Matukio ya wananchi kumwagiwa tindikali yameendelea kushika kasi
nchini baada ya Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema wa
Mburahati Dar es Salaam, kumwagiwa kemikali hiyo mwishoni mwa wiki na
watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilus
Wambura alisema hana taarifa hizo licha ya tukio hilo kutokea mbele ya
Kituo cha Polisi Mburahati.
“Kwa sasa sina hizo taarifa, labda mpaka niulize,” alisema Kamanda Wambura.
Msema maarufu kama ‘Mnyalu’ amelihusisha tukio
hilo lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi
ambapo yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa)
kulitumia kuegesha magari yake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mburahati, Dickson Tungaraza
amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo“Mimi ninachojua hakuna mgogoro… wewe
uko wapi? njoo ofisini ndiyo utajua yote,” alisema.
Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
alikolazwa, alisema baada ya kufunga duka lake, watu waliokuwa kwenye
pikipiki ya matairi matatu (Bajaj) walimwagia kemikali hiyo na kutoweka.
“Ilikuwa saa mbili usiku baada ya kufunga duka
langu nikawa naelekea nyumbani, mara ikaja Bajaj ikasimama mbele yangu.
Mmoja wa abiria akaniuliza, vipi bosi, ndiyo unakwenda kuangalia kiwanja
chako? Nilipomwangalia ndiyo wakanimwagia tindikali,” alisema Msema na
kuongeza:
“Nilipiga mayowe wezi hao wezi hao! Lakini
walikimbia bila kukamatwa. Walikuja watu wakanimwagia maji na maziwa na
kuniwahisha hospitali.”
No comments:
Post a Comment