Mwanamke mmoja mfanyabiashara mjini Nairobi, Kenya,
ambaye alikiri kosa la kupanga njama ya kumuua mumewe, ameachiliwa na
mahakama
Bi Faith Wairimu Maina, aliachiliwa huru baada ya mumewe kuitaka mahakama kufuta kesi yake kwani amemsamehe.
Bi Faith alikiri kuwa aliwakodi
mamluki kumuangamiza mumewe. “Nataka kumsamehe kwa sababu ya watoto na
familia yetu,” mumewe Faith aliambia mahakama.
Mwanamke huyo alikiri makosa ya kupanga njama ya
kutaka kumuua mumewe baada ya kukamatwa ingawa baadaye alibadili
msimamo wake na kukanusha madai hayo na alitarajiwa kushtakiwa.
Polisi walitibua njama ya mwanamke huyo baada ya
majasusi waliokuwa wanajidai kuwa mamluki kupokea malipo ya shilingi
40,000 kuitekeleza njama hiyo.
Mwendesha mkuu wa mashtaka alisema kuwa
alifahamishwa wanandoa hao walikubali kusameheana na kuwa bwana Muthee
ambaye ni mumewe mwanamke huyo akataka kesi hiyo kufungwa.
Wakili wa mwanamke huyo alisema kuwa hakuwa na
pingamizi zozote kutupilia mbali kesi hiyo. Bwana Muthee alisema kuwa
mwanamke huyo ni mkewe na alimsamehe kwa sababu ya familia, jambo
linaloruhusiwa na mahakama.
Mwanamke huyo tayari alikuwa amewalipa mamluki
kumuua mumewe na kisha kuwataka wamletee nguo zake zenye damu ili aweze
kuwalipa pesa zitakazokuwa zimesalia ambazo ni shilingi 160,000 na pia
aweze kuthibitisha kuwa mumewe ameuawa.
Majajusi walisema kuwa ilikuwa mara ya pili kwa
mwanamke huyo kujaribu kumuua mumewe baada ya njama ya kwanza kukosa
kufaulu licha ya kuwalipa mamluki waliomwambia kuwa walishikwa na uoga.
Mwanamke huyo alipanga njama ya kumuua mumewe kutokana na madai kuwa alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine.
BBC
No comments:
Post a Comment