Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani ametawazwa
kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar na kusema
ameshangazwa na mashambulizi ya tindikali dhidi ya viongozi wa dini
Visiwani humo.
Akizungumza na waaandishi wa habari
mara baada ya kutawazwa ndani ya Kanisa la Anglikana la Minara Miwili
Mjini Unguja, Jaji Ramadhan amesema vitendo vya hujuma vinavyofanywa
dhidi ya viongozi wa dini na Serikali ni kinyume na utamaduni wa
Zanzibar.
Alisema Wakristo na Waislamu Zanzibar
kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kama ndugu bila ya kubaguana kwa
sababu za itikadi ya dini licha ya Waislamu kuwa asilimia 95.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa wakristo
wana mchango katika harakati za ukombozi wa Zanzibar, ambapo idadi kubwa
ya waumini wake walianzisha Chama cha African Association mwaka 1935,
ambapo rais wake wa kwanza alikuwa hayati, Mzee Augustino Ramadhan na
baadaye akafuata hayati Mzee Abeid Amani Karume.
"Vitendo vya watu kumwagiwa tindikali
vinanishangaza, sababu halisi siifahamu, najiuliza haya yametokea wapi,
siyo jambo jema wala siyo sifa ya Zanzibar tokea enzi na enzi," alisema.
Alisema wakati umefika na kuwataka
viongozi kuwa mstari wa mbele kukemea matukio ya hujuma za tindikali na
uhalifu mwingine ikiwemo mashambulizi ya kutumia silaha za moto na watu
kupotezewa maisha.
Jaji Augustino amewahi kuwa Jaji Mkuu
wa Zanzibar na Tanzania, Brigedia Jenerali wa JWTZ pia amewahi kuwa Jaji
wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mahakama ya Afrika Mashariki, ambapo
amesema kazi ya sheria hazitofautiani na kazi za kiroho kwa vile zote
zinahitaji utende haki na kutimiza wajibu upasavyo. Kwa upande wake
Askofu Philip Baji wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha Dodoma, alisema
huu ni wakati mwafaka kwa Serikali kuwalinda viongozi wa dini bila ya
kujali tofauti ya madhehebu yao kutokana na kukithiri kwa vitendo vya
hujuma.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment