WAKATI nchi ya Malawi ikiendelea kushikilia msimamo wake, kuwa
mpaka Mashariki mwa Ziwa Nyasa kati yake na Tanzania unatenganishwa na
ardhi ya Tanzania, Wazee wilayani Kyela, wametoboa siri na kuweka
hadharani ukweli wake.
Wazee wengi waliotoa ushahidi juu ya ukweli wa
mpaka kati ya Tanzania na Malawi ndani ya Ziwa nyasa, mbele Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe walisema Malawi
inasababisha chokochoko isiyo na msiongi.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mstaafu, John Mwakipesile(70), ambaye alikuwa wa kwanza, kuzungumzia suala hilo, alisema
anashangazwa na madai hayo mapya ya Malawi kuwa Ziwa lote ni miliki
yao.
Alisema kitendo hicho cha nchi hiyo kukurupuka
kinapaswa kupuuzwa kwa kuwa jambo hilo halina ukweli na linapingana na
historia na desturi za kweli za maisha ya kawaida ya wananchi wa mpakani
wa mataifa haya toka enzi za ukoloni.
Alisema madai ya Malawi hayajazingatia historia ya
kweli ya ziwa hilo kwani madai yao yote ni kujaribu kuficha ukweli kwa
kuwa yeye kama kizazi cha tatu hata siku moja hakuwahi kusikia kuwa
ziwa lote ni mali ya nchi hiyo.
Alisema kuna ushahidi wa kutosha juu ya Tanzania
kuwa miongoni mwa wamiliki wa ziwa hilo, kwani kuna mali za Watanzania
yakiwamo makaburi ndani ya ziwa hilo baada ya kumezwa.
Alitolea mfano shule ya msingi aliyosoma katika
mwaka 1945 kuwa ilishamezwa na ziwa hilo, yakiwemo majengo ya baraza
(Mahakama) katika kijiji alichozaliwa cha Mwaya katika wilayani humo.
“Mimi kwa umri wangu wa miaka 70 ni kizazi cha
tatu katika wilaya hii nakumbuka shule niliyosoma mwaka 1945 pale Mwaya
nilipozaliwa ilishamezwa na Ziwa na ni umbali wa kilomita mbili toka
pwani ya sasa kijijini hapo” alifafanua Mwakipesile.
Naye Maini Mwakisambwe (83), Mkazi wa Kata ya
Katumba songwe, alisema tangu azaliwe alikuwa akijua mpaka ni Mto
Songwe ambao unaingiza maji ndani ya ziwa hilo na ndio uliotumika kama
mpaka wa kuligawa ziwa kwa mataifa haya mawili.
Mbali na hilo, lakini pia wakiwa vijana
walishuhudia viongozi wa Serikali zote mbili wakiheshimu mpaka huo ndani
ya ziwa , kwa kuwa hata waliposafiri toka upande mmoja kwenda mwingine
kila wakifika eneo la Mto Songwe bendera ya upande mmoja ilishushwa na
kupandishwa ya upande mwingine.
Philipo Mwandemele(73) kabla ya kuanza kutoa
maelezo yake alitoa kitabu kimoja kinachozungumzia maisha na desturi za
wakazi wa nchi hizi mbili kama nyaraka muhimu inayoweza kutumika
kueleza ukweli juu ya sakata hilo la mpaka.
No comments:
Post a Comment