Wakati klabu ya Simba ikidhihirisha kuwa imekwama kujenga
uwanja, uongozi wa Yanga umeanza visingizio na kudai kuwa serikali ndiyo
inayowakwamisha kuanza kwa ujenzi wa uwanja wao wa Kaunda.
Ujenzi wa viwanja katika klabu hizo mbili kubwa na
zenye mashabiki wengi zaidi nchini ni sawa na tamthilia maarufu ndefu
ya Afrika Kusini ya Isidingo ambayo haifikii tamati.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga
aliliambia gazeti hili jana wameandika barua muda mrefu serikalini ili
wapate kibali cha Serikali cha kuongeza eneo la uwanja huo.
Yanga ipo katika mikakati ya kuujenga uwanja wake
wa Kaunda ili uweze kuwa wa kisasa zaidi na kuwa katika nyasi bandia
ambapo awali walieleza kuwa ungeanza mwezi Juni ukiwa unagharimu Sh32
bilioni.
“Ramani ya uwanja ambayo wametupa Wachina inaingia
sehemu kidogo ya uwanja wa wazi wa serikali, ni muda mrefu sasa
tumeandika barua watuongezee kipande kilichozidi lakini bado
hawajatuambia chochote ndio maana tumesimama.
“Tumekwama hata kusaka vyanzo vya mapato kwa ajili
ya uwanja ila kwa sasa tumeshapata mtu wa masoko atashughulikia,”
alisema Sanga muda mfupi baada ya kumtangaza George Simba kuwa mmoja wa
watu muhimu katika sekretarieti ya Yanga katika kusaidia kuboresha
mapato ya klabu hiyo.
Alisema Simba ndiye atakayefanikisha mapendekezo
ya uongozi kwa wanachama ya kuchangia Sh250 kila mmoja kila wiki kwa
lengo la kupata Sh8 bilioni, kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwamo
makusanyo ya ada za uanachama, michango mbalimbali, harambee, kalenda
na mauzo ya jezi na bidhaa zenye nembo ya Yanga pamoja na kusaka taasisi
mbalimbali za kibenki kwa ajili ya kuwezesha kukamilika kwa ujenzi wa
uwanja huo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Makazi, Goodlucky Ole Medeye aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa
hawajapokea barua yoyote ya Yanga ya kuomba kupewa sehemu hiyo ya
Jangwani na kwamba iwapo itawafikia hawana pingamizi.
Yanga ipo katika mikakati ya kuujenga uwanja wake
wa Kaunda ili uweze kuwa wa kisasa zaidi na kuwa katika nyasi bandia
ambapo awali walieleza kuwa wangeanza ujenzi mwezi Juni.
Desemba mwaka jana uongozi wa Yanga ulitoa ahadi
ya kuijengea klabu hiyo uwanja wa kisasa na Januari mwaka huu
ukamtangaza mkandarasi, Kampuni ya Beijing Constructions Engineering
Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwamba ndiye
atakayejenga uwanja huo mpya wa Yanga.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ujenzi huo wa
uwanja utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 lakini
hadi sasa hakuna hata dalili za kuanza.
Kuhusu ukarabati wa jengo la Mafia na kuwa jengo la kitega uchumi la
klabu uliunda Kamati chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete kusimamia
suala hilo Sanga alisema “Kuna vitu vinakwamisha, kuna document
(nyaraka) mara nyingine zipo kwa huyu, nyingine kwa yule, ndio wanaoleta
ugumu, tutawaita wanaoshughulikia suala hili waje waweke wazi
walipofikia, lakini bado kuna vizuizi vingi.”
No comments:
Post a Comment