Waziri wa Katiba na Sheria,Mathias Chikawe |
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amesema Serikali
haikusudii kufanya marekebisho yoyote kwenye Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba baada ya kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete hivi
karibuni.
Chikawe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na
Mwananchi kwa njia ya simu, ambapo alifafanua kuwa isipokuwa kama kuna
watu kutoka katika taasisi ambazo zina mapendekezo yao wanayoona ni
vyema yaingizwe kwenye sheria hiyo, wanatakiwa kufuata utaratibu
unaotakiwa ili kufanikisha.
“Serikali haina marekebisho yoyote ila najua kuna
vyama vya siasa vinakutana na vinakusanya mapendekezo yao, naamini
kwamba watafuata taratibu zinazotakiwa ili marekebisho wanayopendekeza
yaweze kuingizwa kwenye sheria hiyo.
Awali mwenyekiti wa mchakato shiriki wa vyama
vyenye wawakilishi bungeni, James Mbatia alieeleza kuwa wapo katika
hatua nzuri ya majadiliano ambayo yanalenga katika kupambana na
changamoto kwenye sheria hiyo.
“Nakuhakikishia mwandishi kwamba kuna ushirikiano
mzuri miongoni mwa vyama vyote vinavyoshiriki katika mchakato huo,
tunaangalia makosa yaliyojitokeza na kuzusha changamoto ni mchakato wa
kupata Katiba Mpya, tutakutana tena siku ya Jumapili baada ya hapo
tunazungumza na vyombo vya habari tupeni muda kwanza,” alisema Mbatia.
Alivitaja vyama vinavyoshiriki katika mchakato huo
kuwa ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), NCCR-Mageuzi, Chama cha
Dekmokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Labour Party (TLP) Chama cha
Wananchi (CUF) na United Democratic Party (UDP).
Waziri Chikawe kabla ya mswada kusainiwa na Rais
Kikwete aliwahi kuonya kuwa muswada huo ukirudi bungeni bila kusainiwa
unaweza kusababisha vurugu kubwa zaidi ya zile za mara ya kwanza
kutokana na tofauti kati ya wabunge wa CCM na wale wa vyama vya Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi.
Rais Kikwete, alisaini Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya 2011, uliopitishwa na Bunge
mjini Dodoma, Novemba 18 mwaka huu.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment