Monday, July 7, 2014

HII NI KUHUSU SIKUKUU ZA SABA SABA

Tarehe kama ya leo mwaka 1954 TANU ilizaliwa. Mkutano wa uzinduzi wa TANU ulihudhuriwa na kikundi kidogo cha takriban watu 20 miongoni mwao Julius Nyerere, Abdulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia, Mshume Kiyate, Makisi Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Clement Mtamila, Rajabu Diwani, Schneider Plantan, Marsha Bilali, Rashid Ally Meli, Frederick Njiliwa, Iddi Faiz Mafongo, Iddi Tulio, Denis Phombeah na wengineo.
Julius Nyerere alichaguliwa rais wa TANU tarehe 17 Aprili, 1953; badala ya Abdulwahid Sykes ambae ni mtoto wa Kleist Sykes.
Kasella Bantu ndiyo mtu aliyempeleka Julius Nyerere kwa Abdulwahid kumtambulisha. Hii ilikuwa mwaka wa 1952. Bantu na Nyerere walikuwa wakijuana toka huko nyuma walipokuwa wakifundisha Tabora.
Ally Sykes ndiye aliyechora kadi ya TANU na kuchagua rangi na nembo yake. Rangi alizochagua zilikuwa nyeusi ikiwakilisha taifa la Kiafrika na kijani kwa ardhi ya Tanganyika. Mfano wa kadi ya TANU ilitokana na kadi yake ya Tanganyika Legion. Baada ya kumaliza kuichora ile kadi, aliwaendea Tanganyika Standard Newspapers ili wamchapishie.
Kutoka mfukoni mwake mwenyewe alichapisha kadi 1000 za kwanza na akitumia fedha za TAGSA alichapisha kadi nyingine 2000. Kadi nambari 1 ilitolewa na Ally Sykes kwa rais wa TANU, Julius Kambarage Nyerere na Ally aliweka sahihi yake kama afisa aliyeitoa. Ilipendekezwa kwamba kadi chache za mwanzo lazima zipigwe mnada na fedha zitakazokusanywa zitiwe kwenye hazina ya chama. Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na wengine walipanda dau kununua kadi hizo. Ally alimshinda kaka yake Abdulwahid kwa bei akapata kadi ya TANU nambari 2; Abdulwahid alipewa kadi nambari 3; Dossa Aziz kadi nambari 4; Phombeah kadi nambari 5; Dome Okochi, mmoja wa wale wazalendo kutoka Kenya katika TANU alipata kadi nambari 6 na Rupia kadi nambari 7. Bibi Titi kadi nambari 16; Iddi Tosiri kadi nambari 25.
Mara baada ya kuundwa kwa TANU ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulikuja Tanganyika mnamo Agosti, 1954. Kamati kuu ya TANU iliwakilisha madai yake kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukizuru Tanganyika.
TANU ilionyesha katika madai yake kuwa kwa Waafrika wa Tanganyika suala muhimu sana kwao lilikuwa kutafuta uvumbuzi wa ule mgogoro wa ardhi ya Wameru kwa njia za amani. Uzito wa jambo hilo kwa TANU unaweza kuonekana katika maneno ambayo inasemekana yaliandikwa na Abdulwahid, Nyerere, Stephen Mhando na Earl Seaton.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Ukombozi wa Taifa letu. TANU ikamzaa CCM tarehe 5.2.1977. Mafanikio ya CCM yanatokana na nguzo imara iliyowekwa na TANU.
Na Yona Maro

No comments:

Zilizosomwa zaidi