Friday, September 6, 2013

KAMBI YA UPINZANI KUMTAKA JOB NDUNGAI AOMBE RADHI..

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aiombe radhi Kambi ya Upinzani kwa kitendo cha kumtoa ndani ya Bunge kiongozi wa kambi hiyo bungeni, Freeman Mbowe. 
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Mtatiro alisema kitendo hicho ni ukiukaji wa kanuni na sheria za Bunge, na kimeidhalilisha kambi hiyo.
“Tukio lililotokea jana (juzi), si la kawaida, Naibu Spika ni kiongozi wa Bunge lakini wapo watu wakubwa ambao wanapaswa kuheshimika sana.

“Kambi ya Upinzani ina kiongozi wake ambaye ni Freeman Mbowe mwenye nafasi kubwa kama aliyonayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

“Tofauti ya Pinda ipo nje ya Bunge wakiwa ndani ya Bunge wote wana heshima ya kufanana.

“Sijui jeuri ya Ndugai imetoka wapi hivi Pinda angekuwa amesimama Naibu Spika angewaamuru askari wa Bunge wamtoe? Ndugai anapaswa kuomba radhi kwa njia ya ustaarabu tu,”alisema Mtatiro.

Naye Oliver Oswald anaripoti kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba amelishauri Bunge kutumia mfumo wa kupiga kura katika kutafuta au kutoa uamuzi kuepusha mizozo ya mara kwa mara inayozidi kujitokeza katika vikao vya bunge mjini Dodoma.

Alisema inafaa utaratibu huo ukatumika bungeni kurudisha nidhamu iliyopotea kwa kipindi kirefu kwa sababu mizozo hiyo inazidi kutoa sifa mbaya kwa wapiga kura na jamii kwa ujumla.

No comments:

Zilizosomwa zaidi