Denis Mpagaze-Mwandishi wa Makala hii |
Ubabe, dharau, kejeli na unafiki ni dhambi ambazo
zinalitafuna Taifa letu kwa kasi zaidi ya upepo. Nchi yetu imegeuka kuwa kisima
cha ubabe, vitisho na dharau. Kitendo cha Mbunge wa Kasulu kuhoji mstakabali wa
nchi yetu na kuitwa tumbili ni ubabe, dharau na kejeli. Kitendo cha wananchi wa
Kigamboni kuhoji uhalali wa kuongezeka kwa
nauli ya kivuko na kuambiwa asiyeweza kulipa apige mbizi ni dharau.
Kitendo cha
wananchi kuambiwa maji sio mkojo kupatikana kila sehemu ni kebehi. Kitendo cha
wananchi kuuliza uhalali wa kigogo kutumia ndege ya serikali na kujibiwa
mlitaka atumie punda ni majivuno.
Kitendo cha waandishi wa habari kuhoji
mstakabali wa nchi yetu na kuishia kung’olewa kucha na meno bila ganzi ni
vitisho. Kitendo cha kusimama Bungeni na kukosoa bajeti na baadaye kuunga hoja
kwa asilimia zote ni unafiki.
Kitendo cha kuwaambia watanzania asiyeweza
kulipia umeme atumie kibatari ni dharau. Mwisho wa dhambi hii siku zote
hushangaza. Kwa nini nasema hivi?
Robert Kiyosaki kupitia kitabu chake cha Rich Dad
Poor Dad anasema kwamba historia ni mwalimu mzuri. Ni historia inayonipa nguvu
na ujasiri kusema kwamba matokeo ya ubabe, dharau, unafiki na kejeli siku zote
hushangaza. Bas twende pamoja katika kuthibitisha kauli yangu kwa kurejea
kumbukumbu katika historia.
Katika kitabu chake kiitwacho, “A Night to
Remember”cha mwaka 1976, uk 73 Walter Lord ameonesha dharau na majivuno
aliyokuwanayo mbunifu wa meli ya Titatic. Mbunifu huyo alipoulizwa na waandishi
wa habari kuhusu usalama wa meli hiyo kubwa kuwahi kutokea, alijibu “meli hiyo
ni kubwa kiasi ambacho hata Mungu hawezi kuizamisha”. Matokeo ya kauli hii
yaliishangaza dunia. Meli hiyo ilizama na kuacha huzuni kuu. Na hili ni funzo
kwa viongozi mliojaa dharau na mizaa mpaka kumkufuru hata Mungu. Acheni!
ITAENDELEA KESHO....
Na Denis Mpagaze
No comments:
Post a Comment