Saturday, November 30, 2013

CCM: CHADEMA MRUDISHENI ITTO ILI KUNUSURU CHAMA

Godbless Lema
Godbless Lema
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ameeleza kushangazwa na jitihada za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe asichukuliwe hatua zaidi kwa madai ya kukinusuru chama kisisambaratike.
 
Lema alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kilombero.

Alisema kuwa CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani kinachowanyima CCM usingizi, walipaswa kufurahia kusambaratika kwao, lakini cha kushangaza viongozi wa chama tawala wamekuwa wakiwaasa wasimfukuze Zitto.

“Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wanalia wakitaka tupatane. Mbunge wao wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba naye analia kuwa CHADEMA tumefanya vibaya, tumrudishe Zitto.

“Sisi tunawauliza tukifanya vibaya ni faida kwao, kwanini wanalia. CCM wanalalamika CHADEMA hatuna demokrasia, ni chama cha kibabe, tumemwonea Zitto, kwamba tutapasuka. Hivi tukipasuka wao wataimarika sasa wanalia nini badala ya kufurahi?” alihoji Lema.

Naye Mwenyekiti wa madiwani wa Jiji la Arusha, Doita Isaya alikemea tabia ya baadhi ya walimu kuacha kufundisha ipasavyo muda wa kazi ili baadaye wafanye hivyo kwenye masomo ya ziada ya kujiingizia kipato.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro alisema kipaumbele cha kwanza cha CHADEMA ni elimu, ndiyo sababu kwa kipindi cha miaka mitatu walichoongoza halmashauri wameisimamia ipasavyo na kuhakikisha madarasa 51 yanajengwa. 
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Zilizosomwa zaidi