Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji
Peter Msigwa (Chadema) amesema kama Rais Jakaya Kikwete anadhamira ya
kweli kutokomeza ujangili nchini ni vyema akasafisha kwanza Serikali na
chama chake. (HM)
Akihutubia mkutano wa hadhara
uliofanyika Viwanja vya Mwembetogwa mjini hapa juzi, Mchungaji Msigwa
alisema kasi ya ujangili ni kubwa na baadhi ya wahusika ni vigogo ndani
ya CCM.
Alisema wengine wanatoka serikalini
hususan jeshini; Idara ya Usalama wa Taifa na Polisi jambo
linalosababisha operesheni hiyo kuwa ngumu kwa utekelezaji.
Alisema hali hiyo ndiyo chanzo hata cha Operesheni Tokomeza Ujangili iliyositishwa kwa muda kupoteza mwelekeo.
"Tulipoanza kupiga kelele juu ya
vitendo vya ujangili tuliambiwa tunataka umaarufu kisiasa, lakini hali
ilipofikia wao wenyewe wamekubali na kuanzisha hata Operesheni Tukomeza
Ujangili, lakini niliwaambia mtandao wa ujangili ni mkubwa," alisema
Mchungaji Msigwa na kuongeza:
"Unahusisha vigogo ndani ya CCM, si
mnakumbuka niliwahi kuwatajia majina na kuwaambia wawekwe mbali na
Tembo... baadhi yao ni polisi wengine ni wanajeshi, kama kweli Rais
Kikwete ana nia ya dhati kupambana na ujangili ni vyema akasafisha
nyumba yake kwanza."
Mchungaji Msigwa alisema Serikali
ilianzisha Operesheni Tokomeza Ujangili kwa nia njema, lakini kwa sababu
majangili wanatoka ndani ya Serikali hivyo imekuwa vigumu kufanikisha
kazi hiyo. Alisema ndiyo sababu hata malengo yake yalipotoshwa, huku
walengwa wakiachwa na kuanza kuua raia wasio na hatia.
Mbunge huyo alisema hivi sasa kasi ya
ujangili inatisha na kuongeza kuwa, kwa siku zaidi ya Tembo 60 wamekuwa
wakiuawa jambo linalowafanya wanyama hao muhimu kuwa hatarini kutoweka.
Alisema hatua ya mawaziri wanne
kujiuzulu inaonyesha dhahiri wabunge wa upinzani na Bunge kwa jumla
limetekeleza wajibu wake na kwamba, hiyo inatosha kujiaminisha kwa
wapigakura wao.
Hata hivyo, Msigwa alisema msimamo
wake ni kwamba Serikali ina viongozi mzigo, huku akimtaja Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kuwa ni kiongozi mzigo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment