Wednesday, July 29, 2015

HII NDIO SIRI NZITO YA LOWASSA KUGOMBEA URAISI KUPITIA UKAWA

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa, aliweka masharti ya namna ya kupitishwa kuwa mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na hatimaye Ukawa, ili kukwepa mchujo mithili ya ule aliokumbana nao katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Masharti hayo ambayo yamefanikiwa kwa sehemu kubwa na akitarajiwa kuidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais baadaye wiki hii, yalimhakikishia mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, kutoshindanishwa na wanachama wengine “wenyeji” katika Chadema au wengine kutoka vyama vinavyounda Ukawa.
Pamoja na masharti hayo, taarifa za uhakika kutoka ndani ya vikao vya majadiliano kuhusu Lowassa katika Chadema na kisha Ukawa, zinabainisha kwamba naye amekubali kufuta mchakato wa Katiba Mpya ulioasisiwa na Rais Jakaya Kikwete, kama ataingia Ikulu.
“Aliweka masharti kadhaa, mojawapo ni kujihakikishia yeye mwenyewe anakwepa mchujo ama hali ya kushindanishwa na wanachama wengine wenyeji ambao wangeweza kujitokeza kuwania kuteuliwa wawe wagombea urais. Akasema anataka apitishwe bila kupambanishwa.
“Lakini pili, kati ya mambo ambayo alijifunga kwa Ukawa ni kwamba kama atashinda urais, basi atafuta mchakato wa Katiba Mpya wa Kikwete, ataanzisha mchakato mwingine mpya na hili ni suala ambalo limekuwa likisimamiwa kwa nguvu zote Ukawa,” alisema mtoa habari wetu huyo.
Inadaiwa kwamba hali ya kukwepa mchujo msingi wake ni msukumo wa wapambe wa Lowassa ambao baadhi bado wako ndani ya CCM wakilenga kuhakikisha mwanasiasa huyo anagombea urais na hata kushinda na kuapishwa kama Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kati ya wanasiasa ambao wangeweza kuhatarisha uwezekano wa Lowassa kuwa mgombea endapo mchujo wa wagombea wa nafasi hiyo ungefanyika ndani ya Chadema ni Dk. Wilbroad Slaa, huyu ni tishio na anakubalika ndani na nje ya wananchi, kwa hiyo ilikuwa ni Lowassa lazima aje na sharti hilo na amefanikiwa kuwa shujaa, ameshawishi viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa,” alisema mtoa habari wetu kutoka Chadema alitaka jina lake lihifadhiwe.
Hata hivyo, masharti hayo ya Lowassa kuepushwa na mchujo yanadaiwa kuanza kuzua mjadala ndani ya vyama vinavyounda Ukawa na katika hilo, mmoja wa wanasiasa wakubwa ndani ya Ukawa (jina linahifadhiwa) alizungumza na mwandishi wetu akisema; “Kuna wanachama wanataka mchakato wa kawaida wa kusaka mgombea urais uzingatiwe, watu wajitokeze kuchukua fomu, kuhojiwa na kupigiwa kura. Wanataka iwe hivyo ili kukiepusha Chadema na mwonekano wa kufinya demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa ndani ya Chama.”
Lakini wakati hayo yakiendelea, Raia Mwema limeelezwa kwamba wanachama wengine wenye ushawishi ndani ya Chadema wamejikuta katika wakati mgumu wa kukanusha mbele ya umma tuhuma walizowahi kuzielekeza kwa viongozi wa CCM, na hasa Lowassa kwamba ni fisadi.
“Kwa mfano Dk. Slaa, amekuwa akirudia mara kwa mara majukwaani kuhusu ufisadi wa Lowassa na alimtaja pale Mwembe Yanga Septemba 15, 2008. Slaa ni mtu ambaye background (rekodi) yake ni maadili ya kidini, amewahi kuwa padre, sidhani kama ni rahisi kwake kufuta kile alichokuwa akikiamini tena akisema anao ushahidi. Kwa ninavyomfahamu hili suala kama amekubali atakuwa amekubali kwa shingo upande, na hata Profesa Ibrahim Lipumba, naye najua hafurahishwi na hatua hii, hawa bado wanaamini nguvu za uadilifu za Ukawa zinatosha,” alisema kiongozi huyo mwandamizi, akihofu kwamba inaweza kuibuka nguvu ya chini kwa chini ya kumpinga Lowassa ndani ya Ukawa.
Hesabu ndani ya Ukawa
Chanzo chetu kingine cha uhakika cha habari kutoka Ukawa kinabainisha kwamba hadi kufikia uamuzi wa kumkubali Lowassa Ukawa, masuala kadhaa yalichukua sehemu kubwa ya mjadala miongoni mwa vyama vinavyounda umoja huo, kila kimoja kikitaka uhakika wa namna kitakavyonufaika, baada ya Uchaguzi Mkuu baadaye Oktoba 25, mwaka huu.
Suala mojawapo ni mgawanyo wa ruzuku baina ya vyama hivyo na namna Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atakavyoweza kuendesha ukaguzi wake bila kukutana na mazingira yatakayomlazimu kutoa hati chafu kwa vyama hivyo, na hasa katika mgawo wa ruzuku.
Kwa sasa ruzuku hutolewa kwa vyama vya siasa kwa kuzingatia vigezo kadhaa, ambavyo ni pamoja na idadi ya wabunge na hata kura za jumla za mgombea urais. Kwa mfano, kwa kuwa Ukawa wataweka mgombea urais na mgombea mwenza ambao ni lazima watokane na chama kimoja kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, na kwa kuwa ruzuku hugawanywa kwa vyama kwa kufuata idadi ya kura za mgombea urais kama mojawapo ya kigezo, sehemu ya ruzuku hiyo ni lazima ivifikie vyama vingine ndani ya umoja huo ambavyo haiba ya kila kimoja ilitumika kuvuta kura za urais.
“Sasa unapogawa ruzuku kutoka chama A kilichoipokea kwenda vyama vingine hapo ni lazima mazingira tata yanaibuka pale CAG atakapokagua hesabu za chama husika. Hapo kutakuwa na kuchakachua taarifa bila shaka ili mambo yaende vizuri kuepuka hati chafu,” kilieleza chanzo chetu hicho cha habari.
Mwenendo wa Lowassa
Katika mwaka huu, Lowassa amekuwa akitoa kauli mbalimbali ambazo ziliashiria kwamba hawezi kuhama CCM lakini pia isingefikiriwa kama ataweza kupinga mchakato wa Katiba Mpya ambao ulizaa Katiba Inayopendekezwa aliyoipigia kura ya NDIO katika Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo, sasa amegeuka, amekwishaahidi kufuta mchakato huo wa Katiba Mpya ambao vyama vinavyounda Ukawa vimekwishautangaza kuwa ni “haramu.”
Lakini vile vile mwisho mwa mwezi Mei, mwaka huu, akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma, Lowassa aliwaambia waandishi wa habari na baadhi ya wahariri aliokutana nao kwamba; hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema hatahama na endapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, basi, ni vyema huyo anayemchukia ndiye akahama.
Katika mkutano wake huo ambao aliutumia pia kuzungumzia mwenendo wa afya yake, aliulizwa kuhusu kujiunga upinzani endapo angeondolewa katika kinyang’anyiro cha urais, naye akajibu; “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwanaCCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM. Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.”
Kuhusu CCM kama taasisi, Lowassa alisema chama hicho kimefanya mambo mazuri; “Sisi ni chama dola tumefanya mambo mazuri, lakini tusibweteke wenzetu wanajiandaa vizuri na sisi tunapaswa kujiandaa vizuri. Vyama vingi vilivyoleta ukombozi sehemu nyingi vimeshaondolewa mfano UNIP, Kanu na mkishaondolewa hamrudi madarakani, meseji yangu kubwa kwa chama changu tusifanye mchezo, tusibweteke badala yake tufanye kazi kubwa zaidi.”
Kutokana na hali hiyo, taarifa zaidi zinabainisha kwamba uongozi wa juu wa CCM umekwishaanza mikakati ya kujipanga kudhibiti wimbi la wanaCCM watakaohama chama hicho kumfuata Lowassa.
Hatua hiyo ya CCM inakuja huku Ijumaa ya wiki hii majina ya watangaza nia ya kugombea ubunge kupitia chama hicho yakipigiwa kura na wanachama katika kila kona ya nchi, ikielezwa kwamba baadhi ya watakakosa kura za kuwafanya wawe wagombea watamfuata Lowassa kwenda kuimarisha kampeni zake za kusaka urais, dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli

Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Zilizosomwa zaidi