Uchunguzi wa kina wa Mwananchi Jumapili umebaini
kuwa kundi hilo limekuwa likiwalenga wanaume walio katika ndoa na wenye
uwezo wa kifedha, ambao baada ya kunaswa katika fumanizi hizo hupigwa
picha zinazogeuzwa mradi.
Utapeli huo unawalenga wafanyabiashara, watu wenye nyadhifa kwenye taasisi na hata viongozi wa dini.
Kundi hilo lenye mtandao mpana nchini, linaonekana katika siku za karibuni kujikita katika mkoa wa Kilimanjaro.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa katika kipindi cha
wiki mbili, watu wanne wamejikuta wakinaswa katika mtego huo na kutoa
kitita cha kati ya Sh3 milioni na Sh10 milioni, gharama hizo zikiwa nje
ya zile za kukomboa picha.
Kundi hilo hufanya kazi kwa kuwatumia wasichana
wadogo na wakubwa, ambao wanaajiriwa maalumu kwa kazi hiyo ambayo
haitofautiani na ya uchangudoa.
Mbali na waume za watu, wengine ambao wamenaswa
kwenye mtego huo ni baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki, ambao
hulazimika ‘kumalizana’ nao wakihofia kuchafuliwa kwa kashfa iwapo jambo
hilo litaanikwa kwa umma.
Katika tukio la hivi karibuni, mfanyabiashara
mmoja wa mjini Moshi alinaswa katika fumanizi hilo na mwanamke mmoja
aliyedaiwa ni mkazi wa eneo la KDC Barabara Kuu ya Moshi-Himo na kulipa
Sh3 milioni.
“Kwa hofu ya taarifa kumfikia mkewe, jamaa yangu
aliamua kutoa fedha walizotaka, na unajua unapofumaniwa akili zinapotea
kwa muda na unakuwa huna ujanja,” kilidokeza chanzo chetu.
Hata hivyo, chanzo hicho kilidai kuwa baada ya
kupita wiki moja, mfanyabiashara huyo alipigiwa simu na mtu
aliyejitambulisha kuwa ni mwandishi wa gazeti moja la udaku akimtaarifu
kuwa ana picha za mfanyabiashara huyo alizopigwa kwenye
fumanizi.
“Baada ya hapo tuliifuatilia namba yake na
tumegundua anaitwa (jina tunalo), lakini kule kwenye lile gazeti
hawamfahamu kabisa wala hiyo namba hawaijui,” alidai ndugu wa
mfanyabiashara huyo.
Alidai kuwa, baada ya kumfuatilia mwanamke
anayedaiwa kufumaniwa na ndugu yao, waligundua pia kwamba, tukio hilo
ulikuwa ni mchezo mchafu.
Ndugu huyo alidai kuwa, mwanamke huyo anafahamika mjini Moshi na
kwamba, anaishi kwa ujanja-ujanja kwani hana kazi maalumu na wala
hajaolewa.
Kati ya matukio 10 yaliyotokea, tapeli huyo
anayejifanya mwandishi wa gazeti hilo la udaku, ndiye anayetajwa
kuhusika kupiga simu, akitishia kuwa asipolipwa, atachapisha picha za
fumanizi.
Imedaiwa kuwa, vigogo wenye nyadhifa mbalimbali katika taasisi kadhaa mkoani Kilimanjaro wameingia kwenye mtego huo.
Padri mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa, pia
anadaiwa kunaswa katika mtego huo na kulipa Sh5 milioni, lakini baadaye
alilazimika kutoa kitita kingine cha Sh3 milioni ili kukomboa picha
zake.
Uchunguzi umebaini kuwa padri mwingine wa shirika
moja alilazimika kutoa Sh6 milioni, baada ya ‘mwandishi’ huyo kumpigia
simu akimweleza ana picha za mtoto aliyezaa na mwanamke mmoja.
“Unajua hawa wenzetu hawaruhusiwi kufanya tendo la
ndoa, lakini baadhi yao tunaowafahamu wana watoto, hivyo wanapotokewa
huwa wanachanganyikiwa,” alidokeza ndugu wa karibu wa padri huyo.
Hata hivyo, baadhi ya wanawake waliohojiwa na
gazeti hili walidai kuwa wako tayari kukilipa kikundi hicho ili waume
zao wafumaniwe na kuaibishwa kama njia ya kuwarejesha kwenye mstari.
Pamoja na kukiri kuwapo kwa mchezo huo mkoani
humo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema uhalifu
huo ni vigumu kuudhibiti kwa vile wanaofanyiwa hivyo hawawezi kutoa
taarifa polisi wakihofia wake zao kubaini uchafu wao.
Alisema kuwa, badala ya waathirika wa matukio
hayo kuwafichua wahusika wa matukio hayo, huamua kufa na tai shingoni
huku wakiendelea kugeuzwa mradi na matapeli hao na kuwaomba wananchi
kutoa ushirikiano ili kikundi hicho cha matapeli kiweze kukamatwa.
Chanzo: gazeti la mwananchi.
Chanzo: gazeti la mwananchi.
No comments:
Post a Comment