Tumbili wapo wa kutosha tu kisiwani hapo.
Ofisi za wasimamizi wa hifadhi ya Taifa ya Saa Nane. Awali kisiwa
hiki kilikuwa ni hifadhi lakini mwanzoni mwa mwezi wa Tisa mwaka huu,
Bunge limekipandisha hadhi na kukifanya kisiwa hiki kuwa Hifadhi ya
Taifa na kuwa chini ya usimamizi wa TANAPA.
Kisiwa cha Saa nane kinafikika kwa njia ya boti tokea jiji la Mwanza.
Boti inayoonekana juu ndio iliyompeleka Mdau Abdul mpaka Kisiwa cha Saa
Nane tokea Mwanza mjini.
Mdau Akiwa kwenye boti tayari kwa kuanza safari kuelekea Kisiwani. Hapa ni akiwa upande wa Mwanza mjini
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
KISIWA CHA SAANANE CHATANGAZWA RASMI HIFADHI YA TAIFA
Kisiwa cha Saanane kimetangazwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa kufuatia Tangazo la Serikali Namba 227 lililotolewa hivi karibuni.
Kutangazwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane kunafuatia
kupitishwa kwa Azimio la Bunge mwezi Oktoba mwaka jana lililoridhia
kupandishwa hadhi kwa kisiwa hicho kutoka Pori la Akiba na kuwa Hifadhi
ya Taifa.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane itakuwa na ukubwa wa kilomita za
mraba 2.18 na itajumuisha maeneo ya lililokuwa Pori la Akiba , Visiwa
vya Chankende kubwa na ndogo pamoja na eneo la maji ya Ziwa Victoria
linalozunguka visiwa hivyo.
Kuanzishwa kwa Hifadhi mpya ya Taifa ya Saanane kutawezesha haja ya
kuongeza spishi mbalimbali za wanyamapori na hivyo kuongeza utalii wa
mjini, utalii wa ndani, utafiti na kutoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi
na wananchi watakaotembelea hifadhi hii mpya.
Aidha, uamuzi huu utasaidia kutunza hali ya bioanuwai, uhifadhi wa
mazalia na makuzio ya samaki na uendelezaji wa utalii wa mjini kuendelea
kuimarika.
Kabla ya kupandishwa hadhi, Kisiwa cha Saanane kilikuwa Bustani ya
wanyama mwaka 1964 kabla ya kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka
1991. Ilipofika mwaka 2006, Serikali ilikikabidhi kisiwa hicho kwa
Shirika la Hifadhi za Taifa kwa ajili ya kukiendesha na kusimamia
mchakato wa kukipandisha hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa.
Kufuatia uamuzi huu, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) sasa litakuwa
na jumla ya Hifadhi 16 nchi nzima ambazo nyingine ni pamoja na
Serengeti; Ziwa Manyara; Tarangire na Arusha.
Nyingine ni pamoja na Kilimanjaro; Mkomazi; Saadani; Mikumi; Milima ya
Udzungwa; Ruaha; Kitulo; Katavi; Gombe; Milima ya Mahale na Kisiwa cha
Rubondo.
Wakati huohuo, eneo la Hifadhi ya Taifa Gombe limeongezwa ukubwa kutoka
Kilometa za mraba 33.74 hadi kufikia kilometa za mraba 56. Uamuzi huu
unatokana na Tangazo la Serikali Namba 228 lililotolewa hivi karibuni
ambalo linafuatia Azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lililotolewa mwaka jana linalohusu kuridhiwa kwa uamuzi wa kurekebisha
mipaka ya Hifadhi ya Taifa Gombe kwa kuondoa eneo la makaburi na
kuliacha kwa wananchi pamoja na kujumuisha eneo la ufukwe wa maji ya
Ziwa Victoria na eneo la ukanda wa maji.
Kuongezeka kwa eneo la ufukwe wa ziwa na ukanda wa maji kwenye eneo la
hifadhi kutaongeza wigo wa shughuli za utalii katika Hifadhi kama vile
kuogelea, utalii wa boti, mitumbwi na uvuvi wa kitalii.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S. L. P 3134
ARUSHA
03.09.2013
No comments:
Post a Comment