Mkuu wa jeshi la anga la
Malaysia, amekanusha madai kuwa ndege ya Malaysia iliyotoweka,
ilionekana mara ya mwisho Magharibi ya rasi ya nchi hiyo, eneo ambalo ni
mbali zaidi na njia iliyostahili kupita.
Generali Rodzali Daud, amesema kuwa hawawezi
kupuuza uwezekano huo, lakini amesema madai kuwa mawasiliano ya ndege
hiyo yalinaswa na mtambo wa radar katika eneo hilo sio kweli.
Amesema
mawasiliano ya mwisho ya ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Kuala Lumpur
kuelekea Beijing yalinaswa katika rasi iliyoko kati ya Malaysia na
Vietnam.
Ndege na meli kadhaa zimekuwa zikitafuta mabaki
ya ndege hiyo katika eneo la bahari ya Malaysia, lakini hazijafanikiwa
kupata mabaki ya ndege hiyo.
Jeshi la Malaysia limesema kuwa, mtambo wake wa
radar unaashiria ndege hiyo iliyotoweka, ilielekea eneo la Magharibi,
mbali na njia iliyostahili kupita kabla ya kutoweka.
Ndege hiyo MH370 ilitoweka siku ya Jumamosi, baada ya kupaa ikiwa na abiria mia mbili na thelathini tisa.
Juhudi za kimataifa za kutafuta ndege hiyo zimepanuliwa na kuimarishwa.
Awali ilibainika kuwa watu wawili waliokuwa
wakisafiri kwa kutumia paspoti zilizoibiwa walikuwa raia wa Iran ambao
hawana uhusiano na kundi lolote la Kigaidi.
No comments:
Post a Comment