiriki
kuipitisha. Tena basi, baadhi yao walikuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni
iliyopendekeza Kanuni hizo. Unapowaona watu wale wale sasa wanakuwa
vinara wa kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, unajiuliza maswali
mengi kuhusu watu hao bila ya kupata majibu yaliyo sahihi na kutosheleza
akili na ufahamu wetu.
Ndugu Wananchi,
Unaposoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalumu, hii
ni dhahiri kwamba wote walikuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mamlaka ya
Bunge Maalumu ya kujadili Rasimu iliyoandaliwa na Tume na kutunga Katiba inayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
Kinachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume
Ndugu Wananchi;
Yapo madai yanayotolewa na kuenezwa na Wajumbe waliosusia Bunge Maalumu
la Katiba kwamba kinachojadiliwa Bungeni siyo Rasimu ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ndiyo maana basi wanaweka sharti la kujadiliwa
Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ndipo warudi Bungeni. Madai haya nayo
yananipa taabu kuyaelewa. Ndugu zetu hawa walishiriki siku zote 19 za
Kamati 12 zilipokutana kujadili Sura yaKwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume. Halikadhalika. walikuwepo na kushiriki kwa ukamilifu wakati taarifa za Kamati, tangu ya Kwanza mpaka ya 12,zilipowasilishwa kwenye Bunge zima. Aidha, na wao walishiriki kutoa maoni ya wachache kwa dakika 20 na
kutoa ufafanuzi kwa muda wa dakika 30 kwa kila Kamati. Haya maneno ya
sasa kwamba kinachojadiliwa Bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba
bali nyingine kabisa ambayo wanadai eti ni ya CCM yanatoka wapi.
Mimi nadhani kuwa huenda katika Kamati kumefanyika marekebisho kwenye
Rasimu ambayo hayakuwapendeza. Kama hivyo ndivyo, wawe wakweli kuhusu
jambo hilo kuliko kusema mambo yasiyowakilisha ukweli halisi wa Rasimu
inayojadiliwa. Matokeo yake ni kuwafanya wafuasi wao na wapenzi wao na
hata watu wengine waamini kuwa kinachojadiliwa siyo Rasimu ya Tume ya
Jaji Warioba bali nyingine tena ni ya CCM. Jambo hilo si kweli na
wenyewe wanajua kwamba si kweli ila sijui kwa nini wameamua kupotosha
ukweli.
Ndugu Wananchi;
Kinachonishangaza, zaidi ni kwamba, kama hawakuridhishwa na
yaliyofanyika, kwa nini wasingetumia mifumo waliyojitengenezea wenyewe
kwenye Kanuni kumaliza tofauti zao? Kanuni zinaelekeza kuwa mambo
wasiyoridhika nayo yajadiliwe kwenye Kamati ya Mashauriano na
Maridhiano. Ukiacha mifumo ya maridhiano ndani ya Bunge ukaenda nje kwa
wananchi au vyombo vya habari na mitandao si jawabu la tatizo.
Ndugu Wananchi;
Ndiyo maana nashawishika kuunga mkono wale wote wanaowasihi Wajumbe wa
CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine warejee Bungeni. Watumie mifumo
maalum ya Bunge iliyowekwa na Kanuni kutafuta maridhiano. Hali
kadhalika, wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama vingine vya siasa na
hasa CCM kutafuta maelewano. Mimi niko tayari kusaidia pale watakapoona
inafaa kufanya hivyo kama ambavyo nimekuwa nikifanya ziku za nyuma.
Nililolisema mwanzoni kabisa mwa mchakato na nalirudia tena leo kwamba,
ili tuweze kufanikiwa kupata Katiba Mpya ambayo sote tunaitaka,
maelewano baina ya wadau wakuu wa kisiasa ni jambo lisilokuwa na badala
yake. Vinginevyo kupata theluthi mbili kwa pande zote mbili za Muungano
haitawezekana. Ndiyo maana nampongeza sana Msajili wa Vyama vya Siasa,
Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, kwa uamuzi wa kuvikutanisha vyama vinne
vikuu vya siasa kujadili namna ya kuondoa mtihani uliopo sasa katika
mchakato wa Katiba.
Ombi langu kwa viongozi wa vyama hivyo ni kuitumia vyema fursa ya
majadiliano kuukwamua mchakato kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Hali kadhalika nampongeza sana Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Mheshimiwa Samwel Sitta, kwa kuitisha kikao cha Kamati ya Mashauriano na
Maridhiano. Bahati mbaya ni kwamba Wajumbe wa vyama vilivyosusia Bunge
Maalumu hawakushiriki. Ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa Sitta hatokata
tamaa kuendeleza juhudi za mashauriano na kwamba katika vikao vijavyo
na wenzetu hawa watashiriki.
Ndugu Wananchi;
Hivi karibuni kumekuwepo pia madai yanayoelekeza lawama kwangu. Kwanza
nalaumiwa eti kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale nilipotoa
hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika. Pili nalaumiwa
kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na mimi ni mmoja wa
watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo.
Niruhusuni nianze na hili la pili. Nadhani ndugu zetu wanaotoa madai
haya yameitafsiri isivyo sahihi yangu katika Gazeti la Serikali
lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume
kumaliza kazi yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya
Muungano amepewa kazi tatu kufanya. Kwanza, kupokea Rasimu hiyo na
Taarifa ya Tume kutoka kwa Mwenyekiti jambo ambalo lilifanywa tarehe 30
Desemba, 2013. Pili, amepewa kazi ya kuitangaza rasmi Rasimu ya Katiba
na Taarifa ya Tume kwa watu wote kuiona na kuisoma ndani ya siku 30.
Alipewa sharti la kuitangaza katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine
vya habari. Hili nalo lilifanywa hivyo tarehe 22 Januari, 2014.
Ndugu Wananchi;
Katika kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza
ajitambulishe kuwa yeye ni nani na atie sahihi yake. Kwa kufanya hivyo,
hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila
kinachopendekezwa na Tume. Sahihi zilizomo ndani ya Rasimu na Taarifa ya
Tume ni za Wajumbe wa Tume, kamwe sahihi ya Rais haimo hivyo hawezi
kulaumiwa kuwa anaikana sahihi yake. Yeye ametimiza wajibu wake wa
kutangaza, akaiweka hadharini kwa umma wa Watanzania kuiona na kusoma
Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume vilivyotayarishwa na kutiwa sahihi
na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi ya tatu ni kuitisha
Bunge Maalumu ambayo nayo imekamilika tangu tarehe 18 Februari, 2014.
Ndugu Wananchi,
Jambo lingine linalofanana na hilo ni yale madai kwamba nilikuwa napata
taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume mara kwa mara, iweje leo
nitoe maoni tofauti kama niliyoyatoa katika hotuba yangu kwenye Bunge
Maalumu. Ni kweli kabisa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, Makamu wake, Mheshimiwa Jaji Agustino
Ramadhani na Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim wamekutana na mimi kwa
nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato. Lakini, hayakuwa
mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo
ya Tume. Ukweli ni kwamba Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza
nilipokabidhiwa rasmi, tena kwa uwazi. Napenda watu wasijenge dhana kuwa
nilipewa Rasimu na kuisoma kabla ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni
yangu. Tume hii ilikuwa huru na niliiacha iwe hivyo. Sikuiingilia kwa
namna yo yote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo. Kuthibitisha
dhamira yangu ya kutaka Tume iwe huru katika kufanya kazi zao hata pale
waliponitaka nitoe maoni niliwaomba tusifanye hivyo ili nisiwakwaze
katika kufanya kazi zao, wakapata taabu ya kuwianisha wanayofikiria na
mawazo yangu.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu madai kwamba mambo yalikuwa yanakwenda vizuri na kwamba hotuba
yangu iliyavuruga, napenda kusema wazi kuwa lawama hizo hazina ukweli wo
wote. Ni madai yasiyokuwa na msingi. Kwani mimi hasa siku ile nilifanya
lipi la ajabu. Ukweli ni kwamba nilisema yale yale ambayo Tume yenyewe
imeyasema katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume. Niliyoyasema
kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano na uzuri na
changamoto za miundo ya Serikali mbili na Serikali tatu ni yale yale
yaliyomo kwenye taarifa za Tume. Nimetumia takwimu zile zile za Tume.
Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo
na mapendekezo ya Tume.
Jambo lingine ambalo nimelifanya ni kutoa maoni yangu kuhusu baadhi ya
vipengele vya Rasimu hususan uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo.
Silioni kosa langu kwa kufanya hivyo, kwani Rasimu imetolewa hadharani
kwa watu kuijadili. Na mimi kama raia ninayo haki ya kufanya hivyo kama
wafanyavyo wengine. Kwa nini nilaumiwe kwa kutumia haki yangu hiyo.
Lakini, pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo dhamana ya uongozi na
ulezi wa taifa letu. Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatma ya nchi yetu
nilinyamazie kimya. Watanzania wangeshangaa na wangekuwa na haki ya
kuhoji Rais wao ana maoni gani. Bahati nzuri nilitoa maoni yangu mahali
penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Hata hivyo,
ni muhimu kusisitiza kuwa namna nilvyotoa maoni yangu sikuwa natoa
maagizo wala kushurutisha, ndiyo maana kila wakati niliwakumbusha
Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao. Yangu yalikuwa maoni tu
wanahiyari ya kuyakubali au kuyakataa. Niliwataka Wajumbe wasome na
kuielewa vyema Rasimu. Nilisema wasome sura kwa sura, mstari kwa mstari
na neno kwa neno. Niliwaomba wajiridhishe kuhusu uandishi na dhana
mbalimbali. Nilitoa mifano ya mambo yahusuyo uandishi ambayo ni vyema
wayatazame. Pia nilitoa mifano ya dhana ambazo niliwasihi wajiridhishe
juu ya kufaa kwake kuwepo.
Kuhusu muundo wa Serikali tatu, nilieleza wazi kuwa sina tatizo nao kama
ndiyo matakwa ya Watanzania. Lakini, nilieleza hofu yangu kuhusu
mapendekezo ya Tume na kuwataka Wajumbe wafanye kazi ya ziada kuondosha
udhaifu iwapo wataukubali muundo unaopendekezwa. Nilieleza nia yangu ya
kutaka tuwe na Serikali ya Muungano yenye ukuu unaoonekana, yenye nguvu
ya kuweza kusimama yenyewe, inayoweza kuwa tegemeo kwa nchi Washirika,
Serikali isiyokuwa tegemezi wala egemezi kwa nchi washirika na ambayo
inavyo vyanzo vya uhakika vya mapato. Hivi kwa kutoa ushauri huo kwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba inageuka kuwa nongwa. Kwa kweli
sielewi lawama ni ya nini?.
Naamini sistahili lawama bali pongezi kwa kuwa muwazi na kutoa ushauri
wa msingi ambao utasaidia nchi kupata Katiba nzuri inayojali maslahi ya
watu wa nchi yetu na ya nchi zetu mbili zilizoungana miaka 50
iliyopita.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mwisho, ni maoni yangu ya dhati kuwa mgogoro uliopo sasa katika mchakato
wa Katiba hauna sababu ya kuendelea kuwepo. Naamini hayo yote ambayo
Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanayalalamikia yanaweza
kushughulikiwa kwa ukamilifu katika mifumo ya Bunge Maalumu la Katiba
iliyotengenezwa na Wajumbe wote na wao wakiwemo. Nawasihi waitumie. Hali
kadhalika, kwa kupitia mazungumzo wanayofanya na wenzao wa Chama cha
Mapinduzi wanaweza kutengeneza nguvu ya pamoja kutatua changamoto za
sasa na zitakazojitokeza baadaye. Kilicho muhimu ni kwa pande zote kuwa
na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tulipo sasa. Kama utashi wa kisiasa
upo kwa kila mmoja wetu, hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Narudia
kuahidi utayari wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment