Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetahadharisha kuwepo kwa
kimbunga katikati ya bahari kitakachosababisha mvua nyingi za muda
mfupi.
Kwa sababu hiyo mamlaka imewataka wakulima kwenye baadhi ya mikoa hasa
ya kaskazini mwa nchi na iliyopo ukanda wa Ziwa Victoria kupanda mazao
yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.
Viashiria vya vimbunga hivyo vinasababishwa na joto la bahari kupungua
na hivyo kusababisha mvua nyingi za muda mfupi kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi, aliwashauri wakulima wa mikoa
ya kaskazini mwa Dodoma, Singida na Tabora kutafuta ushauri wa maofisa
ugani wa maeneo hayo kwa vile inatabiriwa kuwa na unyevunyevu hafifu kwa
kipindi cha Novemba hadi Desemba.
Alitoa utabiri wa msimu wa Oktoba hadi Desemba na kuwataka wakulima wa
mikoa ya Kagera, Geita, Mara, kaskazini mwa Kigoma, Arusha na
Kilimanjaro kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa sababu hali ya
unyevunyevu wa ardhi utakuwepo wa kutosha.
Mkurugenzi huyo aliyataja maeneo yatakayokuwa na unyevunyevu hafifu wa
udongo kuwa ni Mwanza, Simuyu, Shinyangam Manyara, Tanga, Dar es
Salaam, Unguja, Pemba na Morogoro.
Akizungumzia utabiri wa msimu wa kuanzia Oktoba hadi Desemba alisema
TMA inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wakiwemo wakulima,
wafugaji, mamlaka za wanyamapori, maji na afya wazingatie utabiri huo na
kutafuta ushauri wa wataalamu wa sekta husika ili kuepuka majanga.
Kwa mujibu wa Dk. Kijazi utabiri wa mamlaka hiyo kwa msimu uliopita
ulifanikiwa kwa asilimia 88.2 ambapo maeneo mengi ya nchi yalipata mvua
za wastani.
No comments:
Post a Comment