TUKIO la kigaidi lililotokea nchini Kenya katika jengo la
biashara la Westgate, limeizindua Tanzania na hivyo wamiliki wa majengo
makubwa ya biashara likiwemo Mlimani City jijini Dar es Saalam kuimarisha
ulinzi.
Tangu kutokea kwa tukio hilo linalodaiwa kutekelezwa na kundi la
kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia na kusababisha vifo vya watu 67
na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa, nchi za Afrika Mashariki zimeanza
kuchukua tahadhari kubwa katika kukabiliana na vitendo hivyo.
Tanzania Daima Jumapili jana lilishuhudia msafara mkubwa wa magari
uliokuwa ukiingia katika jengo lenye maduka mbalimbali ya biashara la
Mlimani City yakifanyiwa upekuzi wa kina, huku madereva wakitakiwa
kuteremka na kuyaacha tupu.
Aidha, baadhi ya wafanyakazi wa jengo hilo waliovalia vifaa maalumu
walikuwa wakivipitisha chini ya magari yaliyoingia katika jengo hilo kwa
umakini wa hali ya juu tofauti na siku za nyuma ambazo watu waliingia
na kutoka bila kukaguliwa.
Mmoja wa kiongozi wa ukaguzi huo ambaye ni raia wa kigeni, alionekana
kuwa makini na kuwataka wateja wote walioingia na magari yao ndani ya
eneo hilo kuyaweka pembeni ili yafanyiwe upekuzi.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa madereva, Juliaus Janco alisema
kuwa ni vyema utaratibu huo ukawekwa katika kila jengo lenye msongamano
wa watu ili kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea, hasa katika kipindi
hiki cha uwepo wa magaidi.
Alisema kuwa pamoja na baadhi kuonekana kukerwa na utaratibu huo,
lakini wanapaswa kuelewa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hofu
iliyojengeka sasa, hasa watu wanapoingia katika majengo kama hayo.
Katika hotuba yake ya juzi, Rais Jakaya Kikwete pia aligusia tukio
hilo la kigaidi la Kenya akisema kuwa anafahamu kuwa baada ya tukio hilo
watu wengi nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama.
“Ni hofu ya msingi kwani Agosti 8, 1998, Ubalozi wa Marekani hapa
nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia
walipoteza maisha,” alisema.
Alisema kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, serikali imekuwa ikijenga
uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja
mbalimbali.
“Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na
Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili
hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa,”
alisema.
Rais aliongeza kuwa baada ya tukio la Kenya, vyombo vya ulinzi na
usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Kwamba pamoja na kujizatiti
hawawezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.
“Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri
yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na
wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
“Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya
watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa waweke kamera
za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao,” alisema.
Pia aliwataka waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal
detectors and x-rays). Kwamba anajua watu wanaweza kulalamikia usumbufu
au gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi
kuliko ya usumbufu huo.
Kenya yataja watuhumiwa ugaidi
Wakati huohuo, habari kutoka Nairobi, Kenya zinasema kuwa nchi hiyo
imetoa majina ya watu wanne ambao inasemekana walifanya shambulio dhidi
ya jengo la maduka la Westgate wiki mbili zilizopita.
Watu ambao wote ni wanaume, walionekana kwenye picha za kamera za
usalama zilizopatikana Westgate baada ya jengo hilo kushikiliwa na
Al-Shabaab kwa siku nne.
Msemaji wa jeshi aliwataja watu hao kuwa ni Abu Baara al-Sudani, Omar Nabhan, Khattab al-Kene na Umayr.
Taarifa zinasema kuwa wawili kati yao wana uhusiano na al-Qaeda na
mmoja ana uhusiano na wapiganai wa al-Shabaab ambao walikiri kuhusika na
shambulio la Westgate.
No comments:
Post a Comment