Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka
2013, imebainika kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote
waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku
wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili.
Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa,
imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka
jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia)
kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo
kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule
uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha
pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato
cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili
kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha
pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya
pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje
ya mfumo rasmi.
Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16
mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na
Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu
nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na
Shule Binafsi (Tamongsco).
Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao
kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na
masomo ya kidato cha tatu.
“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na
kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo
imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na
asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi
watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara
ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya
mfumo rasmi.”
Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa
wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu
mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa
kufikisha alama 30 watatimuliwa.
“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi
39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,”
inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale
walioshindwa kwa mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi
atakayerudishwa nyumbani.”
Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha
kuwa inawapa taarifa mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili
kusimamia utekelezaji wa uamuzi kuhusu matokeo hayo.
Kauli ya wizara
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome
alisema, “Suala la wizara kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na
masomo ya kidato cha tatu mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo
watakaorudia.”
Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za
matokeo hayo na uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila
shule ina taarifa hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”
Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili
mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo
ya kidato cha pili yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”
“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama
matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha
pili ni kama mwendelezo wa tathmini ‘Continuous assessment’ kwa
mwanafunzi, hutumika pia katika mtihani wa kidato cha nne.”
Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika
shule husika. “Baada ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo
inaweza kutolewa taarifa za matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk
Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo,
lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Msimamo wa Tamongsco
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin
Nkonya kueleza kama wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema,
“Inaonekana Serikali haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).”
“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na
ufaulu mdogo kuendelea na masomo katika mfumo wa vidato (formal
education), lazima tutegemee kuona wanafunzi wakifanya vibaya katika
mitihani ya kidato cha nne.”
Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni
Watanzania wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali
kwa sababu siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo
ya kisiasa ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania
wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.
“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa
wamekubali kupoteza muda wa vijana wetu huku wakijua kwamba watafika
kidato cha nne, kupata daraja sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza
dawa za kulevya, bangi, wizi na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria,
kanuni na taratibu,” alisema.
Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa
kuendelea na masomo yao; “Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya
asilimia 45 aondolewe katika mfumo wa elimu ya vidato (formal
education) na kuingizwa katika mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET -
Technical education and vocational education).”
Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586
kati ya vyuo 750 vya ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati
ya vyuo 1988 vya ufundi stadi (technical institutes) ambavyo
vinasimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).
“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote
ambao wana ufaulu wa chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu.
Kikwazo pekee kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za
uendeshaji wake.”
“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za
ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama
ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.
Kidato cha pili 2012
Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923
kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli
ilikuwa sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana
62,903, waliofaulu walikuwa wanafunzi 245.9,32.
No comments:
Post a Comment