
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha 
Mapinduzi (CCM) Mwigulu Nchemba, amemwonya Spika wa Bunge, Anne Makinda 
kuacha kutumia vibaya fedha za Serikali kwa kuwapa posho wabunge kwa 
ajili ya kwenda kwenye michezo nje ya nchi.
Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba 
Magharibi alitoa kauli hiyo juzi bungeni wakati akichangia Muswada wa 
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa bidhaa ya mwaka 2013 
iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salumu.
Mkuya katika maelezo yake alisema kuwa
 kodi hiyo imefutwa kwa laini za simu kwa mtu mmoja mmoja na badala yake
 imeongezwa katika kodi kutoka asilimia 14.5 hadi asilimia 17.
Katika mchango wake, mbunge huyo 
alionya kuwa kumekuwa na tabia ya kutumia vibaya fedha za umma jambo 
alilosema linaanzia ndani ya bunge.
"Naomba tukubaliane katika kubana 
matumizi, na hivyo ninakuomba Mheshimiwa Spika tuanze na ofisi yako 
achana na kutoa fedha kwa kuwapa wabunge kwa ajili ya kwenda Dubai kwa 
burudani,"alisema Nchemba.
Alisema umefika wakati ambao Serikali 
inatakiwa kufanya uamuzi wa kutumia fedha katika mambo muhimu ambayo 
yanaigusa jamii kuliko mambo ambayo hayana maana. Kwa upande mwingine 
aliwalaumu watendaji kuwa wameiangusha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi 
kwa kushindwa kutoa ushauri na usimamizi mzuri katika makusanyo ya kodi.
Kwa upande wake Mbunge wa kuteuliwa 
James Mbatia aliinyooshea vidole Serikali kuwa ndiyo iliyovuruga 
mchakato mzima wa makusanyo ya kodi ambayo muswada wake ulishapitishwa.
Mbatia alitoa sababu kuwa ndani ya Serikali wamekuwa wakiamua mambo lakini kwenye utekelezaji wake wanagawanyika.
No comments:
Post a Comment