Friday, September 13, 2013

MWANDISHI WA GAZETI LA MWANANCHI AKATWAKATWA MAPANGA

Mwandishi wa Habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti mkoani Singida, Awila Silla amejeruhiwa baada ya kukatwa na mapanga kichwani na  mtu asiyejulikana.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 2 usiku Jumapili iliyopita maeneo ya Utemini ambapo alivamiwa na mtu huyo ambao mbali na kumjeruhi kwa mapanga, pia alimpiga ngumi na mateke na kumjeruhi katika jicho lake la kushoto.
Silla amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida ambapo alifikishwa na kijana mmoja (jina halikumbuki) ambaye alimkuta akiwa hajitambui.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kuwa hana taarifa yoyote na kuahidi kuwa atafuatilia tukio hilo.
Silla ni mwakilishi wa gazeti hili mkoani humo na huandika zaidi Makala za kijamii na kiutamaduni.
Tangu afikishwe katika hospitali hiyo, watu mbalimbali walikwenda kumjulia hali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone.
Akisimulia mkasa huo akiwa hospitalini, Silla alisema, nilikuwa nikirejea nyumbani muda ya jioni nilipofika maeneo ya Utemini simu yake ya kiganjani ikaita na kulazimika kuzungumza ghafla akatokea kijana ambaye alikuwa amejifunika shuka la kimasai na kuanza kumfuata.
 “Nilipogundua yule kijana ananifuata kwa kasi nikaongeza mwendo lakini kila nilipojaribu kumkwepa alizidi kunifuata mpaka nilipofika karibu na uzio wa nyumba moja akanikaribia na kuanza kunivamia kisha kunibamiza katika geti la nyumba hiyo.”
Alisema baada ya kufanikiwa kunidhibiti akaanza kunicharanga na mapanga huku akidai nimpatie pesa, nikamwambia sina pesa lakini cha kushangaza akasema wewe huwa una hela.
“Alinishangaza sana, inaonekana kama ananijua, lakini kila nilipokuwa namkaribia ili nimjue vizuri alikuwa anazidi kunisukuma nisimgundue.”
Kwa mujibu wa Silla, mtu huyo alimnyang’anya simu pamoja na mfuko uliokuwa na vifaa vidogo ambavyo alitoka kununua yakiwamo mafuta.
Mwananchi

No comments: