Mkuu wa Majeshi Nchini, Davis 
Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema nao wametakiwa 
kujiuzulu kutokana na uozo uliobainika katika ripoti ya Operesheni 
Tokomeza Ujangili, iliyosababisha Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa
 mawaziri wake wanne.
Akizungumza na waandishi wa habari 
jana jijini Dar es Salaam katibu wa madiwani wa jiji hilo, Julian Bujugo
 alisema wakuu hao wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa wao ndio wanaotoa amri 
kwa askari wao na siyo mawaziri.
"Nao wanatakiwa kuchukua uamuzi wa 
kujiuzulu kama hatua ya kuonyesha uwajibikaji wao, askari wao wamefanya 
maovu makubwa," alisema. Alisema kama wakuu hao wa watakaidi agizo la 
madiwani watalipeleka suala hilo kwa Rais Kikwete.
"Watendaji wa Serikali ndio chanzo cha
 uonevu, hata mawaziri 'mizigo', nao wanatakiwa kujiuzulu. Alimtolea 
mfano Waziri wa Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Bujugo alisema 
ameshindwa kuwasimamia wakulima na kusababisha mvutano na vurugu katika 
Sekta ya Kilimo.(P.T)
Chiza alitajwa kama waziri 'mzigo' na Kamati Kuu ya CCM iliyokutana wiki mbili zilizopita chini ya uenyekiti wa rais Kikwete.
Bujugo ambaye ni diwani wa Kata ya 
Magomeni alisema mbali na wakuu hao wa ulinzi na usalama, pia wakuu wote
 wa wilaya waliohusika kusimamia operesheni hiyo nao wanapaswa 
kuwajibika kwa kuwa walijua na waliona wazi vitendo vichafu 
walivyofanyiwa wananchi lakini walikaa kimya.
Ripoti ya tume ya kuchunguza 
Operesheni Tokomeza Ujangili ilisomwa bungeni mjini Dodoma mwishoni mwa 
wiki iliyopita na mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembelii na kuwango'a
 mawaziri hao.
Waliong'olewa ni Waziri wa Maliasili 
na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk 
Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Waziri 
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, huku Waziri 
Mkuu, Mizengo Pinda akiwa njia panda kutokana na wabunge kuendesha 
mpango wa chini chini wa kupiga kura ya kutokuwa na Imani naye kwa 
maelezo kuwa ameshindwa kuwasimamia mawaziri wake.
Chanzo: Mwananchi 
No comments:
Post a Comment