Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula
Edward Lowassa (HM)
Unaweza kusema sasa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula
kusema kuwa wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015
watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini;
"Wapo watu wanataka waichanechane CCM
kwa sababu ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata
urais. Kuna makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe
hatuwezi kuyafumbia macho."
Akifafanua hilo Mangula alisema:
"Tutawaita wote walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji
kwanini wanafanya hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza
katika mikutano wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua dhamira yao ni nini."
katika mikutano wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua dhamira yao ni nini."
Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa
imepita siku moja tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye kusema mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania
urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya
Lowassa siku mbili zilizopita, kutangaza nia 'kimtindo' akisema anaanza
rasmi safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza
ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya
uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa
mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa
2015, alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka
mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika
wa Monduli.
Mangula aliwashukia vigogo wa chama
hicho wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati
ya Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa
salamu za mwaka mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.
Ataja kanuni za uongozi
Katika mkutano huo Mangula alisaidiwa
kusoma kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea ufafanuzi
mambo mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa
CCM na wanachama taifa, Masoud Mbengula.
Moja ya kanuni hizo inasema "Ni mwiko
kwa kiongozi wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au
eneo analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye
mwenyewe ama mgombea anayemuunga mkono."
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni
za chama hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa
msaliti na hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza
chama wakati wowote.
"Tutawachukulia hatua kali wale wote
ambao wameanza kuonyesha dalili kama hizo za kutoa michango, misaada,
zawadi. Lengo la mwanachama huyo ni kutaka kuungwa mkono, wanaotaka
madaraka wasubiri muda ufike ndiyo wafanye hivyo."
Aliongeza "Hivi haya mapenzi ya
kusaidia yameanza lini, fedha hizo zinatoka wapi, hawa wanaosadiwa
wanatakiwa kutambua kuwa yote hayo ni kampeni kwa kuwekeza, hatuwezi
kuwa na viongozi wa nchi wa namna hii wa uchu wa madaraka, CCM
haitawafumbia macho lazima kanuni na miongozo ifuatwe."
"Kuna watu wameanza kudhani kuwa muda
wa kampeni umeanza, muda wa kampeni haujafika na hakuna majina
yaliyotangazwa ya kugombea udiwani, ubunge hata urais," alisema Mangula
na kuongeza;
"Kuna makundi yanaifanya nchi ya
Somalia isitawalike. Makundi ya aina hiyo naona yapo hata CCM; watu
wanaibua vita ya maneno ndani ya chama, wanataka wakichanechane chama
kwa sababu ya uroho wa madaraka tu."
Bila kuyataja makundi hayo Mangula
alisema: "Utaongozaje nchi ambayo imegawanyika katika makundi? Watu
wameanza kuvuruga chama chetu, kila mtu
ana kundi lake na wakati mwingine wanayatumia makundi kuwabomoa wenzao, hili jambo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo."
ana kundi lake na wakati mwingine wanayatumia makundi kuwabomoa wenzao, hili jambo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo."
Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa
kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Makamba hivi karibuni amekuwa akitoa
misaada kwa vikundi vya waendesha bodaboda katika mikoa mbalimbali, hali
ambayo inatafsiriwa kuwa ni kujiimarisha kisiasa.
Hata hivyo, mwaka jana Rais Jakaya
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa alinukuliwa akisema kuwa
sio vibaya kwa wanachama wa chama hicho kuonyesha nia ya kuwania nafasi
za uongozi ndani ya chama, lakini siyo kufanya kampeni.
Mei 26 mwaka jana, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Iringa, alisisitiza kwamba chama
kitamwadhibu bila huruma mwanachama yeyote anayejipitisha katika maeneo
mbalimbali na kufanya kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.
Akifunga mafunzo ya makatibu na
wenyeviti wa wilaya na mikoa mjini Dodoma mwaka jana, Rais Kikwete
alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza
kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya
kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama
bunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo
watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali
za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea
kukishushia hadhi chama hicho.
Uchaguzi Serikali za Mitaa
Mangula akizungumzia uchaguzi wa
serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu alisema, viongozi wote
wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni na kujiepusha na vitendo vya
rushwa.
"Vitendo vya rushwa ndio vilitufanya
katika chaguzi zilizopita kufanya vibaya, watu walinunuliwa kadi, sasa
viongozi wa matawi wawe makini tusirudi tulikotoka na tukibaini mtu
hafuati kanuni tutamwajibisha," alisema Mangula.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment