Rais Jakaya Kikwete |
Taarifa iliyotolewa jana jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, ilieleza mambo manne kufafanua hatua za muswada huo kusainiwa na
Rais Kikwete utakapomfikia.
Ilisema kuwa Ofisi ya Rais, Ikulu, haijapokea muswada huo kwamba
inawezekana umekwishakutumwa kutoka bungeni lakini haujamfikia Rais,
hivyo kama haujamfikia hawezi akawa ameutia saini.
“Pili, muswada huo ukimfikia inatarajiwa kuwa atautia saini kwa sababu
umepitia katika mchakato sahihi na halali wa kikatiba kwa maana ya
kufikishwa bungeni na serikali, kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na
Bunge.
“Tatu, kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana yanafaa kufanywa
katika sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Rais kuwa
ametimiza matakwa ya kikatiba ya kutia saini muswada ambao umepitishwa
na Bunge,” ilisema taarifa hiyo.
Katika sababu ya nne Ikulu ilisema kuwa hii haitakuwa mara ya kwanza
kwa sheria kupitishwa na Bunge, ikatiwa saini na Rais na baadaye
kufanyiwa marekebisho na Bunge baada ya kuonekana umuhimu wa kufanya
marekebisho hayo.
Katika hatua nyingine, Ikulu imeanza mawasiliano na viongozi wa vyama
vya siasa nchini vyenye hoja kuhusu muswada huo kwa nia ya kuandaa
mkutano kati yao na Rais Kikwete.
Taarifa ilisema kuwa mawasiliano hayo yalianza jana kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete kwa Ofisi ya Katibu wa Rais.
Kufuatia matukio yaliyotokea bungeni wakati wa kujadiliwa na
kupitishwa kwa muswada huo na kauli mbalimbali za wabunge wa vyama vya
upinzani na wadau wengine, Rais Kikwete alisema kuwa hoja na kauli za
wanaopinga muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka
katika mchakato wa kutafuta Katiba mpya.
“Kwa mujibu wa maandalizi hayo, Ofisi ya Rais, Ikulu, inaangalia
uwezekano wa kuitisha mkutano huo Jumapili ya Oktoba 13 au Jumanne ya
Oktoba 15, mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.
Hofu ya wengi
Kufuatia kuzagaa kwa taarifa hiyo, matumaini ya wengi yaliyeyuka
baada ya ratiba ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
kutoonyesha jambo hilo kama linarudi bungeni.
Wadau wengi walitumaini kuwa Rais Jakaya Kikwete asingeusaini muswada
huo, kufuatia kauli yake ya kuwataka viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF
na NCCR-Mageuzi waachane na maandamano ya kuupinga na badala yake waketi
na kujadiliana na serikali.
Akizungumza juzi na waandishi wa habari, Lissu ambaye ni mnadhimu wa
kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa busara ya Rais kutaka mjadala na
wapinzani ingeonekana jana kwenye ratiba ya kamati.
Alisema kama Rais hajausaini muswada huo, ratiba ya Kamati ya Bunge
ilipaswa kuonyesha kuwa sasa unarudishwa bungeni kufanyiwa marekebisho
ya kasoro zinazolalamikiwa.
Hata hivyo, jana ratiba hiyo iliyotolewa kwa wajumbe wa kamati hiyo,
haikuonyesha jambo lolote kuhusu muswada huo unaopigiwa kelele, jambo
lililozua hisia kuwa umeishatiwa saini na Rais.
Lissu alisema licha ya Rais Kikwete kusema jambo hilo linazungumzika,
sasa amemaanisha kuwa hana nia ya kutosaini muswada huo wenye mapungufu
mengi.
Katika ratiba ya kamati ambayo Tanzania Daima imefanikiwa kupata
nakala yake, wajumbe wake sasa wamepangiwa ratiba ya siku tatu kuanzia
Oktoba 9 hadi 12 kwenda Zanzibar kukusanya maoni ya wadau kuhusu miswada
ya sheria ya kura za maoni 2013 na sheria ya mbadiliko ya sheria
mbalimbali ya mwaka 2013.
Mbowe afunguka
Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, amesema kuwa
Kikwete amemkosea Tundu Lissu kwa kumuita mwongo, mzushi, mfitini na
mzandiki na kwamba anapaswa kumwomba radhi.
Akifungua semina ya siku tatu ya mafunzo ya wakufunzi wa kanda za
CHADEMA jana jijini Dar es Salaam, Mbowe alimtahadharisha Rais Kikwete
kuwa makini na suala la Katiba kwani ni roho ya nchi.
Alisema Katiba ni sheria mama na suala linaloweza kuleta mpasuko,
hivyo anapolizungumzia awe amejiridhisha kuliko kutegemea maneno ya
kuambiwa, kufahamishwa, kuelezwa na washauri wake ambao wamekuwa
wakimshauri vibaya na wakati mwingine kumdanganya.
“Rais awe makini na kauli zake kabla ya kuzungumza na Watanzania na
atumie fursa hiyo kujiridhisha na katika suala la Katiba asifanye
utani,” alisema.
Alisema kuwa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete
ametangaza uhasama binafsi na Lissu kutokana na hotuba aliyotoa bungeni.
Mbowe alisema Rais amemwonea Lissu na kwamba hata mkubwa akikosea
huomba radhi, hivyo katika hilo anapaswa amwombe Lissu radhi.
“Lissu alikuwa akitimiza wajibu wa kibunge, alifanya hayo kwa mujibu
wa kanuni za Bunge na alikuwa anawakilisha maoni ya kambi ya upinzani.
“Nashindwa kuelewa kwa nini Rais hakuelewa hili na maneno aliyotumia
sio maneno ambayo Rais anapaswa kuyatumia anapohutubia wananchi,”
alisema.
Aliongeza kuwa inashangaza kuona Rais Kikwete hana utamaduni wa
kujisomea, kwamba asingesema mjadala wa bungeni ulienda vizuri bila
kusoma kumbukumbu za Bunge (Hansard) au kuangalia mikanda iliyorekodiwa.
“Amezingatia ushauri wa mawaziri wake, kukubali hata mambo ambayo
yamechomekwa katika muswada ulioletwa bungeni,” alisema Mbowe.
Mapema akifungua semina hiyo, alisema CHADEMA imetambua vipaji
mbalimbali katika ngazi za uongozi, hivyo imegatua madaraka kupeleka
kwenye kanda badala ya mamlaka yote kutolewa na makao makuu.
Aliongeza kwamba mkakati uliopo sasa wa CHADEMA ni kuifanya kuwa ya
kidijitali (cha kisasa) katika maana kuwa wakufunzi wapya wataendesha
chama kitaalamu.
Wadau wanena
Wadau mbalimbali wamepokea kwa mitazamo tofauti hotuba ya mwisho wa
mwezi ya Rais Kikwete ambayo imeonyesha mgawanyiko juu ya mchakato wa
Katiba unapoelekea.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana kwa nyakati tofauti, wadau hao
walisema kuwa tangu kuanza kwa mchakato huo umekuwa na dosari, hatua
inayoashiria kuwa kuna uwezekano wa kushindwa kuafikiana.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Bashiru Ally, alisema kuwa ni wazi kuwa mchakato huo unaashiria
kushindwa kupatikana kwa muafaka.
Alisema kuwa mchakato huo umevamiwa na wanasiasa na wameuathiri hivyo itakuwa ndoto kupata Katiba iliyo ya Watanzania.
“Mjadala huu umeingia dosari tangu mwanzo kuanzia kutungwa kwa sheria
yenyewe na hata kuundwa kwa tume ambayo ina sura za mgawanyiko kwani
wale waliopo kila mmoja ana maslai yake binafsi na sio tume ya kitaifa,”
alisema.
Mhadhiri huyo alisema kuwa Katiba inatungwa kwa kuketi chini na
kujadiliana na sio kama inavyotokea ambapo wanasiasa wamebadili muelekeo
na kuitana majina ya wanafiki na wazandiki, jambo ambalo linaashiria
kutokuamiana.
Naye mhadhiri mstaafu wa chuo hicho, Dk. Azavel Lwaitama, alisema kuwa
lugha aliyotumia Rais Kikwete inaonyesha kuwa ni wa kundi la Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Alisema kuwa Rais ameonyesha nia ya kutaka kusaini muswada huo na hilo
linaashiria kuwa Katiba itakayopatikana itakuwa ni ya CCM.
“Kama Rais Kikwete kaonyesha nia ya kutaka mchakato uendelee na asaini
huo mswada basi hakuna haja ya kukutana na wapinzani kama anavyotaka;
itakuwa ni sawa na kupoteza muda tu na wala haja ya kurudisha bungeni,”
alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Habari na Haki za Binadamu wa CUF Zanzibar,
Salum Bimani, alisema kuwa kama hotuba ya Rais Kikwete itaweza
kutekelezwa kuna uwezekano wa kupatikana kwa Katiba ya Watanzania.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment