Luteni
Kanali Coelestine Seromba aneyedaiwa kutoroka ndani ya Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), bado hajulikani alipo hadi hivi sasa. Msemaji
wa JWTZ, Meja Erick Komba ameliambia gazeti hili jana kuwa kazi ya
kumtafuta Luteni Kanali Seromba inaendelea kimyakimya na kusisitiza kuwa
suala hilo halihitaji kutangazia umma wamefikia hatua gani.
Komba alisema wanajeshi kadhaa walikimbia katika jeshi hilo lakini
hawajatangazwa na wao kama jeshi hawaoni sababu ya kufanya hivyo kwani
wana utaratibu wao. “Huyo Luteni Kanali Coelestine Seromba anayedaiwa
kukimbia ni mwanajeshi mtoro kama wanajeshi wengine watoro na pindi
atapopatikana atatiwa hatiani kama kanuni za jeshi zinavyosema,” alisema
Meja Komba.
Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusu kuchelewa
kukamatwa kwa Luteni Kanali Seromba, Meja Komba alisema hatua za
kumfuatilia si lazima zitangazwe na pia mahali lilipofikia jeshi hilo
katika kumtafuta ni siri yao.
Meja Komba alisisitiza kuwa Luteni Kanali Seromba hakuondoka na nyaraka
yoyote ya jeshi hilo wala vifaa vyovyote kama inavyoripotiwa na baadhi
ya vyombo vya habari.
Komba aliwasihi waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi kwa
kuandika habari za kweli na zenye tija kwa pande zote ili kutojenga
chuki baina ya jeshi na taasisi zingine.
Alitolea mfano kuwa miaka ya hivi karibuni ambapo baadhi ya wanasiasa
walitamka wazi kuwa jeshi hilo linakula bure hivyo hakuna umuhimu wa
kutengewa bajeti kubwa huku wakisahau jukumu la jeshi hilo ni kulinda
amani ya nchi na mipaka yake ili wananchi waishi kwa usalama.
Meja Komba alitoa mfano wa vurugu zilizotokea bungeni hivi karibuni kuwa
kama Polisi wangeshindwa kudhibiti vurugu hizo hatua ya mwisho ilikuwa
jeshi kuingilia kati, lakini watu wanadai wanajeshi wanakula bure.
“Kikubwa ninachoweza kueleza hapa ni kalamu za waandishi kutumika vizuri
ili kutoweka chuki kati ya taasisi zingine likiwemo jeshi letu nje ya
nchi,” alisema Meja Komba huku akigusia namna msuguano kati ya viongozi
wa Tanzania na Rwanda ulivyoripotiwa.
“Mengi yaliyoripotiwa ni kama nchi hii na Rwanda zinaingia vitani na
uhasama huo kuhamia kwa wananchi na kujenga chuki na baadaye kuchukiana
na hata kuweza kugombana wenyewe kwa wenyewe,” alisema.
Pia aliwakumbusha wananchi kuendeleza amani iliyopo kwani vita vina
gharama kubwa na endapo nchi ipo vitani hata Bunge linaweza kusitishwa
kutokana na fedha nyingi kupelekwa katika mapigano.
Chanzo kimoja kutoka ndani jeshi hilo kimesema kutoroka kwa Luteni
Kanali Seromba aneyedaiwa kukimbilia Rwanda hakuwezi kuleta tishio
lolote ndani ya jeshi hilo.
Pia taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa kitengo
alichokuwa Luteni Kanali Seromba ni kitengo cha kawaida na kwamba
mafunzo yake hutolewa kimataifa na kila nchi ina mtu kama huyo.
CHANZO: Jambo leo
No comments:
Post a Comment