HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili ina uwezo wa kufanya tiba zote za
upasuaji wa magonjwa ya moyo na hakuna tena haja kwa Serikali kupeleka
wagonjwa wote wa maradhi hayo India, imeelezwa.
Kutokana na uwezo huo, uongozi wa hospitali hiyo umeiomba Serikali
fedha inazotumia kutibu mgonjwa mmoja nje ya nchi dola 10,000 za
Marekani, ili kupeleka wagonjwa hao hospitalini hapo iwatibu kwa dola
6,000.
Akizungumza hospitalini hapo jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi
Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela, alisema wametoa ombi hilo
kwa maelezo kuwa iwapo Serikali itatumia kituo cha moyo cha Muhimbili,
fedha inazotumia kutibu wagonjwa wa moyo nje ya nchi zitaiwezesha
kuimarika zaidi.
Muhimbili imepata uwezo huo baada ya baadhi ya madaktari wake kupata
mafunzo India na Israeli na tangu huduma hizo zianze mwaka 2008 wagonjwa
453 wenye maradhi ya moyo wamefanyiwa upasuaji.
“Upasuaji wa moyo unaofanyika katika hospitali yetu ni sawa na
upasuaji unaofanywa katika vituo vikubwa vya upasuaji moyo duniani
kote,” alisema jana Dk Njelekela.
Miongoni mwa huduma zinazotolewa na hospitali hiyo katika kitengo
hicho cha moyo ni upasuaji wa kuziba matundu kwenye moyo, kubadilisha
valvu ambazo zimebana na kushindwa kuruhusu damu kupita kwenye moyo au
kulegea na kufanya damu kuvuja kwenda sehemu isiyohusika na kurudisha
moyo katika hali yake ya kawaida ya afya.
Njelekela pia alisema pamoja na kufanya upasuaji, huduma nyingine
ambazo zinafanywa na kituo hicho cha moyo ni kliniki za magonjwa ya
valvu, moyo kupanuka, mishipa kuziba, mapigo kushuka, magonjwa ya moyo
ya kuzaliwa kwa watoto na upasuaji moyo na mishipa ya damu.
Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa hadi Aprili, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ilipeleka wagonjwa 402 kupata matibabu nje ya nchi.
Kati yao, 189 walikuwa na matatizo ya moyo, 39 saratani, 34 figo na
140 magonjwa mengine. Wagonjwa hao ni ambao matibabu yao yalishindikana
nchini.
Vifaa vya kisasa
Dk Njelekela alisema kituo hicho kina vifaa vya kisasa na vya hali ya
juu na mahususi kumudu matibabu ya magonjwa makubwa ya moyo.
“Tunaendelea kutafuta taasisi zenye uzoefu mkubwa wa matibabu ya moyo
ili kuanzisha ushirikiano utakaowezesha kupata wataalamu wao kuja
kushirikiana na wa nchini ili kutibu magonjwa makubwa ya moyo kama njia
ya kuongeza uwezo kitaaluma.
Alisema Serikali imetoa fedha kununulia mtambo mkubwa wa kuchunguza
mishipa na shinikizo ndani ya moyo na maradhi makubwa ya moyo ya
kuzaliwa.
“Huu ndio mtambo ambao kwa kipindi kirefu umekuwa ukisababisha
Serikali kupeleka wagonjwa wengi wa moyo India,” alisema Dk Njelekela na
kuongeza kuwa mtambo huo ambao umenunuliwa kwa Sh bilioni 3.6 ulifungwa
hivi karibuni na wataufanyia majaribio mwezi ujao.
Alisema ndio unaosaidia kuangalia mishipa ya damu inayokwenda kwenye
moyo na kuangalia moyo unavyofanya kazi na pia kama mtu anatakiwa
kufanyiwa upasuaji.
Gharama za matibabu
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali hiyo, Agnes Kuhenga
alisema mgonjwa mwenye rufaa kutoka hospitali za mikoa atatibiwa kwa Sh
10,000 kumwona daktari, Sh 20,000 akilazwa na akifanyiwa upasuaji
atalipa Sh 50,000.
Habari leo
No comments:
Post a Comment