
Tumekuwa
na mazungumzo na wenzetu na hili jambo ni moja ya mambo ambayo
tumekubaliana kushirikiana, maana kila upande unahitaji mwenzake katika
kuikomboa nchi hii” Freeman Mbowe,Mwenyekiti wa Chadema( katikati)
Dodoma. Mvutano katika mchakato wa Katiba umeimarisha ushirikiano wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na sasa kuna mpango wa kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri Kivuli ambalo litawajumuisha wabunge wa vyama hivyo.
Baraza
la Kivuli la sasa linawajumuisha wabunge kutoka Chadema pekee, ambacho
kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni tangu kuanza kwa Bunge la 10,
Novemba 2010.
Mwenyekiti
wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe alithibitisha kuwapo kwa mpango huo na kwamba atapanga upya
baraza lake katika siku za mwanzo za Bunge la Bajeti linalotarajiwa
kuanza mapema mwezi ujao.
“Tumekuwa
na mazungumzo na wenzetu na hili jambo ni moja ya mambo ambayo
tumekubaliana kushirikiana, maana kila upande sasa umekubali kuwa
unahitaji mwenzake katika harakati za kuikomboa nchi hii,” alisema
Mbowe.
Taarifa
za kuwaingiza wabunge wa NCCR-Mageuzi na CUF katika Baraza la Mawaziri
Kivuli, imekuja wakati ambao vyama hivyo pamoja na wajumbe wengine
kadhaa wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa wameunda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Ukawa
ndiyo iliyowaongoza baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka nje juzi
kususia mchakato wa Katiba Mpya kutokana na kile ilichodai kuwa ni
kutoridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda.
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alithibitisha kuwapo kwa mpango huo:
“Kweli ninafahamu kuwapo kwa mpango huo, lakini niseme tu kwamba
mazungumzo haya hayakuanza sasa, yamekuwapo kwa muda mrefu kuona namna
ya kushirikiana,” alisema Mbatia.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alipoulizwa
hakukanusha wala kukubali kuhusu kuwapo kwa mpango huo, badala yake
alitaka atafutwe Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa
Lipumba hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake
ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.
Akizungumza
kupitia simu yake ya mkononi, kiongozi wa wabunge wa CUF, Habib Mnyaa
alisema hakuwa akifahamu chochote kuhusu mpango huo kutokana na
kutokuwepo nchini kwa siku kadhaa.
Pigo kwa CCM
Kuendelea
kuimarika kwa ushirikiano wa kisiasa hasa baina ya CUF na Chadema ni
pigo kwa chama tawala, CCM ambacho kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa
(SUK) na CUF Tanzania Visiwani.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment