Wakati Operesheni Kimbunga inayoondoa wahamiaji haramu nchini
ikiendelea, raia wa Rwanda, France Mathias amejinyonga wilayani Kyerwa,
Kagera baada ya mkewe kumgomea kuuza mali na kuondoka nchini.
Tukio hilo lilitokea juzi katika kitongoji cha Kikukulu wilayani humo
ambapo binti yake, Melania, alithibitisha tukio hilo akidai kuwa tangu
operesheni hiyo ianze, wazazi wake hao wamekuwa kwenye mzozo mkubwa.
Kutokana na mzozo huo, “baba alitaka wauze mali na kuondoka nchini,
lakini mama akampinga na kisha usiku akatoroka na watoto watatu,” alidai
Melania na kusema mama yake ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, Tanzania na
kwamba kuna wakati baba yao alitishia kuwaua.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikukulu, Joseph Leo alipozungumza na
mwandishi wa habari hizi, alithibitisha Mathias kuwa katika orodha ya
wahamiaji haramu iliyoandaliwa na uongozi wake na kwamba amekuwa
akifahamu kuwapo ugomvi mkubwa ndani ya familia hiyo.
Pia alisema anafahamu baba yake alikuwa na uwezo wa kumiliki kiasi
hicho cha fedha ingawa hakufahamu anapozihifadhi na kuwa upo wakati
alitishia kuwaua baada ya kuibuka mzozo kwenye familia yao.
Alisema yeye alikuwa miongoni mwa viongozi waliofika juzi kwenye eneo
la tukio na kushuhudia Mathias ambaye alifika eneo hilo mwaka 1976
akiwa amejinyonga, huku vipande vya noti za Sh 5,000 na Sh 10,000
zinazokadiriwa kufikia Sh milioni saba vikiwa vimetapakaa chini.
Ofisa Tarafa ya Kituntu, Nicholaus Rugemalira, alisema Mathias
alikuwa raia wa Rwanda na kwamba eneo alilojinyongea kulikutwa pia
kiberiti na panga hali iliyoashiria kuwa pengine alikuwa na mpango wa
kuiteketeza familia yake kwa moto au kuiua kwa panga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alipoulizwa kwa
njia ya simu alisema alikuwa hajapata taarifa kamili juu ya tukio hilo
ila atafuatilia na kutoa taarifa baadaye.
No comments:
Post a Comment