Thursday, October 11, 2012

LOWASA NA CHATANDA ARUSHA


article thumbnail

SIASA za makundi ndani ya CCM, zimeendelea kujidhihirisha wazi baada ya katibu wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda kukwepa kumtambulisha Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) kupitia Wilaya ya Monduli, Edward Lowassa aliyekuwa meza kuu.Tukio hilo la aina yake lilitokea jana wakati Chatanda akitambulisha wageni waalikwa na viongozi wa chama  na Serikali waliokuwa meza kuu katika mkutano wa uchaguzi wa nafasi ya  mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha.

Mara baada ya Msema Chochote (MC) kumpa kipaza sauti Chatanda, alianza kwa kuwatambulisha viongozi hao na kuwapa nafasi ya kusalimia, lakini ilipofika kwa Lowassa alimruka na kumkaribisha Mwenyekiti wa Mkoa aliyemaliza muda wake, Onesmo Nangole ili kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa mkutano huo, walianza kupaza sauti  huku wakisisitiza ‘bado mjumbe mmoja, bado mjumbe mmoja’  ndipo Chatanda alipomtambulisha Lowassa na kumkaribisha kusalimia wajumbe.
Mara baada ya Lowassa, aliyekuwa kiti cha mbele meza kuu, kusimama, ukumbi ulilipuka kwa maneno  ya CCM, CCM, CCM ambapo aliwapungia mkono hadi waliponyamaza.

Hata hivyo, Lowassa licha ya kusimama hakusema chochote hadi wajumbe hao waliponyamaza ndipo na yeye akaketi.Chatanda ambaye anatajwa kuwa katika kambi ya Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe, amekuwa akilumbana mara kwa mara na wana-CCM ambao wanamuunga mkono Lowassa katika chaguzi mbalimbali.Hata hivyo, baadaye jioni Lowassa alitambulishwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Jumanne Maghembe ambaye ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Nangole, Lowassa alisema inawezekana Chatanda alipitiwa kidogo kutokana na  hekaheka za chaguzi zilizopita na hasa baada ya watu aliokuwa anawataka kushindwa.
Hata hivyo, Lowassa alimpongeza katibu huyo kwa kazi nzuri alizofanya.


Kwa upande mwingine, Lowassa alimrushia dongo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuwa ni kijana mdogo, lakini hana shaka naye na  akasema kuwa ni mchapakazi  na anapaswa kusaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayoukabili mkoa huo.
Baadaye jioni mwandishi alimfuata Chatanda na kutaka ufafanuzi kuhusiana na hali hiyo ambapo alijibu kwa mkato kuwa “Sitaki maneno” na kupanda katika gari lake na kuondoka.Hata hivyo, baadaye alimpigia simu mwandishi na kusema, “ Mpaka ifikie mwanaume anitaje, mimi ni jembe na moto ni uleule.”

No comments:

Zilizosomwa zaidi