Msanii anayetamba na wimbo
wa Nai Nai, Me and You, na sasa Tupogo, Faraji Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz ameanika
hadharani siri za mafanikio ambapo amesema alijifunza muziki miaka
10, kabla ya kuingia rasmi katika muziki.
“Nilikuwa na ndoto za kuja kuwa mwanamuziki mkubwa
sana, lakini sikuwa na uwezo wa kuyafikia mafanikio hayo kwani sikuwa
na ujuzi wowote, lakini hivi sasa nashkuru Mungu kwani niliitumia fursa
ambayo leo hii imenipa mafanikio niliyokuwa nayaota.”
Ommy Dimpoz anayesisitiza wasanii wasikurupuke
kuingia kwenye muziki kabla ya ujuzi, amefafanua zaidi namna alivyoanza
kuonekana “Nilitumia miaka yangu mitano nikiwa chini ya mwanamuziki
Khalid Mohamed ‘TID’ huko nilijifunza yaliyo mengi ambayo yamenijengea
msingi imara.
“Unajua unapokuwa unajifunza unakuwa kama upo
gereji maana unalifungua gari na kulifunga upya, nilipopata fursa ile
niliitumia vilivyo sikuhitaji kunung’unika kwani nilijua nini nafanya na
nahitaji nini, japokuwa ni miaka mingi ila nilitoka pale nimeiva ndio
maana leo hii nasimama kama msanii ninayejitegemea,” anasema.
Amesema wasanii wengi wanaingia katika muziki kwa kukurupuka ndio maana wanashindwa kuhimili katika soko la muziki.
“Mfano mwingine ni Diamond, sisi ni wasanii
tuliojifunza kwa muda mrefu muziki ndio maana mpaka leo tupo vizuri,
nashukuru nilijifunza na wadau wa muziki nao wakaniona kupitia bendi
hiyo,” anasema.
Amefafanua kuwa wakati amefanya maamuzi ya
kujiengua katika bendi ile, alitoa wimbo wake mpya Nai Nai ambao anakiri
kuusambaza pasipo kutumia fedha yoyote.
“Nilisambaza Nai Nai bila kulipa gharama yoyote,
kila mtu aliyeusikia wimbo ule aliupenda, nilipigiwa simu na vyombo
mbalimbali vya habari wakihitaji nipeleke kazi zangu, haikuwa rahisi
kwangu kwa kuwa nilipata ujuzi kabla ya kuingia kwenye muziki.”
No comments:
Post a Comment