Thursday, September 25, 2014

MECHI YA SIMBA NA YANGA KUAHIRISHWA


 
Ule mpambano uliokua ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki na wapenzi wa soka kote nchini hususani mashabiki wa timu za Simba na Yanga lililokua lifanyike Octoba 12 mwaka huu katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam limesogezwa mbele
Kusogezwa mbele kwa mtanange wa watani wa jadi Simba na Yanga umetokana na sababu kubwa moja kuwa siku hiyo timu ya Taifa ya tanzania taifa stars itakua na majukumu ya kimataifa
Ambapo timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka huu kuikabili Benin katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Programu ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya mechi hiyo itatangazwa baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya mechi hiyo ikiwemo usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 28.
Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Wakati huo huo, kutokana na mechi hiyo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inafanyiwa marekebisho madogo, na marekebisho hayo yatatangazwa kesho (Septemba 26 mwaka huu).

No comments:

Zilizosomwa zaidi