Takriban wachimba migodi 80,000 wa dhahabu nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kuanza mgomo kudai nyongeza ya mishahara
Wafanyakazi hao wiki jana walikataa
pendekezo walilopewa la nyongeza ya asilimia 6 ambacho ni kiwango cha
mfumuko wa bei kwa sasa.
Sekta ya madini ya dhahabu ndio moja ya sekta
kubwa duniani lakini imekuwa ikikumbwa na misukosuko katika miaka ya
hivi karibuni huku ile ya madini ya platinum ikijikwamua kutokana na
athari za migomo iliyokumba sekta hiyo mwaka jana.
Inakisiwa kuwa migomo hiyo ya wachimbaji migodi ikiwa itafanyika, itapotezea nchi hiyo zaidi ya dola milioni 30 kila siku.
Wamiliki wa migodi wanaonya kuwa migomo hiyo
huenda ikasababisha migodi ya dhahabu kufungwa na maelfu kupoteza kazi
zao kufuatia kushuka kwa bei ya dhahabu.
Wanasema kuwa gharama za uchimbaji dhahabu
zimepanda kwani wamelazimika kutumia pesa nyingi zaidi katika shughuli
nzima za uzalishaji.
Kwa miezi mingi Afrika Kusini ilikuwa nchi yenye
kuzalisha zaidi dhahabu ikiwa inazalisha asilimia 68 ya dhahabu yote
duniani katika miaka ya sabini.
Lakini kwa sasa iko katika nafasi ya tano katika
uzalishaji wa madini hayo ikiwa ni asilimia sita pekee ya dhahabu yote
duniani ingawa bado ni sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi hiyo.
Rais Jocob Zuma ametaka pande zote mbili kwenye mgogoro huu kuafikiana ili kuzuia hasara kwa pande zote mbili.
Wafanyakazi watalazimika kuondoka kazini saa
sita asubuhi kwa mujibu wa msemaji wa chama cha wafanyakazi hao, alisema
Lesiba Seshoka.
Hata hivyo alikanusha madai kuwa nyongeza
wanayotaka ya asilimia 60 ni kubwa sana. Chama cha wafanyakazi cha NUM
kinawakilisha asilimia 64 ya wafanyakazi 120,000 wanaochimba dhabahu
migodini.
Wananchi wa Afrika Kusini walishangazwa sana
mwaka jana wakati polisi walipowaua wachimba migodi 34 wa Platinum
waliokuwa wamefanya mgomo haramu uliokuwa umeitishwa na chama chao na
kutuhumu NUM kuwa na uhusiano wa karibu na serikali.
No comments:
Post a Comment