Mgombea Ubunge wa Chalinze kwa tiketi ya Chadema, Mathayo Torongey akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kutambulishwa. |
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimempitisha Mathayo Torongey kuwa mgombea rasmi wa ubunge kwa tiketi ya
chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze.
Akimtambulisha mgombea huyo kwa Waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa
Chadema, John Mrema alisema Torongey alipitishwa juzi na Sekretariati ya
chama kwa niaba ya kamati kuu.
“Kikao cha Sekretariati kilizingatia maoni na
ushauri wa wanachama na viongozi wetu wa ngazi za chini, Hivyo kwa kuwa
hakukuwa na kipingamizi chochote juu ya agombea, chama kilimpitisha
Torongey” alisema Mrema.
Torongey alishinda kura za maoni za chama hicho
jimboni Chalinze kwa kupata kura 280 dhidi ya 510 zilizopigwa.
Aliwashinda wapinzani wake, Omar Mvambo aliyepata kura 84, Francis Mgasa
61 na Frank Mzoo alijinyakulia kura 23.
Mgombea huyo anatarajia kushindana na Fabian
Leonard aliyepitishwa na chama cha CUF pamoja na Ridhiwani Kikwete
anayesubiriwa kupitishwa na kamati kuu ya CCM (CC-CCM).
Mshindi wa uchaguzi huo anatarajia kuziba pengo la
aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki Januari 22
mwaka huu.
Mrema ambaye pia ameteuliwa kuwa Mkuu wa
Operesheni wa Uchaguzi mdogo wa Chalinze, alisema Chadema kina imani
kubwa na Torongey kushinda uchaguzi wa jimbo hilo unaotarajia kufanyika
Aprili 6.
Alisema uchaguzi wa jimbo hilo ni muhimu sana kwa
chama kwa kuwa limeshawahi kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 15
bila ya kuwa na maendeleo yoyote.
Mrema alisema Chadema hakitishwi na historia ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwapitisha baadhi ya watoto wa vigogo
katika chaguzi ndogo mbalimbali za ubunge zilizowahi kufanyika nchini
kama njia ya kuwarithi wazazi wao.
Alizitaja chaguzi zile za Arumeru Mashariki ambapo
CCM kilimpitisha Sioi Sumari kumrithi baba yake marehemu Jeremia
Sumari, Kalenga; Godfery Mgimwa kumrithi William Mgimwa, na hatimaye
uchaguzi wa Chalinze ambapo mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani anatarajia
kuwania.
Naye aliyekuwa mgombea katika kura za maoni katika
kinyang’anyiro cha ubunge ndani ya chama hicho, Omari Mvambo alisema
aliridhishwa na matokeo na mchakato mzima wa uchaguzi.
“Mchakato mzima wa uchaguzi ulienda vizuri na
wagombea wote tuliridhika na matokeo yalikuwa sahihi. Kwa hiyo nimeamua
kujidhihirisha kuwa ntampa nguvu mgombea aliyepitishwa kushinda
uchaguzi,” alibainisha Mvambo.
Mgombea aliyepitishwa na Chadema, Torongey alisema kuwa
anatarajia sifa yake ya uenyeji na historia ya maisha yake duni vitakuwa
moja ya chachu za kushinda wapinzani wake katika uchaguzi unaotarajiwa
kuwa na upinzani mkubwa.
Alisema akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo
hilo, atahakikisha anatatua changamoto za maji, elimu na pia
kushughulikia masuala ya mgogoro baina ya wafugaji na wakulima uliodumu
kwa muda mrefu.Mgombea huyo alichukua fomu maalumu ya tume ya uchaguzi
Mjini Bagamoyo jana ya kugombea ubunge wa jimbo hilo la Chalinze.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment