DK. Willibroad Slaa |
Amefafanua kuwa CCM inaua ubunifu wa vijana, kwamba asilimia 90 ya
wanafunzi wanafeli shuleni huku viongozi wa chama hicho wakiwahadaa
wananchi kwamba wanaleta maendeleo.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana alipozuru Shirika la Anga la Marekani
(NASA) huko Huntsville nchini Marekani, ambako anaendelea na ziara yake
ya kujifunza katika majimbo mbalimbali.
Akiongozana na mkewe, Josephine Mshumbusi, katibu mkuu huyo alilakiwa
na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Charles Frank Bolden Jr. pamoja na
watendaji wengine na kupata fursa ya kutembezwa sehemu kadhaa.
Dk. Slaa alifika hapo kujifunza mambo mbalimbali, ikiwamo namna ya
kuwashirikisha na kuwapa vijana wa Kitanzania changamoto ili waweke
jitihada zaidi kwenye masomo ya sayansi, waweze kuinyanyua Tanzania
kutoka kwenye shimo la umaskini.
Taarifa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimnukuu Dk.
Slaa akisema kuwa wanasayansi wa Kimarekani walifika mwezini baada ya
kupata changamoto kutoka kwa aliyekuwa Rais wao, John F. Keneddy,
aliyewaomba wanasayansi hao kufikisha mtu mwezini chini ya miaka 10.
Alisema kuwa wanasayansi hao walimjibu na kufika mwezini chini ya
miaka minane. Hali aliyodai ilitokana na Serikali ya Marekani kuipa
kipaumbele elimu.
Dk. Slaa alisema kuwa baada ya uhuru, hayati Mwalimu Nyerere aliipa
kipaumbele elimu kwa ujumla. Akitolea mfano kwamba aliwachukua vijana
watano wanajeshi na kuwapeleka nchini Ireland kusomea mambo ya uhandisi.
“Waliporudi walipelekwa Kibaha ambako walibuni na kutengeneza gari la kwanza lililoitwa Nyumbu, ambalo ni ubunifu wao.
“Baadaye Mwalimu Nyerere aliwabunia wanajeshi hao mradi wa dhahabu wa
Buhemba, ambao ungewawezesha kulipia gharama za kutengeneza magari
mengi,” alisema.
Katibu mkuu huyo aliongeza kuwa kwa bahati mbaya baada ya Mwalimu
kustaafu, mafisadi walijipenyeza na kuuchukua mradi huo. Kwamba huo ndio
ufisadi uliozaa Meremeta.
“Mradi wa Nyumbu ukafa na kilichotokea ni ufisadi wa sh bilioni 155
uliohusisha Benki ya Netherlands ya Afrika Kusini. Hadi leo hakuna
maelezo licha ya fedha hizo kutumika kwenye kampeni za CCM za mwaka
1995,” alisema.
Dk. Slaa alihoji ni maendeleo gani wanazungumzia CCM wakati watoto
hawajui kusoma wala kuandika, huku wanajeshi waadilifu, wabunifu,
wazalendo na wanaojituma wamefikia kuishi maisha ya ajabu.
“Ubunifu wao kama mradi wa Nyumbu umeuawa na CCM, imefanya maisha yao
kuwa magumu na ya kusikitisha. Wanajeshi waliostaafu wamebaki kama
ombaomba.
“Wale wanaoshiriki kulinda amani nje ya nchi wanadhulumiwa hela zao
pale wanaporudi Tanzania. Nchi ambayo haiwezi kuwahudumia wanajeshi wake
ni nchi isiyofaa kuwa katika ramani ya dunia,” alisema.
Dk. Slaa aliwaomba wanajeshi na vijana kutokata tamaa wala kusikitika
kwani CHADEMA inasikia vilio vyao, na kwamba wanatambua kuwa ugumu wao
wa maisha umesababishwa na CCM.
“Wakati hao CCM wanajineemesha na hela zetu za kodi, wanajeshi na
wananchi kwa ujumla wanashindwa hata kujenga nyumba ya kujisitiri punde
wanapostaafu,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM imeua ubunifu ndani ya Tanzania na kuamua kuwaweka vijana kuwa mazezeta ili waendelee kuwatawala.
“Wenzetu wanapeleka watu mwezini, lakini Watanzania hata wembe
tunanunua kutoka nje kwa sababu ya CCM. Wakiendelea kuwanyima wananchi
haki zao za msingi muda utafika watachoka,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment