Monday, July 7, 2014

KUNDI LA MRC LASHUTUMIWA KWA SHAMBULIZI NCHINI KENYA

Polisi wa kagua mwili wa mtu aliyeuliwa na washambulizi katika kijiji cha Hindi, Lamu Kenya
Polisi nchini Kenya inaeleza kwamba washambuliaji wamewauwa watu 29 huko Lamu na Tana River. Polisi inasema wahusika wa shambulio hilo ni wanachama wa kundi la Mombasa Republic Council-MRC ingawa kundi la wanamgambo wa Al-Shabab kutoka Somalia linadai kuhusika.
Vyombo vya habari vya kenya vinamnukuu naibu inspeka mkuu wa polisi Grace Kaindi akisema jumapili kwamba watuhumiwa wakuu ni wanachama wa MRC na kwamba malengo yao huwenda yakawa ni ya kisiasa, kikabila au suala la mashamba. "Kundi la kiasi cha watu 30 hadi 50 waliwashambulia maafisa wa polisi waliokua katika kituo cha polisi cha Gamba . kulikuwepo na mashambulizi makali. Na kundi moja la washambuliaji walifanikiwa kuingia ndani ya kituo na kuwauwa watu watano waliokua wanashikiliwa huko. Afisa moja wa polisi aliuliwa na wawili kujeruhiwa"
Kundi la wanamgambo la Al-shabab limedai kuhusika na mashambulizi ya jumamosi usiku sawa na ilivyohusika katika mauwaji ya Mpeketoni mwezi uliyopita.
Lakini serikali inakanusha madai hayo ikidai mashambulizi yamesababishwa na wanasiasa na kuzusha mjadala mkali nchini humo kutoka upinzani, pamoja na gavana wa Lamu kushikiliwa kwa siku 5 kabla ya kuachiliwa kwa dhamana baada ya hakimu wa Mombasa kusema polisi hawakuwa na ushahidi wa kutosha.
Katika shambulio la Hindi katika kaunti ya Lamu polisi inaeleza kwamba washambulizi walichoma moto nyumba kadhaa pamoja na kanisa moja kabla ya kuwauwa watu 12. Ripoti za alfajiri ya jumatatu kutoka Hindi zinaeleza kwamba wengi wa wanaume waliouliwa walihojiwa kwanza na washambuliaji kabla ya kuchinjwa.
Maafisa wa usalama Kenya watizama ubao mweusi uloandikwa maneno kuunga mkono MRC
Polisi wanasema wanawadhania wanachama wa MRC walihusika kwani walikuta maandishi ya kuunga mkono kundi hilo yameandikwa kwenye ubao mweusi wa shule uliowekwa katika njia panda huko Hindi na wanasema wanaendelea na uchunguzi wa kina.
Wakati uchunguzi ukiwa unafanyika juu ya mashambulizi hayo watalii wawili wa kirusi walishambuliwa na majambazi katika jengo la makumbusho la Fort Jesus mjini Mombasa na kumuua mmoja na wapili kujeruhiwa. Polisi inaeleza kwamba washambuliaji walimpiga mwanamke mmoja kwa risasi alipokataa kuwapa mkoba wake na polisi wanawatafuta washambuliaji.

No comments:

Zilizosomwa zaidi