Vyombo vya habari nchini vimeandika historia ya aina yake ya
kupitisha azimio la kuwafungia kwa muda usiojulikana, Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni takriban wiki mbili tangu viongozi hao
kutumia mamlaka wanayopewa na sheria ya magazeti ya mwaka 1976,
kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kutochapishwa kwa madai ya
kuchapisha habari za uchochezi.
Wakati gazeti la Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, Mtanzania limefungiwa kwa siku 90.
Vilevile hatua hiyo imekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu viongozi hao
walifungie gazeti la wiki la MwanaHalisi pia kwa madai ya kuchapisha
habari za uchochezi.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri (TEF) jana, ilisema kuwa
uamuzi huo umefikiwa kwa pamoja na Jukwaa hilo, Chama cha Wamiliki wa
Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini
mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA Tan).
Wamo pia Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Klabu za Waandishi
wa Habari Tanzania (UTPC), Dar City Press Club (DCPC) na Tanzania Human
Rights Defenders Coalition (THRDC).
Hatua hiyo inamaanisha kuwa kuanzia jana, habari zozote zitakazotolewa
au kuwahusisha Waziri Mukangara na Mkurugenzi wa Maelezo, Mwambene,
hazitaandikwa ama kutangazwa na chombo chochote cha habari kwa muda
usiojulikana.
Hatua ya kuwafungia viongozi hao inafuatia kikao cha pamoja cha wadau
hao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam kutokana na hatua ya
serikali kuyafungia magazeti hayo.
Mukangara na Mwambene wamefungiwa kwa tuhuma ya kudharau na kufanya
uamuzi wa kuyafungia magazeti hayo bila kusikiliza hoja za upande wa
pili.
Wanadaiwa pia kutoa maneno yaliyolenga kupotosha umma kwa makusudi juu ya hatua ya kuyafungia magazeti hayo.
Wadau hao walieleza kusikitishwa na hatua ya serikali ya kupuuza kilio
chao cha kuomba kusitishwa kwa sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka
1976.
Vilevile wanalalamikia kudhoofishwa kwa mchakato wa kuibadilisha
sheria hiyo iliyotajwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992, kuwa
ipo kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hivyo tunasitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote
zitakazowahusisha au kuratibiwa na Waziri Mukangara na Mwambene hadi
hapo itakapotangazwa vinginevyo.
“Wadau wa habari tutaendelea kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976
kwa kupigia kelele kufutwa kwa sheria hiyo na kuongeza nguvu ya kisheria
mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Hali Halisi
Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo,” ilisema taarifa ya
TEF.
No comments:
Post a Comment