Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda
jana alisababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro
baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa
kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi inayomkabili katika Mahakama
ya Mkoa wa Morogoro.
Tofauti
na Agosti 19, mwaka huu wakati aliposafirishwa kwa helikopta, jana
Sheikh Ponda alisafirishwa kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi
Morogoro akiwa chini ya ulinzi.
Mbali
ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kufungwa, nyingine ni Hazina
Ndogo, Madini, Posta, Vipimo, Ukaguzi na Maktaba ya Mkoa.
Sababu
za kufungwa kwa ofisi hizo pamoja na Mtaa wa Stesheni na maeneo ya
Posta ni kuwa jirani na Mahakama hiyo. Magari yalizuiwa kutembea katika
njia na maeneo ya karibu na ofisi pamoja na Mahakama hiyo huku kukiwa na
idadi kubwa ya askari polisi na magereza kwa muda wote wa takriban saa
mbili.
Alifikishwa
mahakamani hapo saa 4:10 asubuhi akiwa katika basi la Magereza ambalo
lilisindikizwa na jingine dogo, huku magari mengine yakisimamishwa
kupisha msafara huo. Mahakama hiyo ilifurika umati wa wafuasi wa
kiongozi kiasi cha kuwalazimu polisi na wana usalama wengine kuweka
utepe kuwazuia wengi wao kufika katika jengo lililokuwa likitumika
kuendesha kesi hiyo.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Shughuli
katika eneo hilo zilirejea katika hali yake ya kawaida saa 6:25 mchana
baada kesi yake kuahirishwa na msafara wa Sheikh Ponda kurejea katika
Gereza la Segerea, Dar es Salaam ambako yuko rumande.
Muda
wote tangu kuwasili mpaka kusikilizwa kwa kesi hiyo, wafuasi hao
walikuwa kimya hadi pale ilipoahirishwa na hasa baada ya Sheikh Ponda
kuwapungia mkono alipokuwa akielekea kwenye basi ambako walisikika
wakisema: “Takbriir na kuitikia Allahu Akbar – (Mungu Mkubwa).”
Kesi yenyewe
Katika
kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Benard Kongola alisema mbele ya Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate kuwa Sheikh Ponda
alitenda makosa ya uchochezi Agosti 10, mwaka huu saa 11.45 jioni kwenye
maeneo ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro.
Alisema
siku hiyo, Sheikh Ponda alialikwa kutoa maelezo machache kwenye
Kongamano la Eid lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri Mkoa wa Morogoro
(Uwamo) na kwamba akiwa hapo alitamka maneno: “Ndugu Waislamu, msikubali
uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo
zimeundwa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), ambao ni vibaraka wa
CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha
kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango
na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana,” huku akijua kutoa
maneno hayo ni kosa kisheria.
Alisema
kwa kufanya hivyo, Sheikh Ponda anayetetewa na mawakili watatu
wanaoongozwa na Juma Nassoro, alivunja masharti ya Mahakama ya kifungo
cha nje iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka
huu iliyokuwa imetamka kuhubiri amani.
Katika
shtaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kutenda
kosa la jinai kwa kuwaambia: Serikali ilipeleka jeshi Mtwara
kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka
na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu,
lakini haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa Mwarabu
asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa
sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.” Shtaka la tatu ni
kudaiwa kutamka maneno yaliyoumiza imani ya watu wengine kama yalivyo
katika shtaka la pili.
Baada
ya kusoma mashtaka hayo, Kongola alisema walikuwa na mashahidi 15 na
vielelezo vitatu ambavyo ni DVD mbili na kibali kilichotolewa na Mkuu wa
Polisi Wilaya ya Morogoro(OCD), Agosti Mosi, 2013 cha kongamano husika
na hati ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, Mei 9, 2013.
Baada
ya kusomewa, Sheikh Ponda alikana mashtaka yote matatu huku akikubali
kuwemo kwenye kongamano hilo. Alikiri kukamatwa na polisi Agosti 11, Dar
es Salaam.
Wakili
wa utetezi, Nassor aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja akisema
mashtaka hayo yote kisheria yana dhamana. Pia aliwasilisha ombi la
kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwani alisema kuwa kutokana na upelelezi upande wa mashtaka
kukamilika, wanahitaji maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa utetezi.
Hata
hivyo, Wakili Kongola aliiomba Mahakama kutompa dhamana mshtakiwa
kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga
dhamana ya mshtakiwa huyo kwa masilahi ya usalama wa nchi.
Akitoa
mwongozo wa maombi yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Hakimu Kabate
aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, mwaka huu itakapotajwa tena na
kwamba Septemba 17, mwaka huu Mahakama itatoa uamuzi endapo mshtakiwa
atapewa dhamana au la wakati itakapoanza kusikilizwa.
No comments:
Post a Comment