Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuvisihi vyama vya
CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kusitisha maandamano yao na kurejea meza ya
mazungumzo ili kupata muafaka wa muswada wa sheria ya kubadili sheria
ya mabadiliko ya katiba, vyama hivyo vimetoa masharti mazito ya kukutana
naye.
Hatua hiyo inakuja wakati vyama hivyo vikiendelea kushikilia msimamo
wao wa kuitisha maandamano ya nchi nzima kupinga muswada huo, wanaodai
kuwa unalenga kuipa CCM nafasi ya kuhodhi mchakato wa katiba mpya.
Wakati vyama hivyo vikiwa vimefanya mikutano ya ndani na makundi
mbalimbali, na kisha mikutano miwili ya hadhara Dar es Salaam na
Zanzibar, CCM nayo inakazana kumshinikiza rais asaini muswada huo kama
ulivyopitishwa na Bunge.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwepo mvutano mkali ndani ya CCM,
ambako makundi ya vigogo wanaotajwa kugombea urais mwaka 2015,
wanampinga Rais Kikwete kwa jinsi anavyoendesha mchakato huo, wakidai
anawabeba wapinzani.
Licha ya wadadisi wa masuala ya kisiasa kumtabiria Rais Kikwete kuwa
anaweza kujiandikia historia nzuri endapo mchakato huo ukifanikiwa kwa
kuzingatia matakwa ya wananchi, CCM inamtazama mwenyekiti huyo kama
anataka kuwakomoa wenzake.
“Kuna msuguano mkali ndani ya CCM, Rais Kikwete ana nia njema na
mchakato huu ili ukamilike kwa amani, lakini wenzake ndani ya chama
wanadhani anataka kuwanufaisha wapinzani kwani hatakuwa na chochote cha
kupoteza,” alisema kigogo mmoja wa CCM.
Ni katika nia njema hiyo Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa
mwezi, aliwasihi viongozi wa vyama vitatu vya upinzani kutoandamana,
badala yake wakae na kutafuta njia mbadala ya kisheria kuboresha muswada
huo, na kwamba serikali iko tayari kuwasikiliza.
Hata hivyo, wito wa Rais Kikwete umepokelewa kwa taswira tofauti na
vyama hivyo, vikisema kuwa yeye ndiye anapaswa kuwaandikia barua
kuwaomba akutane nao kwa mazungumzo Ikulu, kwani wao hawajawahi kuomba
kukutana naye.
Badala yake, vyama hivyo vilisisitiza kuwa viliomba kukutana na wadau
mbalimbali na wananchi kumshinikiza asisaini muswada, na kwamba msimamo
wao uko pale pale.
Katika msimamo huo, vyama hivyo vimesema maandamano yaliyotangazwa
kufanyika Oktoba 10 nchi nzima yako pale pale, na kamati ya maandalizi
inaendelea kufanya taratibu zote.
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam, wawakilishi wa vyama hivyo,
John Mnyika (CHADEMA), Faustine Sungura (NCCR-Mageuzi) na Abdul Kambaya
(CUF), walisema kuwa kamati ya maandalizi ya maandamano inaendelea kwa
kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake hakugusia suala lolote kama
atasaini muswada huo au la.
“Rais amezungumzia hoja za upinzani za kuvunjwa kwa Tume ya Jaji
Joseph Warioba kabla ya kumaliza muda wake, kwa hili tunampongeza,
amekuwa wazi. Lakini afahamu kuwa hiyo si hoja kuu iliyosababisha
tuandae maandamano kushinikiza asisaini huo muswada.
“Mambo mengine mazito yapo, kuhusu muundo wa Bunge la Katiba na idadi
ya wajumbe kwa uwiano sawa wa Zanzibar na Tanganyika na kuhusu maoni ya
wadau kuachwa,” alisema Mnyika.
Alisema kuwa maoni ya wadau yamepuuzwa, uchakachuaji umefanyika,
taasisi zilipeleka majina, lakini Rais Kikwete anasema kuwa alizingatia
hilo, kwamba wanamwomba aseme kwanini hakuchukua jina kati ya yale
yaliyopendekezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),
Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu (Shiwavyata) na CCT.
Alisema kuwa hao walijitokeza kwenye kamati wala hawakusema kwa siri,
hivyo Rais Kikwete awaambie mawaziri wake wamwambie ukweli.
Alihoji kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake ametumia neno
‘nimeambiwa’ kwa kiasi kikubwa, kwamba ingefaa mawaziri wake hasa Waziri
wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi; Waziri wa Sheria na Katiba,
Mathias Chikawe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu,
Stephen Wassira na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Sophia Simba wamwambie ukweli.
“Huyu huyu rais ndie aliwaambia wafanyakazi wakati wa mgomo wao kuwa
akili za kuambiwa na viongozi wao wachanganye na za kwao, kwanini katika
mambo aliyoambiwa na wasaidizi wake hakujiridhisha kwanza?” alihoji.
Hivi karibuni, Waziri Wassira aliwakejeli wapinzani kuwa wasitarajie
tena kukaribishwa Ikulu, kutokana na msimamo wao wa kususia mjadala wa
muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013.
Alisema kuwa maandamano yaliyokuwa yanaandaliwa kumshinikiza rais
asisaini muswada huo, hayana maana kwani rais hana sababu za kutousaini.
Licha ya Wassira kudai milango ya wapinzani kuzungumza na rais katika
suala hilo imefungwa, Rais Kikwete amewasihi wapinzani wakae na serikali
wajadili kasoro zilizopo kwenye muswada kama walivyofanya mwaka 2011
wakati mchakato unaanza hatua ya kwanza.
Hata Waziri Chikawe naye alimtisha rais hivi karibuni kuwa iwapo
ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia
saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge
kutokana na chombo hicho kukamilisha kazi yake.
Lakini rais amewapuuza mawaziri wake hao na kutumia busara akisema
kuhusu hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutokufanya vikao
Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau, saula hilo lilianzia bungeni hivyo
linaweza kurudishwa huko lijadiliwe tena.
Kuhusu rais kumwandama Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu kuwa
alisema uongo bungeni, Mnyika alisema hakufanya vema kumshambulia mbunge
huyo kwani hayo hayakuwa mawazo yake binafsi bali maoni ya kambi ya
upinzani.
“Inakuwa sio vizuri mbunge aliyetoa mawazo bungeni kwa mujibu wa
katiba na kanuni za Bunge kushambuliwa kwa maneno makali na rais wakati
alikuwa anatoa mawazo ya kambi wala si yake,” alisema Mnyika.
Lissu ajibu
Akizungumza na gazeti hili, Lissu amehoji hotuba ya Rais Kikwete
iliyojaa neno “nimeambiwa” akisema ana uhakika gani wale waliomwambia
kama hawakumdanganya?
“Maneno yaliyotajwa na rais kuhusu uteuzi wa wajumbe toka Shirikisho
la Vyama vya Wenye Ulemavu, TEC na CCT yalizungumzwa kwenye kamati sio
maneno yangu. Kikwete hakuwepo kwenye kamati, mimi nilikuwepo. Sasa
mawaziri wake na wabunge wake wa CCM wamwambie ukweli, waache
kumdanganya.
“Kikwete amesema mimi ni muongo, mnafiki, lakini hoja ambazo
tulizipinga mfano ya ushiriki wa wadau wa Zanzibar, hata Waziri wa
Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakari Khamisi naye ameniunga mkono.
Je, na huyu ni mzushi, muongo na mfitini?” alihoji.
Aliongeza kuwa hoja ambayo rais anakimbilia kwamba alimzuia asiteue
wajumbe 166, ilikuja bungeni mwaka 2011, wakaipinga, ikaondolewa. Lakini
mwaka huu wameirejesha tena.
No comments:
Post a Comment