Wahamiaji haramu 194 waliorudishwa
makwao wakati wa kutekeleza awamu ya kwanza ya Operesheni Kimbunga
iliyoisha mwishoni mwa wiki iliyopita, wamekataliwa na nchi zao na
kurejeshwa tena nchini. Mamlaka zinazohusika na operesheni hiyo zimesema
kuwa wamewapokea tena watu hao wakati wanasubiri hatua za kisheria
kuchukuliwa.
Awamu ya kwanza ya operesheni hiyo
ilianza Septemba 6 na kuhitimishwa Septemba 20 mwaka huu baada ya baadhi
ya wahamiaji haramu, kukaidi mwito wa Rais Jakaya Kikwete wa kurejea
makwao na kama wanataka kurudi, wafuate utaratibu wa Sheria.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Kamishna wa
Polisi, Simon Sirro, ilieleza kuwa watu hao pamoja na kutokuwa na sifa
ya kuwa raia wa Tanzania, wamerejeshwa nchini kwa kuwa pia wamekosa sifa
ya kuwa raia wa nchi jirani ambako Serikali iliwapeleka baada ya vigezo
kuthibitisha kuwa ni raia wa nchi hizo.
"Hadi kufikia mwisho wa Awamu ya Kwanza
wa Operesheni hii, timu ya Operesheni imefanikiwa kukamata wahalifu wa
unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na washirika wao na kuhakiki uraia
wa watuhumiwa wa uhamiaji haramu," alisema Sirro.
Kwa mujibu wa Sirro, kati ya
waliokamatwa wapo watuhumiwa 212 wa unyang’anyi wa kutumia silaha na
majangili ambao ni raia wa Tanzania 23.
Silaha Silaha zilizokamatwa ni mabomu 10
ya kutupwa kwa mkono, silaha 61 zikiwemo bunduki aina ya SMG (50,
Shotgun (8), Mark IV (1), Riffle (1), pistol (1), pisto za kienyeji (3)
na magobori 42 pamoja na mitambo miwili ya kutengeneza silaha aina ya
magobori.
Zingine ni risasi 665 zikiwemo za
bunduki aina ya SMG na SAR risasi 561, shotgun risasi 22, gobori risasi
82 na fataki 8, suruali sare za Jeshi na kibuyu cha maji vya Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Sirro aliongeza kuwa wahamiaji haramu
12,704 wamekamatwa, kati yao Wanyarwanda 3,448, Warundi 6,125, Waganda
2,496, Wakongo 589 Wasomali 44, Myemeni mmoja na raia wa India mmoja.
“Wahamiaji haramu 2,129 walikubali
kuondoka nchini kwa hiari yao; 8,696 waliondoshwa nchini kwa amri ya
Mahakama baada ya kupewa hati ya kufukuzwa nchini na 1,852 waliachiwa
huru baada ya Serikali kuthibitisha uraia wao wakati wengine 2,286
wanaendelea na mahojiano ili kuthibitisha uraia wao,” alisema.
Kiongozi huyo wa operesheni alisema
ng’ombe 8,226 walikamatwa wakiwa wanachungwa katika hifadhi za misitu na
Sh milioni 32.5 zimepatikana, ikiwa ni tozo za faini ya ng’ombe
walioachwa kwenye hifadhi ya Taifa.
Vingine vilivyokamatwa ni ngozi za
wanyama aina ya duma (1), swala (2), nyati (1) na vipande 10 vya nyama
vinavyodhaniwa kuwa nyara za Serikali.
Vingine vilivyokamatwa ni vipande viwili
vya meno ya tembo pamoja na mbao 2,105, magogo 86, mkaa magunia 467,
pombe haramu ya gongo lita 375 na mtambo wa gongo mmoja . Pia wamekamata
bangi kilo 77 na makokoro yanayotumika kuvua samaki kinyume cha sheria.
"Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Kagera
unaongoza kwa kukamata wahamiaji haramu 7,001, ukifuatiwa na mkoa wa
Kigoma uliokamata wahamiaji haramu 5,005 wakati mkoa wa Geita wahamiaji
haramu waliokamatwa walikuwa 698," alisema Sirro.
Sirro alisema pamoja na mafanikio
yaliyopatikana, kumekuwepo na changamoto zilizojitokeza, ikiwa ni pamoja
na hali ya maisha mchanganyiko ya Watanzania asilimia 60 na wahamiaji
asilimia 40 katika mikoa ya mpakani.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni
baadhi ya wananchi wenye nia mbaya au kulipizana visasi, waliotaka
kutumia operesheni hiyo kukomoana kwa kuwataja baadhi ya watu kuwa ni
wahalifu kumbe ni uongo.
Nyingine ni baadhi ya wahamiaji baada ya
kukamatwa walikosa sifa za uraia wa Tanzania na hata waliporudishwa
kwenye nchi wanazodhaniwa kutoka, walikosa sifa za uraia na kuleta
mgongano kuhusu uraia wao. Alisema ukosefu wa vitambulisho vya uraia
ulisababisha ugumu wa kutambua wahamiaji haramu.
Pia kutokuwepo kwa uzio katika mipaka ya
nchi yetu, kumesababisha wahamiaji haramu wanapopelekwa kwao, kurudi
kupitia njia za panya. Matarajio Sirro alisema baada ya kukamilisha
Awamu ya Kwanza ya Operesheni Kimbunga, wanatarajia Serikali
itashughulikia changamoto zilizojitokeza, ili kupunguza baadhi ya
matatizo katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita hususan yanayohusu
uhalifu na masuala ya kiuhamiaji.
"Tunatarajia kuanzisha kikosi kazi kila
mkoa, kwa ajili ya ufuatiliaji wa wahalifu sugu wanaotumia silaha za
kivita na wale wanaowafadhili," alisema Sirro.
Alisema uhamasishaji utafanyika kuanzia
ngazi ya familia, kitongoji, mtaa/kijiji, kata, tarafa, wilaya mkoa na
taifa, ili jamii iimarishe misingi ya ulinzi na usalama kupitia kamati
zilizopo na kutoa taarifa mara moja panapojitokeza jambo lolote
linalohusu ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Alisisitiza kuwa watajipanga kimkakati,
ili kuona namna ya kushughulikia baadhi ya wahamiaji haramu waliokosa
sifa za uraia na kurudishwa nchini mwao, ambao wanang’ang’ania kwa
kusema wao ni Watanzania.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment