Tuesday, March 11, 2014

BUNGE LA KATIBA LAPITISHA KANUNI, MTIKILA NA MKOSAMALI WASUSIA

 
Wakati wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakipitisha Rasimu ya Kanuni za kuendesha Bunge hilo, suala la aina ya kura kwa ajili ya kuamua masuala mbalimbali, limekwama na litaamuliwa na wabunge baada ya kuanza kwa vikao rasmi vya Bunge hilo.
 
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa mvutano wa takriban wiki nne kuhusu rasimu, hasa kifungu cha 37 na 38 kinachoeleza aina ya kura kati ya wazi na ya siri.
Hata hivyo, wajumbe wawili wa Bunge hilo, Mchungaji Christopher Mtikila wa DP na Felix Mkosamali wa NCCR- Mageuzi walisusia kupitisha azimio la kukubali Kanuni za Bunge hilo, wakidai kusalitiwa katika uamuzi huo na wenzao walioko kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wajumbe na viongozi mbalimbali wa vyama vyenye ushawishi bungeni, kwa pamoja waliridhia na kulegeza misimamo yao ili upatikane mwafaka wa kutengeneza Katiba Mpya ndani ya wakati.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndani na nje ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, viongozi hao walisema masilahi ya Watanzania katika mchakato wa Katiba ni ya muhimu kuliko masilahi binafsi ya makundi.
Kinana asema
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahaman Kinana alisema pamoja na malumbano makali yanayoendelea katika Bunge la Katiba, anaamini sasa Katiba itapatikana.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana mjini Dodoma, Kinana alisema haoni tatizo katika malumbano hayo na kwamba anaamini yanatokana na mitazamo tofauti ya makundi wanayotoka wajumbe.
“Pale kila kundi lina msimamo wake, iwe Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, CCM na hata makundi katika kundi la wateule wa Rais. Ilikuwa ni lazima kushuhudia mivutano ya aina hiyo,” alisema Kinana na kuendelea: “Lakini mwisho wa yote, nawaasa wajumbe kuwa na moyo wa kuvumiliana kwa sababu lazima kila kundi litetee hoja zake kulingana na tathmini yake juu ya mwenendo wa siasa na matarajio yake ya baadaye.”
Alisema kwa msingi huo, haoni tatizo kwa CCM kuweka misimamo katika baadhi ya hoja, ingawa chama hicho pia hakitasita kulinganisha nguvu ya hoja zake na hoja za wengine.
Mtikila, Mkosamali wasusia
Mchungaji Christopher Mtikila na Felix Mkosamali ndiyo wajumbe pekee waliosusia kupitisha azimio la kukubali kanuni za Bunge hilo, wakidai kusalitiwa na wenzao walioko kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kuonyesha kutokukubaliana na uamuzi huo, Mchungaji Mtikila alisimama bila kuruhusiwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho na kuhoji sababu za kutopewa nafasi ya kuzungumza katika Bunge hilo.
“Kwa nini unanizuia kuzungumza, unataka nikuheshimu wakati heshima yangu unaivunja? Nataka kujua haki yangu, nataka unijibu, nataka kujua kwanini hutaki nizungumze hapa ndani,” alihoji.
Mtikila aliongeza kusema: “Unachagua watu wa kuzungumza unachofurahia wewe ndicho kina haki ya kuzungumzwa hapa ndani. Nataka kuzungumza ni haki yangu siyo kwa kupenda wewe ni haki yangu. Unawapa watu ambao mnakubaliana na kupitisha kanuni mbovu na wengine unatunyima kusema, siyo haki katika kutengeneza Katiba,” alisema.
Kwa upande wake, Felix Mkosamali aliwasha kipaza sauti na kusema hata yeye anashangaa hapewi nafasi ya kuzungumza anapoomba kufanya hivyo. Alimtuhumu Mwenyekiti kwa kuwapa fursa hiyo wajumbe ambao inaonekana walikubaliana naye kuunga mkono azimio.
Hata hivyo, Kificho aliwaomba radhi wajumbe ambao hawakupata nafasi ya kuzungumza, akisema orodha ilikuwa ndefu na kwamba isigewezekana kwa wote walioomba kupata fursa.
Wakati Mchungaji Mtikila na Mkosamali wakizungumza, baadhi ya wajumbe waliendeleza utamaduni wa kuzomea licha ya kwamba Kificho alishakemea hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge, Mkosamali alisema siyo sahihi Bunge hilo kupitisha kanuni ambazo hazina kifungu kinachoeleza namna ya kufanya uamuzi.
Mkosamali alisema kifungu cha 22(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinamtaka mwenyekiti wa muda kusimamia uandaaji na upitishwaji wa kanuni zote za Bunge Maalumu na siyo nusunusu.
Mbatia: Ilikuwa lazima tukubaliane
Mjumbe mwingine wa Bunge la Katiba, James Mbatia alisema ilikuwa ni lazima wakubaliane na kupitisha Kanuni za Bunge hilo ambazo katika mjadala wake, ziliwagawa wajumbe katika makundi mawili yanayopingana.
Alipoulizwa sababu za kukubali kupita kwa kanuni hizo wakati hazijakamilika, alisema: “Kila jambo linaundwa kwa maridhiano na hata mwafaka wa Zanzibar ulipatikana baada ya pande mbili zilizokuwa zikivutana kukubaliana.
Kwa upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba alielezea matumaini yake kuhusu kufikiwa mapema kwa maafikiano katika vifungu vya 37 na 38.
“Ninawapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na wewe (Kificho) kwa kutuletea kanuni zinazokidhi haja,” alisema.

No comments:

Zilizosomwa zaidi