Friday, September 27, 2013

HIZI NDIO NJIA MPYA ZA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI..

Tohara kwa wanaume inatajwa kama mbinu nyingine mbadala ya kupambana na Ukimwi.
Mapambano dhidi ya Ukimwi nchini  kwa miaka mingi tangu kuzuka kwa ugonjwa huo mwaka 1983 yamehusisha mbinu za aina nyingi ikiwamo ya kampeni za aina mbalimbali.
Mbinu hizo zimeonyesha  mafanikio, ingawa sasa mbinu hizo hazina budi kutazamwa upya.
Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), kwa upande wake imejiwekea lengo la kupunguza maambukizi mapya ya Ukimwi,  kuzuia maambukizi hayo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ili, kutoa dawa kwa wanaoishi na virusi (ARVs), miongoni mwa zile nyingi ili kwenda sambamba na malengo  kumi ya Umoja wa Mataifa (UN) ya mwaka 2011 ambayo Tanzania iliyaridhia.
Mambo kumi yameainishwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Tacaids, Dk Fatma Mrisho na kuyataja   kuwa:
Kupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa njia ya kujaamiiana, kupunguza maambukizi kwa wanaojidunga sindano za dawa za kulevya, kutokomeza maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kufikia lengo la kuwa watu milioni 1.5 walioanza na kuendelea kutumia ARVs, kupunguza vifo vinavyotokana na Ukimwi, Kifua Kikuu, kupunguza mahitaji ya rasilimali fedha za Ukimwi.
Mengine ni,  kuondoa tofauti za kijinsia, uonevu na ukatili wa kijinsia na kuongeza uwezo wa wanawake na watoto kujilinda dhidi ya Ukimwi, kuondoa kabisa unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, kuondoa pingamizi za usafiri kati ya nchi moja na nyingine kwa wanaoishi na Ukimwi, kuboresha mifumo ya kutolea huduma za Ukimwi kwenye sekta ya afya.
Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Raphael Kalinga anasema pamoja na kuifanyia marekebisho Sera ya Ukimwi ya mwaka 2001, pia  wanabuni  mbinu mpya za mapambano ambazo  zitapewa msukumo mpya.
Anaitaja njia hiyo kuwa  ni ya kumshirikisha mtu mmoja mmoja katika jamii kwenye mapambano ya sasa ya Ukimwi. Mbinu hiyo, mtaalamu huyo  anaeleza kuwa ndiyo inatarajiwa kuwa yenye manufaa na tija kwani itamwezesha  kila Mtanzania kutambua mchango wake binafsi katika vita dhidi ya Ukimwi.
Mtu binafsi hana budi kuelewa kuwa yeye ndiye mgonjwa, mtoa huduma badala ya kusubiri mipango ya jumla jumla ikiwamo ya mabango, matangazo, maigizo ambayo imekuwa ikihusisha kijiji, tarafa, wilaya, mkoa au taifa,” anaeleza Dk Kalinga.
Aidha, Dk Kalinga aliwaeleza wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari katika darasa maalum ulililoandaliwa na Tacaids jijini Dar es Salaam kuwa pamoja na mbinu hiyo, pia matumizi ya baadhi ya maneno, misemo haina budi kuangaliwa upya ili kuepuka na upotoshaji.
Majina potofu ya Ukimwi
Anaitaja mifano michache ya majina dhidi ya Ukimwi kama, gonjwa baya, miwaya, ngoma ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa  ikitumika katika jamii nyingi na kuongeza kuwa Ukimwi hauna budi kuchukuliwa au kutazamwa kama magonjwa mengine hatari ambao pia  unaua.
Anaongeza kuwa baada ya kila mtu kujitambua, kujikubali kisha akahamasika, mapambano dhidi ya Ukimwi yatakuwa yamepata mtazamo mpya. Anasema kuwa hilo litasaidia kupambana na unyanyapaa unaoanzia kwa mtu mwenyewe, ambao ukifikia kwenye ngazi ya jamii umekuwa na madhara  mengi yakiwamo ubaguzi, kutengwa wagonjwa, waathirika majumbani au sehemu za kazi, mambo ambayo yanakwamisha kampeni na mapamban katika jamii.
Mchango wa vyombo vya habari
Aidha, Dk Kalinga anaeleza kuwa mchango wa vyombo vya habari nchini katika mapambano dhidi ya Ukimwi hauna budi kuangaliwa upya, hasa wakati huu ambao rasilimali fedha zimezidi kuwa finyu kutokana na wahisani kubadili mwelekeo na  vipaumbele vyao.
Katika hilo, inaelezwa kuwa baadhi ya wahisani wameonyesha kutokuwa tayari kuendelea kuchangia miradi ya Ukimwi baada ya mwaka 2016, jambo ambalo limeacha pengo ambalo halina budi kuzibwa na serikali.
Hadi sasa, wahisani wakubwa wa miradi mbalimbali ya Ukimwi ni Serikali ya Marekani na Mfuko wa Global Fund, ambao wamekuwa wakichangia asilimia 80 za fedha zote.  Tacaids inaeleza kuwa zinahitajika  karibu trilioni moja, lakini fedha zinazopatikana ni karibu Sh500 milioni kwa mwaka.
Dk Mrisho anaongeza kuwa vyombo vya habari nchini mara nyingi vimesubiri kashfa kama ile ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs), badala ya kuwa mstari wa mbele kuibua na kueleza changamoto mbalimbali zinazokabili mapambano dhidi ya Ukimwi.
Akashauri juhudi  zote zinazoendelea katika mapambano dhidi ya Ukimwi, ikiwamo za kukemea unyanyapaa, ubaguzi kama njia zinazokwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo ziachwe, huku tiba na ushauri ukipewa kipaumbele.
Tohara kwa wanaume
Hii inatajwa kama mbinu nyingine mbadala na ambayo haina budi kuangaliwa upya kwa sasa hasa katika maeneo yote nchini ambayo tohara hizo zimekuwa  hazifanyiki.
Hali kadhalika, wanaume wameshindwa kujitokeza kwa hiari kupima afya zao ikilinganishwa na wanawake.  Hadi sasa Watanzania milioni 16 ndiyo wamejitokeza, kupima afya zao, kati yao 710,000 wamekutwa na virusi na kati ya hao, 663,911  ndiyo wamefikiwa, ingawa wanawake ndiyo wengi zaidi.
Wanaume, bado wamekuwa  wakichelewa kuanza kutumia huduma zikiwamo za Ukimwi pamoja na ARVs licha ya vituo kusambaa kote nchini.  Hadi sasa, Tacaids imeweka lengo la kuwafikia watu 700,000 ifikapo mwaka 2015.
Kuhusu tohara, Dk Kalinga anaeleza kuwa tohara hugharimu dola 42 (Sh68,000) kwa ajili ya kumwandaa, kumtahiri, kumhudumia mtu hadi apone na kuonya kwamba  tohara isichukuliwe kuwa kinga dhidi ya ugonjwa huo, bali  ni njia ya kupunguza maambukizi .
Anawashauri wanaume waache tabia  zikiwamo urithi, kutakasa wajane au kuendekeza mila nyingine potofu katika jamii hasa zile zinazochochea Ukimwi.
Njia nyingine  ni pamoja kuhimiza matumizi sahihi ya kondomu (zile za kike na kiume) kwa kila tendo la kujamiiana, akieleza kuwa tayari kondomu 70,000 ziliagizwa na serikali. Hata hivyo, anasema kiasi kikubwa bado zipo kwenye vituo vya afya vya umma. Pia, anatambua mchango wa mashirika binafsi ambayo yamekuwa yakiingiza, kusambaza kondomu nchini.
Kwa nini kondomu zikose wateja?
Jibu ni kuwa baadhi ya Watanzania hawana  elimu ya kutosha kuhusu kondomu na matumizi yake sahihi, ingawa wakati mwingine matumizi yake yamekuwa yakipingwa  kwa imani za kidini na maadili.
Dk Kalinga anaongeza  kuwa woga, hofu kwa baadhi ya  watu imekuwa ni sababu nyingine kubwa ya wao kuendelea kushindwa kuzitumia ipasavyo kondomu na kwa usahihi kama kinga na njia ya kuepuka maambukizi.
Anaongeza kuwa wakati mwingine huduma hiyo imebakia kuwa siri, kiasi kwamba watumiaji wengine hawajui ni wapi kondomu hizo zinapatikana.
Dk Mrisho kwa upande mwingine anaeleza kuwa pamoja na kampeni zile ambazo zimekuwa zikiendelea, maambukizi yamepungua, lakini  si jambo la watu kubweteka  na kurudia ngono zembe.
Anayataja makundi hatarishi  yenye maambukizi  yanayoongezeka kuwa ni wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao (mashoga), vijana wa kike , kiume wanaojidunga sindano za dawa za kulevya, wanawake wanaoshiriki biashara  ya ngono na wale ambao hufanya mapenzi kinyume cha maumbile.

No comments: