
 Vurugu 
za aina yake zimezuka katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, baada ya
 watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wa Chadema kumzomea aliyekuwa Naibu 
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe.
Vurugu 
hizo zilihusisha wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Zitto na wale 
wanaompinga, ambao walikuwa wamebeba mabango ya kumsifia na wengine 
wakiwa wamebeba ya kumkashifu.
        
Katika 
vurugu hizo, baadhi ya wanachama hao waliamua kufanya doria isiyo rasmi 
ndani ya mahakama hiyo ya kuwasaka watu waliodai kuwa ni mamluki, huku 
wakimkamata askari kanzu, kabla ya kumpiga ngumi na kumchania shati mtu 
mmoja wakidai kuwa alikuwa akiwarekodi kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Tukio 
hilo la aina yake lilitokea jana asubuhi ambapo kundi la wanachama hao, 
huku baadhi wakiwa wamevaa nguo za kaki zinazotumiwa na chama hicho 
kufika katika mahakama hiyo kwa lengo la kusikiliza kesi ya pingamizi 
iliyofunguliwa na Zitto.
Mara 
baada ya kuwasili kwa Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, huku akiwa 
ameongozana watu kadhaa wakiwamo wanasheria wake na mabaunsa, wanachama 
hao walianza kumzomea huku baadhi wakimwita fisadi.
Hali hiyo
 iliibua zogo katika eneo la mahakama hiyo, hali iliyowalazimu maofisa 
kadhaa wa polisi kuingilia kati kwa kuamua kumchukua Zitto na kumhifadhi
 kwenye chumba maalumu na kumtoa saa 6 mchana kesi yake ilipoanza 
kusikilizwa. Baadhi ya mabango ya kumkashifu yalisomeka; Zitto 
tulimpenda, CCM imempenda zaidi, Zitto rudisha fedha za CCM.
Yale 
yaliyomsifia yalisomeka; Zitto kama Mandela na Zitto ni Mkombozi.Baada 
ya kumalizika kusikilizwa kwa kesi hiyo, saa 12 jioni wanachama hao 
walianza kurushiana ngumi, hasa baada ya kuibuliwa kwa mabango 
yaliyosomeka 'Zitto kwanza Chadema baadaye'.
Awali hali hiyo ilimfanya Zitto kutaharuki, huku mabaunsa wake wakijihami na kuanza kumlinda.
Baada ya 
Zitto kuhifadhiwa baadhi ya wanachama hao ambao waliingia kwa 
kuandikishwa majina yao getini, walianza kuwasaka watu waliowahisi kuwa 
mamluki, ambapo walimnasa askari kanzu na kuanza kumzonga wakimuhoji 
anapeleleza nini katika eneo hilo.
"Hapa 
tunataka kujua wewe ni nani na unataka nini hapa, maana hatukuelewi 
kabisa kwa nini unakuja kusikiliza mazungumzo yetu, jitambulishe," 
alisisika mmoja wa wanachama hao akimhoji askari huyo huku akiwa 
amemkandamiza ukutani,
"Tunajua wewe ni askari kwa nini hujavaa sare leo? Kisha unajichanganya kwenye kundi letu."
Kesi hiyo
 ilimalizika saa 12 jioni ambapo Zitto alitolewa chini ya ulinzi mkali 
wa polisi kwa kupitia mlango wa nyuma wa mahakama hiyo na kuwaacha 
wafuasi hao wakionyeshana ubabKabla ya kuanza kwa kesi hiyo, Mwanasheria
 Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alimwomba Jaji John Utamwa kuendesha kesi 
hiyo kwa lugha ya Kiswahili kwa kuwa inagusa sehemu ya masilahi ya umma,
 jambo ambalo liliibua shangwe kwa wafuasi wa chama hicho waliokuwa 
wamefurika katika mahakama hiyo.
Hata 
hivyo baada ya kesi kuanza kuendeshwa kwa lugha ya Kiswahili, Jaji 
Utamwa alilazimika kuikatiza, na kuwakemea wanachama wa Chadema baada ya
 sauti za kuguna kusikika wakati wakili wa Zitto, Albert Msando 
alipokuwa akiwasilisha hoja kuhusu msingi wa kesi hiyo.
" Nataka 
kuwakumbusha hapa mahakamani ni tofauti na sehemu nyingine sauti 
zinazosikika sizitaki, anayeona kwamba yanayozungumzwa hakubaliani nayo 
kama hawezi kunyamaza atoke nje vinginevyo hatua za kisheria 
zitachukuliwa," alisema Jaji Utamwa.
Kundi la 
Wanachadema hao huku wengine wakiwa wamevalia sare zao waliwasili 
mahakamani hapo ili kusikiliza kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Kabwe
 akiiomba Mahakama iwazuie Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Katibu Mkuu 
pamoja na Kamati Kuu ya Chadema jana kumjadili, kumchukulia hatua, 
uamuzi wowote wala kuhusu uanachama wake.
Msingi wa kesi
Juzi 
Zitto aliomba Mahakama hiyo kuzuia Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema 
kumjadili hadi rufaa yake aliyoikata kwenye Baraza Kuu la Chadema 
itakaposikilizwa na kuamuliwa na wazuiwe kumwingilia katika utekelezaji 
wa majukumu yake ya ubunge wa Kigoma Kaskazini .
Pia 
aliiomba Mahakama hiyo Kuu kumwamuru Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad
 Slaa ampatie nakala ya mashtaka na maelezo ya uamuzi uliofikiwa na 
Kamati Kuu Novemba 22, 2013 na kusababisha avuliwe nyadhifa zake ili 
aweze kupeleka rufaa yake Baraza Kuu la Chadema kupinga uamuzi huo.
No comments:
Post a Comment