Baada ya Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kumsaka kwa siku mbili
bila mafanikio mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu
(CHADEMA), akidaiwa kumpiga na kumjeruhi mmoja wa askari wa Bunge,
hatimaye alijisalimisha mwenyewe jana jioni.
Taarifa zilizopo sasa, Sugu alikwenda
polisi akiongozana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wabunge
Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Joshua Nassari
(Arumeru Mashariki).
Akizungumza hapo jana mbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema kuwa Sugu hakukamatwa bali
alijipeleka mwenyewe polisi kwa hiari yake na kwamba jioni hiyo majira
ya saa 1:10 alikuwa akiandikisha maelezo yake.
Wakati Sugu akijisalimisha, wanasheria wa Bunge nao walikuwa
wamejifungia kuangalia namna ya kumkabidhi mbunge huyo mikononi mwa
sheria.
Juzi na jana viwanja vya Bunge vilitawaliwa na idadi kubwa ya polisi
waliotumwa kumkamata Sugu lakini mpaka Bunge linaahirishwa jioni
haikujulikana ni wapi alikokuwa mbunge huyo.
Mbunge huyo juzi baada ya kubebwa mzobemzobe na askari wa Bunge na
kisha kutolewa nje ya ukumbi, inadaiwa kuwa alimpiga ngumi mmoja wa
askari aliyemtuhumu kuwa alikuwa amempia ngumi wakati wakimtoka nje.
Askari hao juzi jioni walikuwa kwenye vikundi vikundi nje ya ukumbi wa
Pius Msekwa ambako kulikuwa kukifanyika mkutano wa wabunge wa upinzani
ambapo Sugu pia alikuwa miongoni mwao.
Kutokamatwa kwa Sugu kumewashangaza wengi waliokuwa karibu na askari
hao kwa kuwa alikuwa amekaa jirani nao akizungumza na wenzake kabla ya
kuanza kwa kikao chao.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa askari hao walishindwa kumkamata Sugu
kwa kuwa hapakuwepo na amri ya kukamatwa kwake na hata ilipotolewa
alikuwa ameshaondoka katika viwanja vya Bunge.
Mpaka Bunge linaahirishwa juzi jioni, idadi kubwa ya askari walikuwa
nje ya milango na korido zilipo ofisi za kambi ya upinzani wakimsubiri
Sugu bila mafanikio.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia
askari kusuasua kukamatwa kwa Sugu ni kutokana na kinga ya kibunge
aliyonayo na pia kosa analotuhumiwa kulifanya alilifanya akiwa kwenye
viwanja vya Bunge.
“Tulipata mtanziko wa kumkamata haraka haraka, ilibidi lazima
tuwasiliane na ofisi ya Spika kujua taratibu za kumkamata kiongozi huyo
hasa kwa kuwa alifanya kosa hilo akiwa bungeni,” kilisema chanzo kimoja.
Wakati askari wakihaha kumtafuta Sugu, mbunge wa Simanjiro,
Christopher Ole Sendeka (CCM), jana aliomba mwongozo wa Spika kuhusu
tukio la vurugu zilizotokea juzi bungeni hasa tukio la Sugu kumpiga
askari.
Sendeka alisema tukio hilo limelidhalilisha Bunge na askari
wanaowalinda, hivyo akataka liweke wazi ni hatua gani zitakazochukuliwa
dhidi ya mbunge huyo ili kulinda heshima ya chombo hicho.
“Nataka nijue ibara ya 100 ambayo humpa kinga mbunge na uhuru wa mawazo akiwa ndani ya Bunge inatumikaje katika tukio hili?
“Je, Bunge litalindaje heshima yake dhidi ya tukio hili lililofanywa na mbunge mwenzetu?” alihoji.
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema
tukio hilo ni geni hivyo Bunge limeshindwa kutoa jibu la mara moja.
“Jambo hili halijawahi kutokea katika historia ya Bunge, sasa nami
nitalifikisha kwa wanasheria wa Bunge wanishauri namna ya
kulishughulikia na baada ya hapo nitatoa mwongozo,” alisema.
Akitoa mwongozo huo muda mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa jana jioni,
Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kuwa bado wanashauriana na wanasheria
kuona kanuni zinawaelekezaje.
Alisema kuwa licha ya tukio hilo kutokea katika eneo la Bunge bado
kitendo hicho ni cha jinai na hivyo, mtuhumiwa atashughulikiwa kisheria.
“Ni sawa na jaji yuko mahakamani ambapo kuna kinga kama za Bunge
halafu jaji mwenzake ampige ngumi. Huyo lazima achukuliwe hatua hawezi
kuachwa. Kinga zetu ziko kwenye uhuru wa mawazo tu,” alisema.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, juzi lilitangaza kumsaka Sugu kwa tuhuma za kufanya vurugu na kumjeruhi askari wa Bunge.
“Lakini tuna mashaka sana na hatua yake aliyoifanya nje ya ukumbi
ambapo alimvamia na kumpiga ngumi nzito Koplo Nikwisa Nkisu ambaye
alijeruhiwa jicho,” alisema mmoja wa askari ambaye hakutaka jina lake
litajwe.
Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Dodoma ASP Jumanne Kim, juzi jioni
alithibitisha kusakwa kwa mbunge huyo aliyeondoka maeneo ya Bunge mchana
akiwa ndani ya gari la kiongozi mkuu wa kambi rasmi ya upinzani
bungeni, Freeman Mbowe.
CHANZO: TANZANIA DAMA
No comments:
Post a Comment